Israel na Hamas zatakiwa kusitisha mapigano
https://samchardtz.blogspot.com/2014/07/israel-na-hamas-zatakiwa-kusitisha.html
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limetowa wito wa kusitishwa kwa
mapigano mara moja kwa misingi ya utu katika vita vya Gaza kati ya
Israel na Hamas.katika mkutano wake wa dharura usiku wa Jumapili
(27.07.2014).
Balozi wa Marekani kwa Umooa wa Mataifa Samantha Power (kulia)
akizungumza na balozi wa Uingereza katika baraza hilo Lyall Grant
(kushoto) kabla ya mkutanao wa baraza hilo New York.(27.07.2014).
Baraza hilo limekutana katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New
York wakati Waislamu wakianza kusheherekea siku kuu ya Eid al Fitr ya
kuadhimisha kumalizika kwa mwezi mtukufu wa mfungo wa Ramadhan.Shinikizo la kusitishwa kwa mapigano linakuja kufuatia mashambulizi mapya yaliofanywa na Israel na wapiganaji wa Hamas hapo jana licha ya mapendekezo kadhaa ya kusitisha kwa muda mapigano hayo ya takriban wiki tatu. Usitishaji wa mapigano wa saa 12 hapo Jumamosi uliokubaliwa na pande zote mbili kufuatia juhudi kubwa za usuluhishi za Marekani na Umoja wa Mataifa haukuweza kudumu.
Baraza la Usalama limeitaka Israel na Hamas kukubali na kutekeleza kikamilifu usitishaji wa mapigano chini ya misingi ya utu katika kipindi cha Eid na baada ya kipindi hicho.Limesema hatua hiyo itawezesha kufikishwa kwa misaada inayohitajika kwa dharura.Taarifa ya baraza hilo pia imezitaka kujihusisha na juhudi za kufanikisha usitishaji wa mapigano wa kudumu utakaoheshimiwa kikamilifu kwa kuzingatia juhudi za Misri.
Taarifa yakosolewa
Wapalestina na Waisrael wote wameikosoa taarifa hiyo iliyotolewa na Baraza la Usalama.
Balozi wa Wapalestina katika Umoja wa Mataifa Riyad Mansour amesema baraza hilo lilipaswa kupitisha azimio kali muda mrefu uliopita litakaloshurutisha kisheria kusitishwa mara moja kwa uvamizi wa Israel,kuwapatia ulinzi wananchi wa Kipalestina na kuachana na hatua za kuufungia Ukanda wa Gaza ili kwamba bidhaa na watu viweze kusafirishwa kwa uhuru.
Mansour amesema "Kwa hiyo tutaona iwapo Israel itaheshimu usitishaji huu wa mapigano kwa misingi ya utu au itaendelea na uvamizi wao dhidi ya wananchi wetu kwani wanaendelea kukalia kwa mabavu sehemu ya Ukanda wa Gaza na wanapaswa kuondoka kwa haraka."
Balozi wa Israel kwa Umoja wa Mataifa Ron Prosor amesema taarifa hiyo ya Baraza la Usalama haikuitaja Hamas, maroketi yanayovurumishwa na kundi hilo nchini Israel au haki ya Israel kujihami.
Usitishaji wa mapigano kuheshimiwa ?
Amekwepa masuala kadhaa juu ya iwapo Israel itaheshimu usitishaji mpya wa mapigano na badala yake amesisitiza kwamba ilikubali mara tano kusitisha mapigano tokea kuanza kwa mzozo huo.
Amesema "Tulifanya kila tuwezalo kuepusha kuendeleza mzozo huu lakini Hamas iligoma kukomesha mashambulizi.Israel ilikubali mapendekezo matano ya kusitisha mapigano Hamas iliyakataa au kuyavunja yote hata yale iliyoyaomba yenyewe."
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mara nyingi linagawika vibaya katika masuala ya Israel na Wapalestina ambapo Marekani mshirika muhimu kabisa wa Israel mara zote hukwamisha au hutumia kura yake ya turufu katika taarifa na maazimio yanayowasilishwa na Wapalestina na washirika wao.
Wakati juhudi za kimataifa zikipamba moto kutaka kuwepo kwa usitishaji wa mapigano utakodumu kwa muda mrefu ndege za kivita za Israel zimeshambulia vituo vitatu katika Ukanda wa Gaza leo hii baada ya kombora kuvurumishwa katika mji wa mwambao wa Ashkelon ulioko kusini mwa Israel.