Flatnews

SAMCHARDTZ.COM IKISHIRIKIANA NA MWANANCHI YAWATAKIA EID EL FITR-MUBARAKA NJEMA


http://awakeningart.files.wordpress.com/2009/11/eid_mubarak_13.jpg
Waislamu nchini na duniani kote, leo wanaungana kushelehekea sikukuu ya kuadhimisha ibada tukufu na kongwe ya mwezi baada ya kumalizika Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

Kila Mwislamu anapaswa kumshukuru mola wake kwa kusema “Alhamdulillah” kumwezesha kuifunga ramadhani kwani wapo wengi ambao wangependa kutekeleza ibada hii, lakini hawakuweza kwa matatizo mbalimbali, magonjwa, vita, vifo, ajali na majanga ya njaa na ukame.

Ni kweli kabisa kila aina ya sifa na shukrani zinastahili kwenda kwa Mwenyezi Mungu ambaye ni muumba kutokana na ukarimu na mapenzi yake kwa kuwawezesha watu wake kuukamilisha mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani na kufikia siku adhimu ya kufurahi, kupongezana, kusaidiana, kushirikiana na kuoneana huruma. Ni siku ya Idd El Fitri, Allah azikubali funga za wafungaji wote.

Huu ni wakati wa waumini wa dini ya Kiislamu nchini kuungana na wenzao duniani kote kusherehekea sikukuu hii ya Idd El Fitri baada ya kukamilisha ibada kongwe ambayo pia iliwajibishwa na kutekelezwa na watu (umma) waliowahi kuishi katika hii dunia kabla ya Muhammad (S.A.W). Hivyo ipo kila sababu na haja ya kumuomba Mwenyezi Mungu azipe nguvu na imani nafsi za wafungaji ili ziepukane na fitna, maovu, husda, ukatili na mabalaa mbalimbali ya nyuma na mbele yao, angani na ardhini, kulia na kushoto.

Aidha, siku hii ni ya kumwomba Mwenyezi Mungu awajalie mioyo ya huruma wafungaji wote waliojali ndugu, jamaa, marafiki, watu wenye mahitaji maalumu kama vile wenye ulemavu, mafukara na maskini kwa kuwapa misaada mbalimbali, zaka na hata sadaka ili wasijione madhalili, wanyonge, wapweke na wenye huzuni katika siku hii ya furaha.

Siku ya Idd ni siku ya kuwaangalia kwa jicho la huruma wagonjwa waliomo majumbani na hata hospitalini, wafungwa magerezani kwa kuwatembelea na kuwasaidia kwa kila hali sambamba na kuwaombea dua ya kuwatakia afya njema, nusura ili wamshukuru Mwenyezi Mungu na wajione ni sehemu muhimu katika sherehe hii.

Ni siku ya Waislamu kupongezana kwa kumaliza mfungo wa Ramadhani kwa kuwa ndio lengo la kuifuatishia kwa zaka ya chakula muhimu kinachopendwa katika mji au jamii husika ambacho kwa Tanzania chakula hicho ni mchele.

Ndani ya Ramadhani Waislamu walichukua ahadi kwa ajili kutekeleza ibada ya Funga kwa kujinyima mambo mbalimbali waliyohalalishiwa, ikiwa ni pamoja na kula, kunywa au makutano ya wanandoa mchana wa Ramadhani. Basi leo, Waislam wameruhusiwa kujinafasi kwa mambo hayo na ipo faida kubwa kwa aliyefunga.

Imezoeleka kuzungumzwa katika jamii kwamba, uhuru bila ya mipaka husababisha maafa. Hivyo ndio maana Mwenyezi Mungu ameweka mipaka katika kusherehekea Sikukuu ya Idd. Hivyo wale ambao watajipa mamlaka na uhuru kupita kiasi na kusahau mipaka ya Mwenyezi Mungu mwenyewe anawaona na anayajua yaliyomo ndani ya nyoyo zao.

Miongoni mwa matukio muhimu ya Sikuu hii ya Idd ni kwa Muislamu kushiriki katika swala maalumu ya Idd ambayo hufuatiwa na hotuba kama njia ya kufanya tathmini na kukumbushana, kuhamasishana, kuelekezana na kusisitizana katika kuendeleza utiifu, wema, ukarimu, upendo na heshima iliyojengwa ndani ya mwezi Mtukufu wa Ramadhani kama chuo.

