Athari 12 Za Sheria Mpya Ya Masuala ya Mitandao ( Tanzania Cybercrimes Act, 2015 ) Iliyopitishwa Bungeni......Athari Hizi Zimechambuliwa Na Mbunge David Kafulila
Sheria hii ni muhimu duniani kote na ndio maana hata Tanzania ilikuwa inangojea kupata sheria ya kuongoza masuala ya mitandao yaani ...
https://samchardtz.blogspot.com/2015/04/athari-12-za-sheria-mpya-ya-masuala-ya.html
Sheria hii ni muhimu duniani kote na ndio maana hata Tanzania ilikuwa inangojea kupata sheria ya kuongoza masuala ya mitandao yaani Cyber Law kutokana na uhalifu wa aina mbalimbali wa masuala ya mitandao.
Sifa kuu ya sheria ya kuongoza masuala ya mitandao ni kuweka bayana
makosa ya mitandaoni na pia kuyatolea adhabu. Sheria hii inayopitishwa
kwa dharura madhara yake ni:
Moja, Kifungu 7 (2b): Mpokeaji wa ujumbe (receiver) anaweza kushtakiwa
kwa kosa la kupokea ujumbe ambao sheria imeufanya kuwa wa jinai. (Mfano:
Mtu akikuforwadia ujumbe, ukiupokea na wewe umefanya kosa la jinai).
Pili, Kifungu 21(1): Mtumia mtandao wa Intaneti yeyote hayuko salama
kwani mtoa huduma wake analazimika kutoa habari zake kwa serikali pale
zitakapohitajika (kwa lazima).
Tatu, Kifungu 8: Itakuwa ni kosa la jinai kama mtu ataweka wazi nyaraka
za siri za serikali hata kama ni nyaraka ya kusaidia nchi kwa ujumla
(Mfano: Matumizi mabaya ya mali ya umma).
Nne, Kifungu 14: Picha yoyote yenye mwelekeo unaoweza kuonekana kama
‘mchafu kingono’ inaweza kupelekea mtu kufungwa hadi miaka 10 au kulipa
milioni 30; Sasa kama mtu kaweka picha yake Instagram ambayo sio ya
ponografia lakini ‘ikatafsiriwa’ hivyo. Sheria haijatafsiri ponografia!
Tano, Kifungu 23: Je, ulijua kuwa ‘kusababisha maudhi ya hisia’ kwa mtu
mwingine ni unyanyasaji na unaweza kufungwa kifungo kisichopungua mwaka
mmoja?
Sita, Rejea adhabu ya ibara mbalimbali: Sheria hii kila kosa linaweza
fanya mtu afungwe kifungo hadi cha maisha na kulipa pesa hadi
zisizohesabika kwani hakijawekwa kikomo cha juu cha adhabu bali kikomo
cha chini tu kwa Kiingereza “not less than”
Saba, Sheria haijaeleza vizuri suala la kutumia jina lisilo lako kwenye
mtandao na hivyo mtu anaweza kushitakiwa kama kuna mtu mwingine mwenye
jina kama hilo katika maisha halisi.
Nane, Serikali kupitia waziri husika ndio ina mamlaka ya kusema jambo
lililowekwa kwenye mtandao ni la kweli, uongo au la kupotosha. Kumbuka
hata ESCROW, EPA walisema ni uwongo; ni wangapi katika mtandao
wangeshtakiwa kiuonevu kwa hili?
Tisa, Kifungu 22: Ukiweka ujumbe katika mtandao na ukaufuta au
kuuboresha, kama ukishtakiwa kwa kuweka ujumbe huo unaweza kuhukumiwa
pia kwa adhabu ya kuuboresha au kuufuta. Ni mara ngapi unafuta ‘status’
zako za WhatsApp? Unaweza shtakiwa kwa kuchelewesha ushahidi kisa tu
ulifuta na hamna mtu anayeweza kujua ulifuta kwa kusudi au la.
Kumi, Mkuu wa kituo cha Polisi chochote kile nchini anaweza kuagiza wewe
umpatie simu/laptop yako au taarifa zako zote (kwenye email, chats) au
hata vifaa vyako au ofisi yako kwa ajili ya upelelezi bila oda ya
Mahakama.
Kumi na moja, Kifungu 31 (3a): “As soon as practicable” the law states.
Askari Polisi wakichukua vitu vyako wanaweza kukupatia listi ya vitu
walivyovipokea muda watakaoona kwao inawezekana kufanya hivyo. Jiulize,
inaweza chukua muda gani?
Kumi na mbili, Kifungu 31-35 & 39-45: Kama wewe ni Blogger au mtoa
huduma ya mtandao, pale unapobaini kosa ukalitoa na uko katika mikakati
ya kuitaarifu mamlaka husika (Kama sheria inavyosema), askari naye
anaweza kwa wakati huohuo akaja kukagua na kuchukua vitu vya kazi zako,
hivyo sheria inakinzana yenyewe kwa yenyewe. Blogger yuko sawa kisheria
na askari yuko sawa kisheria.
Je, sheria hii ikisainiwa na Rais Jakaya Kikwete tutapona?
DAVID Kafulila
Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi)