Toleo la kwanza la Charlie Hebdo lachapishwa baada ya shambulizi
Toleo la kwanza la jarida la vikaragosi la Ufaransa la Charlie Hebdo limechapishwa leo (14.01.2015) kwa mara ya kwanza tangu lilipotokea...
https://samchardtz.blogspot.com/2015/01/toleo-la-kwanza-la-charlie-hebdo.html
Toleo la kwanza la jarida la vikaragosi la Ufaransa la Charlie Hebdo
limechapishwa leo (14.01.2015) kwa mara ya kwanza tangu lilipotokea
shambulizi la kigaidi katika ofisi za jarida hilo na kuwaua watu 12.
Jarida hilo la kila wiki limechapishwa likiwa na picha ya kikaragosi cha
Mtume Mohammed, katika ukurasa wake wa juu. Jarida hilo limechapisha
nakala milioni tatu, huku likiwa na kikaragosi cha mtume Mohammed
akitokwa na machozi akiwa ameshika bango lenye maandishi yanayosema ''Je
Suis Charlie', yaani ''Mimi ni Charlie''. Aidha, jarida hilo lina
kichwa cha habari kinachosema, ''Yote Yamesamehewa.''Jarida hilo limeuzwa katika maeneo mengi ya mji mkuu wa Ufaransa, Paris, dakika chache baada ya kuingia sokoni. ''Je Suis Charlie'' ni msemo unaotumiwa na mamilioni ya wananchi wa Ufaransa na ulimwenguni kote, baada ya waandishi wa habari na wachora vikaragosi wanane wa jarida hilo na watu wengine wanne, kuuawa wiki iliyopita.
Kwa kawaida jarida hilo huchapisha nakala 60,000, na litapatikana pia katika lugha za Kiingereza, Kihispania, Kiitaliano, Kiarabu na Kituruki. Wauzaji wa magazeti wamesema mahitaji ya jarida hilo yalikua makubwa kuliko ilivyo kawaida. Mchora vikaragosi Renald Luzier, amesema alilia baada ya kuchora ukurasa wa kwanza wa gazeti hilo, likiwa ni toleo la kwanza tangu lilipotokea shambulizi hilo.
Hata hivyo, toleo la leo limepata maoni tofauti, ambapo Kituo Kikuu cha Utafiti wa Elimu ya Dini ya Kiislamu mjini Cairo, Misri cha Al-Azhar, kuonya kuhusu toleo hilo lenye kikaragosi cha kejeli kwamba litazidisha chuki na hasira. Aidha, kituo hicho kimesema kitendo kama hicho hakitosaidia kuishi kwa amani miongoni mwa watu. Ama kwa upande mwingine, Waziri Mkuu wa Australia, Tony Abbott amesema amekipenda kikaragosi hicho, kwa kuwa kinaonyesha moyo wa kusamehe.
Valls asema Ufaransa inapambana na ugaidi
Akizungumza jana bungeni, Waziri Mkuu wa Ufaransa, Manuel Valls alisema kuwa nchi hiyo iko katika vita dhidi ya ugaidi, lakini amesisitiza kuwa jamii ya Waislamu siku zote itakuwa na mahala pa kuishi kama nyumbani nchini Ufaransa.
Wakati huo huo, mchekeshaji wa Ufaransa mwenye sifa mbaya, Diedonne, amekamatwa leo baada ya kuandika kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Facebook akisema anamwaonea huruma mmoja wa watu waliokuwa na silaha waliofanya mashambulizi mjini Paris.
Duru za kimahakama zimeeleza kuwa waendesha mashtaka walifungua kesi dhidi yake siku ya Jumatatu, baada ya kuchapisha kwenye ukurasa wake wa Facebook maneno yanayosema ''Usiku huu najisikia kama Charlie Coulibaly'', na hivyo kutofautiana na msemo wa ''Je Suis Charlie.'' Ahmed Coulibaly ni mmoja wa watu waliohusika na mashambulizi ya Paris.