HIVI NDIVYO ILIVYOKUWA AJALI YA BAHATI BUKUKU
https://samchardtz.blogspot.com/2014/07/hivi-ndivyo-ilivyokuwa-ajali-ya-bahati.html
NI kweli ajali haina kinga! Nyota
wa nyimbo za Injili Bongo, Bahati Lusako Bukuku ameumia mgongo na
maeneo kadhaa ya mwili (nusu kifo) kiasi cha kushindwa kukaa, kusimama
wala kutembea kufuatia ajali mbaya ya gari iliyotokea kwenye eneo la
Ranchi ya Narco wilayani Kongwa, Dodoma saa tisa usiku wa kuamkia
Jumamosi, Ijumaa Wikienda lina undani wa mkasa mzima.
Nyota wa nyimbo za Injili Bongo, Bahati Lusako Bukuku.
Kwa mujibu wa chanzo makini, katika
ajali hiyo ambayo Bahati alikuwa akienda Kahama, Shinyanga kwenye
mkutano wa Injili, dereva wa gari alilokuwa akisafiria aina ya Toyota
Nadia lenye namba za usajili IT 7945, Edison Mwakabungu ‘Eddy’ (31)
aliumia sana kwenye vidole vya miguu na hawezi kutembea.
Muonekano wa gari hilo kwa ubavuni kulia.
Wengine waliokuwemo kwenye ajali hiyo
ni wacheza shoo wa Bahati, Frank Muha (20) na mwenzake ambaye jina lake
halikupatikana mara moja.
ILIKUWAJE?
Habari zilidai kuwa gari hilo
halikuwa na matatizo hivyo kumfanya dereva wake kukanyaga mafuta kwa
wastani wa kilometa 120 kwa saa.“Sasa walipofika eneo la Kibaigwa,
walikutana na lori likitokea Dodoma kwenda Morogoro, wakavaana kwa
mbele. Nadia likatoka barabarani hadi porini likiwa limeharibika kuanzia
kwenye shoo ya mbele, injini na siti za mbele halafu lori hilo
likakimbia.
“Nadia ilipotulia, Bahati alijikuta
hawezi kufanya chochote, dereva wake naye ameumia kwenye vidole vya
miguu. Wale wawili waliokuwa siti ya nyuma, wote walijeruhiwa lakini
mmoja si sana. Ilibidi yeye abaki pale na gari ili majeruhi wengine
wakimbizwe Hospitali ya Wilaya ya Kongwa, Dodoma kwa matibabu,” kilisema
chanzo hicho.
Gari alilopata nalo ajali mwimbaji wa nyimbo za Injili Bongo, Bahati Bukuku aina ya Toyota Nadia lenye namba za usajili IT 7945.
HABARI NYINGINE
Habari ambazo hazijathibitishwa
na dereva wa Bahati zilisema kuwa, wakati gari hilo linakaribiana na
lori, dereva wa lori aliwasha taa ‘full’ (mwanga mkali) hivyo kumfanya
dereva huyo kushindwa kuona mbele vizuri, jambo ambalo ni kinyume na
sheria za usalama barabarani.
ROSE MUHANDO, JENNIFER MGENDI WAFUNGA SAFARI
Ilidaiwa kuwa usiku huohuo,
waimba Injili mahiri Tanzania, Rose Muhando na Jennifer Mgendi walipata
taarifa za ajali hiyo na kufunga safari ya kwenda Kongwa kuangalia namna
ya kuwahamishia majeruhi hao kwenye Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH)
jijini Dar.
ROSE MUHANDO
Rose Muhando alipotafutwa kwa
simu juzi mchana na kuulizwa kuhusu kusafiri kwenda Kongwa, alikiri na
kusema wameshafika na Jennifer Mgendi.
“Ndiyo tupo kwenye hekaheka
ndugu yangu. Tuna dhamira ya kuwachukua majeruhi kuwapeleka Muhimbili
kwa matibabu zaidi,” alisema Rose.
JENNIFER MGENDI
Yeye alipopatikana alisema
alishtushwa na simu asiyoijua usiku mnene na kuambiwa shoga yake huyo
amepata ajali mbaya ya gari.“Kitu cha kwanza niliuliza hali yake,
nikaambiwa ameumia mgongo, dereva wake mguu. Ndiyo nikaanza kuwataarifu
wadau wengine na mimi kujiandaa kwa safari kutoka Dar kuja Kongwa usiku
huohuo. Kwa kweli ameumia,” alisema Mgendi ambaye ni rafiki mkubwa wa
Bahati.
Naye Katibu wa Chama cha Waimba
Injili Tanzania, Stella Joel alipozungumza na gazeti hili juzi, alikiri
waimba injili hao kuondoka Dar es Salaam kuelekea Dodoma kumpa msaada
mwenzao.
BAHATI BUKUKU AZUNGUMZA KWA TABU
Alfajiri ya juzi, mwandishi wa
habari hizi alimpigia simu Bahati na kuongea naye kuhusu ajali hiyo
ambapo huku akisikika kama anayepata tabu kwa maumivu, alisema:
“Ni kweli tumepata ajali,
nimeumia mgongoni, dereva ameumia mguu. Namshukuru Mungu. Sijui nini
kilitokea, nilishtukia kuona gari kubwa mbele yetu likituvaa, mara
nikashtukia tuko porini. Lakini kabla ya safari Dar tulifanya maombi
makubwa, najua Mungu ametunusuru na kifo kibaya,” alisema Bahati.
Mwandishi: “Unadhani nani
alikuwa na kosa kati ya dereva wako na wa lori?”Bahati: “Sijui
chochote. Halafu najisikia vibaya sana, tuwasiliane baadaye kaka ‘angu.”
UZOEFU WA DEREVA
Habari zinasema kwamba, Eddy ni
dereva wa miaka mingi. Mbali na jijini Dar, pia amekuwa akiendesha
magari kwenda nje ya Tanzania kama Burundi na Rwanda na katika ajali
hiyo alikuwa akienda nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC),
hivyo ana uzoefu wa safari za usiku.
WATU WA INJILI NA AJALI ZA DODOMA
Kumbukumbu zinaonesha kuwa hii
si mara ya kwanza kuripotiwa kwa ajali za magari mkoani Dodoma
zikiwahusisha watu wa tasnia Injili Bongo.
Aprili, mwaka huu, Mkurugenzi
wa Kampuni ya Msama Promotion, Alex Msama alipata ajali mbaya ya gari
kwa kugongana na mwendesha bodaboda.Ajali hiyo ilitokea maeneo ya
Ipagala Mwisho, kilomita chache kabla ya kufika mjini Dodoma. Msama
alikuwa kwenye gari lake aina ya Toyota Mark II GX 100.
Katika ajali hiyo, Msama na
mwendesha bodaboda huyo waliumia sehemu mbalimbali za mwili na
kukimbizwa Hospitali ya Mkoa wa Dodoma kwa matibabu.
Kabla ajali ya Msama haijapoa, Mei,
mwaka huu, Edson Mwasabwite naye alipata ajali kwenye Barabara Kuu ya
Dodoma–Morogoro. Alikuwa akitoka Dodoma kurudi Dar. Alinusurika.