Flatnews

Marekani Yaipa Kibano Tanzania .....Yaitaka Serikali itoe Maelezo Uchaguzi Zanzibar na Sheria ya Mtandao , Yatishia kusitisha Msaada wa Trilioni ...BOFYA HAPA KUSOMA ALICHOKISEMA OBAMA.

Mfuko wa Changamoto za Milenia (MCC) wa Marekani umeonya kuwa hali ya kisiasa Zanzibar na tukio la hivi karibuni la watu kukam...



Mfuko wa Changamoto za Milenia (MCC) wa Marekani umeonya kuwa hali ya kisiasa Zanzibar na tukio la hivi karibuni la watu kukamatwa chini ya sheria mpya ya uhalifu mtandaoni yanaweza kuathiri vigezo vya kuiwezesha Tanzania kupata msaada.

Katika barua ya MCC ya Novemba 19, ambayo imesainiwa na Naibu Makamu wa Rais wa Idara ya Operesheni ya Miradi kwa Afrika, Jonathan O. Bloom kwenda kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dk. Servacius Likwelile, mfuko huo umetaka maelezo kuhusu utatuzi wa mgogoro wa Zanzibar pamoja na ufafanuzi wa sheria ya uhalifu wa mtandaoni.

“MCC inashukuru kwa uongozi na dhamira yako wakati wa mchakato mzima wa maendeleo ya mradi huu. Msaada wa dola milioni 472 (ambazo ni zaidi ya Sh trilioni moja), una nafasi kubwa ya kusaidia kuleta mageuzi katika sekta ya nishati na kuwaunganisha maelfu ya watu katika gridi.

“Lakini mgogoro wa Zanzibar na ukamataji watu wa hivi karibuni kupitia sheria mpya ya uhalifu mtandaoni umetutia wasiwasi.

“Kama ujuavyo, mataifa washirika wa MCC wanapaswa kuendeleza na kuonyesha dhamira ya utawala bora, ambayo ni pamoja na kufuata misingi ya demokrasia na kulinda uhuru wa kutoa mawazo. 
 
"Hata hivyo, matukio ya karibuni yanaifanya MCC na wadau wetu kujawa na maswali kuhusu dhamira hiyo,” inasomeka barua hiyo ya MCC iliyosainiwa na Bloom.

Kwa mujibu wa barua hiyo, MCC inafuatilia kwa karibu nyendo za Serikali katika ushughulikiaji wa masuala hayo ya utawala bora, hasa kipindi hiki kuelekea mkutano wa mwezi ujao wa bodi ya mfuko huo.

“Utatuzi wa mgogoro wa Zanzibar kwa namna ya kuridhisha pande zote husika na haja ya kuiona Serikali ikifafanua hadharani nia yake na sheria ya uhalifu wa mtandaoni, kama vile kuchapisha utekelezaji wa kanuni zinazoakisi mchango wa mdau na kuonyesha dhamira ya kuendelea kulinda uhuru wa kutoa maoni, kutaisaidia MCC kuitathimini Tanzania kwa namna chanya juu ya kuendelea kwa dhamira yake ya kutimiza sharti la kufuzu kupata misaada,” ilisema barua hiyo.

Barua hiyo ilimalizia kwa kusema: “Wasiwasi huu ni kikwazo cha mipango yetu ya ushirika. Tunaamini utashughulikia wasiwasi huu ipasavyo na tunatarajia kupata jibu kutoka kwako.”

Alipotafutwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dk. Likwelile, hakupatikana na hata alipotafutwa kwa njia ya simu hakupokea.

Pamoja na juhudi hizo, pia alipotumiwa ujumbe mfupi wa simu hakujibu, ambapo alipotafutwa Msemaji wa Wizara ya Fedha, Ingiahedi Mduma, kuhusu barua hiyo ya MCC, alisema hana taarifa na hajaiona.

“Sina taarifa na wala sijaiona barua hiyo, hivyo siwezi kusema chochote labda mpaka nitakapoongea na bosi aniambie kama amepokea barua hiyo,” alisema Mduma.

Mwanzoni mwa Oktoba mwaka huu, Rais mstaafu Jakaya Kikwete akiwa nchini Marekani kuhudhuria shughuli za Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UN), alikutana na Mtendaji Mkuu wa MCC, Dana J. Hyde na watumishi waandamizi, akiwamo Makamu wa Rais wa Operesheni za mfuko huo, Kamran Khan.

Katika mkutano huo, MCC ilitangaza kuwa Tanzania imetimiza masharti yote ya kupatiwa awamu ya pili ya fedha za maendeleo kutoka katika mfuko huo, kuanzia mwakani, zaidi ya dola za Marekani milioni 472.8, sawa na zaidi ya Sh trilioni moja za Tanzania.

Katika mkutano huo, Rais mstaafu Kikwete, aliambatana na ujumbe wa maofisa kadhaa akiwamo Waziri wa Fedha wa Zanzibar, Yusuf Omar Mzee.

Katika awamu ya kwanza ya fedha za MCC, Tanzania ilipata dola za Marekani milioni 698 (sawa na Sh trilioni 1.46).

Kama MCC wataridhika na maelezo ya Serikali kupitia Wizara ya Fedha, Tanzania itakuwa imepata jumla ya Sh trilioni 2.45 kwa awamu zote mbili kwa ajili ya miradi ya maendeleo katika kipindi cha miaka 10.

Awamu ya kwanza ya fedha hizo zilitumika kujenga Barabara za Tunduma- Sumbawanga, Tanga-Horohoro na Namtumbo- Songea- Mbinga.

Desemba 10, mwaka jana, Marekani pia ilibainisha hatua ya uamuzi wa utolewaji wa fedha za awamu ya pili za MCC utategemea hatua zitakazochukuliwa na Serikali kuhusu sakata la uchotwaji wa zaidi ya Sh bilioni 200 katika akaunti ya Tegeta Escrow.

Uamuzi huo wa Marekani ambayo inafadhili miradi mingi ya mabilioni ya fedha nchini, ulionekana kama mtihani  wa pili kwa Rais mstaafu Kikwete, baada ya ule wa maazimio ya Bunge yaliyotaka viongozi wakiwamo mawaziri waliotajwa katika kashfa hiyo kuwajibishwa.

Waliowajibishwa na Rais Kikwete ni aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa, Sospeter Muhongo na aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka.

Wengine ni aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakimu Maswi na aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema.
Chanzo: Mtanzania

Related

NEWS 5522200500844707636

Post a Comment

emo-but-icon

item