Flatnews

Wabunge Kupeleka Hoja Bungeni Serikali Ihamie Dodoma Rasmi.

Wabunge wa mkoa wa Dodoma wamejipanga kuwasilisha hoja binafsi bungeni ya kuitaka serikali kuhamia mkoani humo na utungwaji wa sheria...



Wabunge wa mkoa wa Dodoma wamejipanga kuwasilisha hoja binafsi bungeni ya kuitaka serikali kuhamia mkoani humo na utungwaji wa sheria ya kuutambua rasmi kuwa ni makao makuu ya nchi, kutokana na utekelezwaji wake kusuasua.

Wabunge hao walisema hayo mwishoni mwa wiki katika kikao chao cha pamoja na Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu Dodoma (CDA), ambacho lengo lake lilikuwa kujenga hoja za pamoja katika kuishawishi serikali kuhamia mkaoni hapa.




Kikao hicho kiliongozwa na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Dodoma, Adam Kimbisa na wabunge hao waliazimia kushirikiana ili suala hilo likubalike na kutekelezwa.

Mbunge wa Dodoma Mjini, Anthony Mavunde (CCM), alisema pamoja na jitihada hizo ni vyema CDA ikajiangalia upya katika utekelezaji wa majukumu yake ili kusiwapo na msuguano na wananchi.

Aliitaka CDA kuangalia upya gharama za upimaji wa viwanja ambazo asilimia kubwa ya wananchi wa kipato cha chini wanashindwa kuzimudu.

“Kama kuna maeneo ya kurekebisha, yarekebishwe sasa ili kuendana na kasi ya kuitaka serikali ihamie Dodoma ikiwa ni pamoja na gharama hizo kupunguzwa. Gharama ya chini ya upimaji kiwanja kwa sasa inaanzia Sh. 500,000 kiasi ambacho wanashindwa kukimudu.

Naye Mbunge wa Kibakwe, George Simbachawene (CCM), alisema mpango wa serikali kuhamia Dodoma upo, lakini umekuwa ukisuasua, hivyo inatakiwa nguvu mpya ya kulisukuma jambo hilo ili litekelezwe.

“Kwa muda mfupi iangaliwe namna CDA na Manispaa ya Dodoma zinavyoweza kushirikiana katika majukumu yao kutokana na kuwapo kwa mgongano wa kisheria juu ya uundwaji wa mamlaka hiyo na manispaa,” alisema.

Simbachawene aliitaka mamlaka hiyo kufanya kazi kwa karibu na wanasiasa ili kurahisisha ufikishaji wa elimu kwa wananchi na kuondoa malalamiko.

“CDA imefanya kazi katika mazingira magumu, lakini imesaidia Dodoma kuonekana mji wa tofauti kwani umepangika vizuri sana, kuna vitu vichache vya kurekebisha ili isionekane kama ni shetani (kero) kwa wananchi wa Dodoma,” alisema Simbachawene.

Naye Mbunge wa Kondoa Vijijini, Dk. Ashatu Kijaji (CCM), alisema yupo tayari kushirikiana nje na ndani ya Bunge ili Dodoma ifikie matarajio yake.

Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Felista Burra, alisema suala la serikali kuhamia Dodoma limekuwa likiwekewa mikakati, lakini limekuwa likikosa watu wenye dhamira ya dhati kulisukuma ili litekelezwe.

Alisema mchakato huo umekuwa ukikwamishwa na serikali, lakini anaamini hoja hiyo ikiwasilishwa bungeni wabunge wengi watasaidia utekelezaji wake ukamilike.

Kwa upande wake, Kimbisa alisema viongozi wa Dodoma wamekuwa wakilaumiwa na wananchi kwa kushindwa kuibana serikali ihamie mkoani hapa.

Alisema kilio cha watu wa Dodoma ni kuona inakuwa makao makuu ya nchi kama ilivyokwisha tangazwa na serikali.

“Wabunge mnategemewa sana kufanikisha jambo hili, kwani ndiyo mliopewa dhamana, maana hakuna mtu nje ya Bunge atakayeweza kufanikisha,” alisema Kimbisa.

Related

NEWS 5319646150398111756

Post a Comment

emo-but-icon

item