Wazee Wamzawadia Lowassa Ng’ombe Kumuunga Mkono Katika Harakati Zake za Kugombea Urais
Baraza la wazee Wilaya ya Nyamagana na Ilemela jijini Mwanza, limempatia Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa ng’ombe wawili iki...
https://samchardtz.blogspot.com/2015/04/wazee-wamzawadia-lowassa-ngombe.html
Baraza la wazee Wilaya ya Nyamagana na Ilemela jijini Mwanza, limempatia
Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa ng’ombe wawili ikiwa ni sehemu ya
kumuunga mkono katika harakati zake za kugombea urais kupitia Chama Cha
Mapinduzi(CCM), muda ukifika.
Akizungumza wakati wa hafla fupi iliyofanyika mwishoni mwa wiki
iliyopita jijini hapa, wakati wa kupokea mrejesho wa Umoja wa Shirika la
Machinga Mwanza(SHIUMA), waliokwenda wilayani Monduli, mkoani Arusha
kumshawishi Lowassa kuchukua fomu, Mjumbe wa baraza hilo, Yakokumya
Chota alisema wameamua kutoa ng’ombe hao kama ishara ya kumuenzi
Lowassa.
Alisema baraza la wazee ndani ya wilaya hizo, limeamua kumpatia ng’ombe
hao wa kienyeji kwa ajili ya kuwatumia kama kitoweo kwa ajili ya wageni
wanaofika nyumbani kwake kuzungumza naye na kumtia moyo kuhusu kuwania
urais kupitia CCM.
“Tulitamani tuandamane sote kwenda Monduli, lakini wengine umri wetu ni
mkubwa hatuwezi tena kusafiri umbali mrefu, lakini tumefarijika sana na
uwakilishi wetu kwa Lowassa, sisi wazee tunamuunga mkono kwa asilimia
mia moja.
“Pamoja na vikwazo anavyokumbana navyo tuna uhakika atafanikiwa kupenya,
tunaamini katika utendaji kazi wake wa kusimamia maamuzi kwa niaba ya
wnaanchi, ndio maana tumeamua kumuunga mkono kwa nguvu zote,” alisema.
Hata hivyo, wazee hao waliwaomba vijana kuandaa utaratibu wanaona unafaa
kwa ajili ya kuwapeleka ng’ombe hao nyumbani kwa Lowassa.
Naye mlezi wa SHIUMA, Alfred Wambura alisema wamekuwa wakisikitishwa na
namna siasa ndani ya CCM zilivyogeuzwa kuwa za chuki, na kuwataka
viongozi wa ngazi za juu kuacha kuwachagulia wananchi viongozi.
“Siasa ndani ya CCM zimekuwa za kukomoana, viongozi wa ngazi za juu
wamekuwa wakiwachagulia wananchi viongozi hali ambayo imekuwa
ikisababisha chama kushindwa katika chaguzi mbalimbali, wanapaswa
kufuata upepo unavyokwenda na sio vinginevyo, Lowassa kwa sasa ndio
kiongozi anayekubalika,” alisema.