Ama wale ambao watafanya fujo katika siku hii wakidhania kwamba ndio wamefika na wakaamua kuzikomoa swaumu zao kwa matendo maovu, hao watakuwa na tathmini mbovu na watakuwa wameshinda njaa tu lakini hawakufunga, kwani funga humwandaa mtu kuwa mcha Mungu.

Hivyo, wale wote ambao lengo hilo halikufikiwa wanapaswa kujuta, kulia na kumwomba msamaha Mwenyezi Mungu. Ewe Muislamu unayo kila sababu ya kujiepusha na kumuasi Mwenyezi Mungu baada ya mfungo kwani mwenye kufanya hivyo ni sawa na aliyemuasi Mwenyezi Mungu siku ya malipo.

Walioelewa maana ya swaumu na kulifikia lengo lake ndio wale wanaoendeleza mafunzo yake. Wapo wengi waliotumia fedha nyingi kwa kupamba na kukarabati misikiti, kufuturisha watu, kukirimu na kuwahurumia wenzao, kutoa zaka na sadaka kwa wahitaji wakatiu wa mwezi mtukufu.

Ni siku ya furaha, lakini ipo haja ya kuwakumbuka baadhi ya waumini ambao licha ya kula na kunywa, bado hawana furaha ndani ya nafsi zao kwa kuwa na dhiki mbalimbali za kilimwengu kama wafungwa magerezani, waliopata maafa ya ajali za ardhini na angani, wagonjwa hospitalini na walio katika vita kama walivyo Wapalestina hivi sasa.

Wote hawa wangetamani kuungana na wenzao katika siku hii ya furaha, lakini hawakuweza, Allah awape subra, nusura, msamaha na imani kubwa kwake ila wafanikiwe.

Ni siku ya kuiendeleza ahadi uliyoichukua ndani ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani. Kama uliipenda swala, kusoma Quran, kusimama usiku, kukaa itikafu, kukirimu watu, kusaidia wanyonge, kuhurumia wasiojiweza na ukachukia zinaa, dhuluma, rushwa, kusengenya, kusema uongo, kunywa pombe na kuiba.

Ewe Muislamu usijiweke katika kundi la waliofuata mkumbo na kujiingiza katika shiriki kwa kuacha maasi na kufanya mema kwa ajili ya Ramadhani na siyo kwa ajili ya Allah. Kumbuka kama ulikuwa unafanya Ibada kwa ajili ya Allah basi yeye yupo na ataendelea kuwapo daima. Lakini kama ulikuwa unafanya ibada kwa ajili ya mwezi wa Ramadhani basi tayari umeshaondoka na utajiingiza katika kundi la washirikina. Allah akulinde na sifa hiyo mbaya.

Miongoni mwa mambo ambayo ni muhimu kwa Muislamu kuyafanya siku ya Idd kama yalivyofanywa na kusisitizwa na Kiongozi wa Umma, Mtume Muhammad (S.A.W) ni kutoa zakatul fitri na kupata kifungua kinywa kabla ya kuswali swala maalumu ya Idd, kubadili njia wakati wa kwenda au kurudi kuswali Idd, kuswali Idd viwanjani na siyo msikitini.

Pia muhimu zaidi baada ya Idd ni kufunga siku sita katika mwezi huu wa mfunguo mosi kama tulivyozoea kuiita, aidha kwa kuzifuatisha au kuzitofautisha katika makumi ya mwezi huu.

Amesema Mtume rehema na amani ziwe juu yake. “Mwenye kufunga ramadhani na akafuatisha siku sita baada ya Ramadhani, thamani yake ni sawa na aliyefunga mwaka mzima”. Je wewe huzitaki kheri na faida hizo za kufunga siku sita za baada ya Ramadhani? Uzisikose basi.

Kila Muislamu anapaswa kuweka akilini kwamba Sikukuu ya Idd ni siku ya kutubia na siyo kutibua, ni siku kushukuru na siyo kukufuru, ni siku ya kuhurumiana na siyo ya kutesana kwa uadui, ni siku ya kupendana kwa ajili ya Allah na siyo ya kuchukiana, ni siku ya kutembeleana na siyo ya kukimbiana, ni siku kusalimiana na kujuliana hali na siyo ya kutukanana, ni siku ya kusuluhishana migogoro na siyo ya kufufua na kuanzisha migogoro mipya au kugombana, naam ni siku ya furaha na kuombeana kheri na siyo mabaya.

Neno zuri la kumwambia mwenzako siku ya Idd, ‘Takabbala Llahu Minny Waminkumu Sswiyaam ‘Allah azikubali swaumu zangu na zenu pia’.
MWANANCHI

Post a Comment

emo-but-icon

item