Bunge Kuondoa Ajira za Kudumu Serikalini.....Kudumu Kwa Ajira Ya Mfanyakazi Kutategemea Juhudi Zake Kazini
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania litafanyia mabadiliko makubwa sheria za utumishi wa umma kwa kuondoa ajira za kudumu...
https://samchardtz.blogspot.com/2015/11/bunge-kuondoa-ajira-za-kudumu.html
Bunge
la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania litafanyia mabadiliko makubwa sheria
za utumishi wa umma kwa kuondoa ajira za kudumu serikalini, ili
kuwezesha mabadiliko yaliyokusudiwa na Rais Dk. John Magufuli.
Katika
mabadiliko hayo, mfumo sasa wa ajira za serikali kuwa za kudumu
utabadilishwa na badala yake, kudumu kwa ajira ya mfanyakazi kutategemea
juhudi na bidii yake kazini, ili kuondoa uzembe uliodumu miaka nenda
miaka rudi, katika sekta ya umma.
Akizungumza
katika mahoajino binafsi na gazeti la Raia Mwema, mjini Dodoma
mwishoni mwa wiki iliyopita, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Job Ndugai, alisema baadhi ya sheria za kazi zinawafanya
baadhi ya watumishi wa umma kuwa wazembe.
“Kwa
mfano katika serikali ya sasa mfanyakazi mzembe kabisa kabisa hata
waziri kumfukuza kazi hawezi. Hata Katibu Mkuu hawezi mpaka afuate
mlolongo mrefu na hatua nyingi sana, yaani kazi ni guarantee (uhakika)
katika nchi yetu ni permanent and pensionable (ya kudumu na ina
pensheni). Sheria za namna hiyo lazima ziondoke,” alisema Spika Ndugai .
“Katika
nchi ambazo zinaendelea kwa haraka moja ya jambo ambalo huna uhakika
nalo ni ajira, ukifanya vizuri unayo ajira yako ukiboronga unaondoka saa
hiyo hiyo na wakati huo huo, sasa sheria za namna hiyo ni lazima
zibadilishwe ili watu wachape kazi. Wawe wakijua kabisa kwamba nipo kwa
sababu nachapa kazi akileta uzembe kazini kwaheri,” aliongeza.
Aliongeza
kuwa mabadiliko mengine ambayo Rais Magufuli atayaleta ni pamoja na ile
sheria ya ununuzi na sheria nyingine ambazo ni za hovyo hovyo,
zinazoifanya serikali isifanye vizuri. Kwa mujibu wa Ndugai, Bunge
litahakikisha sheria hizo zibadilishwa haraka.
“Huo
ndiyo ushirikiano wetu tutakaompa lakini pia tutachangia vizuri katika
mipango na bajeti zinazokuja tutazitengeneza vizuri zaidi kwa kupunguza
fedha zote za ulaji ulaji, hii ya kila mwaka mapazia, kuweka makochi,
kuweka makapeti na kompyuta kila mwaka na ofisi ni zile zile watu wale
wale, bajeti ilikuwa imejaa ununuzi wa magari vilainishi lazima tukate
kote huko,” alisema.
Akizungumzia
hatua hiyo, Rais wa Shirikisho la Vyama wa Wafanyakazi Tanzania
(TUCTA), Gratian Mukoba, alisema hawezi kuunga mkono au kukataa hoja
hiyo mpaka atakapoona hoja yenyewe na maelezo yake.
“Kwa
kawaida muswada wa sheria huanzia kwanza kwa wadau, wakituletea
tutaona, siyo kila kitu ni kibaya, sheria zinapotungwa zinakuwa na
sababu kwa nini zimetungwa. Unaweza ukawa na maelezo mazuri tukajadili
utekelezaji wake, tutaamua,” alisema.
Alipoulizwa
kuhusu mwenendo wa baadhi ya watumishi wa umma kufanya kazi kwa mazoea
na kama sheria hiyo inaweza kutibu tatizo hilo, alikiri kuwepo kwa hali
hiyo miongoni mwa watumishi wa umma lakini akatahadharisha kwamba tiba
yake siyo kuondoa ajira za kudumu.
“Ziko
sababu nyingi zinazosababisha baadhi ya wafanyakazi kuwa wazembe, siyo
ajira ya kudumu peke yake. Kama kwenye nchi yenu mmeamua kubaguana kwa
malipo, mmoja analipwa mara 30 ya mwingine, huyo anayelipwa kidogo
hawezi kuwa na morali ya kazi, atanyong’onyea.
“Yule
anayepata mara 30 ataathiriwa utendaji wake na hawa wenye kidogo kwa
sababu ni wengi, kwa sababu watajifanya (wanaolipwa kidogo) na serikali
itajifanya inalipa lakini kumbe kinacholipwa hakitoshelezi chochote,” alisema Mukoba.
Aliogeza
kwamba miaka ya 1970 na 1980 watu walikuwa na uhakika wa ajira za
kudumu lakini walikuwa wanachapa kazi kwa bidii kwa kuwa kulikuwa na
uwiano wa haki kwenye malipo ya mishahara, tofauti na sasa, akishauri
pia suala la kushuka kwa morali ya kazi miongoni mwa watumishi wa umma
lifanyiwe utafiti makini na si kulikurupukia.
Chanzo: Raia Mwema