Coutinho, Jaja ndiyo hivyo
https://samchardtz.blogspot.com/2014/07/coutinho-jaja-ndiyo-hivyo.html
Tofauti na wenzake wengi, Coutinho ana mwili wa
wastani, lakini amekuwa ngangari muda wote wa mazoezi huku akigongana na
huyu mara yule ili mradi mambo hayaharibiki.
MBRAZILI wa Yanga, Andrey Coutinho anapambana na
wachezaji wenzake katika jua kali na kusisitiza yeye si mlaini kama
mashabiki wanavyomtafsiri kwa kuangalia umbo na rangi yake, huku benchi
la ufundi likibaini staili ambayo itampa Genilson Santos ‘Jaja’ unafuu
mikoani.
Tofauti na wenzake wengi, Coutinho ana mwili wa
wastani, lakini amekuwa ngangari muda wote wa mazoezi huku akigongana na
huyu mara yule ili mradi mambo hayaharibiki.
Coutinho ameliambia Mwanaspoti: “Unajua huu ni
mpira, sasa lazima upambane ili ufanikiwe. Mimi siyo laini kabisa ndiyo
maana unaniona napambana muda wote.”
Muda mwingi wa mazoezi hayo, Coutinho amekuwa
akionekana kuutamani mpira na hata anapopokonywa amekuwa akiutafuta kwa
nguvu akiwakaba wapinzani wake na kufanikiwa kuuchukua.
Anaonekana kutojali hali ya hewa ya joto na muda
wote amekuwa hashindwi zoezi lolote linalotolewa na Kocha Marcio Maximo
‘The Chosen One’.
Kuna wakati baadhi ya wachezaji huchemsha zoezi la kukimbia kasi au taratibu lakini Coutinho amekuwa akifanya vizuri.
Coutinho ni mmoja wa Wabrazili wawili waliosajiliwa na Yanga akiwemo Jaja na anaonekana ana nafasi kikosi cha kwanza.
Neiva ampa mbinu Jaja
Kocha Msaidizi wa Yanga, Leonardo Neiva amesema
kuwa watakuwa wanatumia staili ya kupiga mipira na pasi ndefu za juu kwa
ajili ya viwanja vibovu na vile vigumu kucheza vinavyoelezwa kuwa ni
taabu kwa wachezaji wa Yanga wanaposafiri mikoani.
“Ili kuepukana na tatizo hilo, tutacheza mifumo
yote ambayo tumekuwa tukiitumia, lakini huko hatutacheza mipira ya
chini, tutakuwa tunacheza mipira mingi ya juu na krosi kwa wingi na hiko
ndicho tunachowafundisha wachezaji kwa sasa,” alisema.
Naye Coutinho alisema: “kiukweli naogopa viwanja
vibovu, lakini kwa pamoja kama timu naamini tutaweza kupata mafanikio.
Mimi binafsi najua kuwa Jaja atafaidi kwa sababu anapiga mipira ya
vichwa na uwezo wake ni mkubwa kwenye kucheza mipira ya juu.
“Unajua ni ngumu kucheza mpira kwenye viwanja
vibovu haswa kucheza pasi za chini. Mara nyingi huweza kupoteza malengo
ya uchezaji hivyo ujanja ambao utaifaidisha timu ni kucheza mipira ya
juu kwa juu.”