Sherehe 30 za Maadhimisho ya Kitaifa Mikononi mwa Magufuli
Sherehe 30 za maadhimisho ya kitaifa zinazofanyika nchini kila mwaka huenda ‘zikachinjw...
https://samchardtz.blogspot.com/2015/11/sherehe-30-za-maadhimisho-ya-kitaifa.html
Wasiwasi
wa kufutwa kwa maadhimisho hayo ya kitaifa umekuja baada ya Rais
Magufuli juzi kufuta maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani iliyopangwa
kuadhimishwa Desemba Mosi kabla ya hapo, alifuta sherehe za Uhuru ambazo
zingefanyika Desemba 9.
Rais
aliagiza kuwa fedha zitakazotumika kwenye maadhimisho ya Siku ya Ukimwi
Duniani, zitumike kununua dawa za kufubaza makali ya Virusi vya Ukimwi
(ARV) na zile za Siku ya Uhuru zitumike kwa usafi wa mazingira ili
kupambana na kipindupindu.
Katika
mwendelezo huo, jana Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue alipiga
marufuku utengenezaji na uchapishaji wa kadi za Krismasi na Mwaka Mpya
kwa gharama za Serikali.
Katika
taarifa yake, Balozi Sefue ameelekeza kuwa yeyote anayetaka kutengeneza
au kuchapisha kadi hizo, afanye hivyo kwa gharama zake na ameagiza
fedha zilizopangwa kugharamia utengenezaji na uchapishaji huo, zitumike
kupunguza madeni ambayo wizara, idara na taasisi za umma zinadaiwa na
wananchi na wazabuni waliotoa huduma kwao au zipelekwe katika matumizi
mengine ya kipaumbele.
Sherehe sasa kwa vipaumbele
Akizungumzia
kufutwa kwa maadhimisho ya sherehe za kitaifa, Sefue alisema Rais
Magufuli amechukua hatua hiyo kwa mamlaka aliyonayo kisheria na kuwa
hatua hiyo si endelevu, bali kwa kuangalia vipaumbele.
Sheria
ya Sikukuu za Kitaifa (The Public Holidays Act, Cap 35), inampa Rais
mamlaka ya kutangaza siku yoyote kuwa sikukuu au mapumziko.
Kutokana
na sheria hiyo, ndiyo maana Rais Mstaafu, Jakaya Kikwete alitangaza
Novemba 5 mwaka huu, kuwa ya mapumziko katika kuhitimisha uongozi wa
awamu ya nne na kuukaribisha wa awamu ya tano.
“Maadhimisho
haya yana umuhimu lakini si lazima yafanyike kila mwaka, tunaweza
kuamua mwaka huu tufanye au turuke mwaka mmoja. Siku ya Ukimwi ina
umuhimu na siku ya Uhuru ina umuhimu pia, lakini tunapima kwa kuangalia
wapi kuna mahitaji zaidi,” alisema.
Alisema
uamuzi huo wa Rais ni njia mpya ya kupanga vipaumbele kutokana na hali
halisi ilivyo katika sekta zenye mahitaji makubwa na ya haraka.
Katika
hotuba yake ya kuzindua Bunge ya Novemba 20, Rais Magufuli alisema
Serikali itadhibiti warsha, semina, makongamano na matamasha ambayo
yanatumia fedha nyingi za lakini hayana tija.
Alisema atahakikisha kila senti inayoongezeka katika mapato ya Serikali inaelekezwa katika kutoa huduma bora zaidi kwa wananchi.
“Tutaziba mianya ya upotevu wa fedha za Serikali ambayo inaipunguzia Serikali uwezo wake wa kuwahudumia wananchi,” alisema katika hotuba hiyo.
Baadhi
ya maeneo ambayo alisema yatasimamiwa ili kupunguza matumizi yasiyo ya
lazima na kuziba mianya ya uvujaji wa fedha za Serikali ni kufuta safari
za nje, posho za kujikimu na kodi.