WAATHIRIKA WA MOTO SOKO LA MCHIKICHINI SASA KUSAIDIWA KUPITIA AKAUNTI MAALUM
http://samchardtz.blogspot.com/2014/06/waathirika-wa-moto-soko-la-mchikichini.html
Kaimu
Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam ambaye pia ni mkuu wa wilaya Ilala Bw.
Raymond Mushi akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es
salaam kuhusu kuanzishwa kwa mfuko wa kuwasaidia wafanyabiashara wa soko
la Mchikichini walioathiriwa na janga la moto kwa lengo la kurejesha
hali ya maisha waliyokuwa nayo hapo awali.
Mmoja wa waanzilishi wa mfuko wa kuwasaidia waathirika wa moto soko la Mchikichini ambaye pia ni Meneja wa Vituo vya mizigo vya nchi kavu wa Kampuni ya AZAM Bw. Raymond Adolph akieleza namna walivyoguswa na tukio la moto lililotokea katika soko hilo na kuwaomba watanzania kuunga mkono juhudi hizo.
Mwenyekiti wa wafanyabiashara wa soko la Mchikichini Bw. Jumanne Kongolo akiongea na waandishi wa habari kuishukuru serikali na wananchi waliojitokeza kufungua mfuko wa kuwasaidia waathirika wa moto katika soko hilo.
Baadhi ya wafanyabiashara wa soko la Mchikichini walioathiriwa na janga la moto wakifuatilia masuala mbalimbali ofisini kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam wakati wa uzinduzi wa mfuko wa kuwasaidia wafanyabiashara hao.
Picha na Aron Msigwa –MAELEZO.
MFUKO WA KUWASIDIA WAFANYABIASHARA WALIOATHIRIWA NA MOTO SOKO LA MCHIKICHINI WAANZISHWA.
Na Aron Msigwa – MAELEZO, Dar es salaam.
Baadhi
ya wakazi wa jiji la Dar es salaam wamejitokeza kuanzisha mfuko maaluum
wa kuwasaidia wafanyabiashara wapatao 5700 wa soko la Mchikichini
walioathiriwa na janga la moto lililotokea usiku wa kuamkia tarehe 12
mwezi huu eneo la Karume,jijini Dar es salaam.
Akaunti
hiyo maalum inayojulikana kwa jina la Mkono wa Pole Chinga 2014
imefunguliwa katika Benki ya CRDB Tawi la Lumumba ili kuwawezesha wadau
mbalimbali wanaoguswa na tukio hilo kutoa mkono wa pole kupitia akaunti
namba 0152270491300.
Kaimu
Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam ambaye pia ni mkuu wa wilaya Ilala Bw.
Raymond Mushi akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es
salaam amesema kuwa mfuko huo unalenga kurejesha hali ya maisha
waliyokuwa nayo wafanyabiashara hao hapo awali kabla ya kuungua kwa
vibanda na bidhaa zao.
Amesema
akaunti hiyo itasimamiwa kwa pamoja na wawakilishi kutoka ofisi ya Mkuu
wa Mkoa wa Dar es salaam, wadau waanzilishi na wafanyabishara
walioathirika.
“Tumeanzisha
akaunti hii kutokana na wananchi kuguswa na tukio hili kwa kuonesha nia
thabiti ya kutaka kutoa mkono wa pole kwa waathirika wa janga hili,
nachoweza kusema jambo hili tumeliwekea utaratibu na tutaliendesha kwa
uwazi mkubwa kwa kushirikiana na wahusika wa tukio” amesema Bw.
Raymond.
Aidha,
amefafanua kuwa serikali kupitia Manispaa ya Ilala ambayo soko hilo
liko chini yake itahakikisha inaboresha hali ya miundombinu katika soko
hilo zikiwemo barabara za kuwezesha magari na vifaa vya uokoaji kupita
wakati wa majanga ya moto huku akiwataka wafanyabiashara hao kutojenga
na kuzuia maeneo ya barabara katika soko hilo.
Mmoja
wa waanzilishi wa mfuko huo ambaye pia ni Meneja wa Vituo vya mizigo
vya nchi kavu vya vya Kampuni ya AZAM Raymond Adolph ameeleza kuwa yeye
kama mfanyakazi na wafanyakazi wengine wameguswa na tukio la moto
lililotokea katika soko hilo na kufafanua kuwa kiasi cha fedha
kitakachopatikana kitakabidhiwa kwa walengwa kwa uwazi huku akiwaomba
watanzania kuunga mkono juhudi hizo.
“Akaunti
hii tuliyoifungua itakuwa chini ya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na kiasi
tutakachopata tutakikabidhi kwa wahusika kwa uwazi na tunawaomba
watanzania wajitokeze ili kwa pamoja tuwasaidie ndugu zetu hawa
waliopata matatizo” amesisitiza.
Kwa
upande wake mwenyekiti wa wafanyabiashara hao ambaye pia aliathiriwa na
moto huo Bw. Jumanne Kongolo ameeleza ameishukuru serikali na wananchi
waliojitokeza kufungua mfuko huo kwa lengo la kuwasaidia wafanyabiashara
walioathirika na moto huo.