Utamaduni wa kujiweka makovu Afrika
http://samchardtz.blogspot.com/2014/06/utamaduni-wa-kujiweka-makovu-afrika.html
Kutia alama mwilini umekuwa utamaduni kwa miongo kadhaa katika maeneo tofauti barani Afrika ili kuashiria urithi wa kikabila.
Vitendo hivi hata hivyo vinapungua lakini bado kuna watu wanaotaka kuendeleza kilichofanya na mababu zao.Houeda ni mojawapo wa makabila nchini Benin inayoamini kuwa tendo la kuchanja watoto – hasa usoni- huwaunganisha na mababu zao.
Watoto hao hupewa majina mapya, wananyolewa vichwa vyao na kupelekwa katika makazi ya watawa ambapo kuna mizimu inayowasaidia kuzungumza na vizazi vya hapo awali.
'Utamaduni unaoenziwa'
“Hii ni sehemu ya tamaduni zetu na ni muhimu sana kwangu,” anasema Genevieve boko, ambaye mwanawe wa kike mwenye umri wa miezi 6, Marina, pamoja na wapwa zake Luc na Hospice wenye umri wa miaka 10 na miaka 12 wote wako tayari kuchanjwa.
“Rafiki zangu waliniuliza iwapo ni uchungu na iwapo nililia na nikasema ‘la!’,” alisema Luc baadae. “Kabla, nilipokuwa nikitembea mitaani pamoja na ndugu yangu mkubwa aliye na makovu, watu hawangeamini kuwa ni ndugu yangu. Sasa nina furaha kwa kuwa tunafanana.”
Tangu mume wake alipoaga dunia, Gamba Dahoui amekuwa akifanya chanjo zote za nyumbani-anasafisha vifaa vya kuchanjia kwa mimea yenye dawa pamoja na tembo. Makaa pia huwekwa kwenye majeraha ili kuyasaidia kupona.
Chanjo hizi hata hivyo zimeanza kupoteza umaarufu. Idadi kubwa ya familia inashiriki sehemu ya kwanza tu ya sherehe hizo, na kuacha kabla ya chanjo kufanywa.
Ni sawa sawa na sehemu mbalimbali ya taifa hilo ambapo kila kabila huwa na mfumo wake wa kuchanja.
'Ni aibu kukosa alama au makovu'
“Nikiwa na makovu yangu, ninatambulika kila mahali ninapokwenda,” anasema Fleury Yoro, anayeishi Atacora, kaskazini mwa taifa hilo. “Iwapo ningepata nafasi ya kufanya uamuzi, singependa kuwekewa makovu namna hii.”
Wengine wana maoni tofauti ya kufanya uamuzi wa kutochanja vizazi vichanga. Sinkeni Ntcha aliacha kitendo hicho baada ya watoto wake 3 wa kwanza ‘‘kwa sababu ya UKIMWI,” anasema. ‘‘Nyembe zinapaswa kubadilishwa kila wakati lakini wakuu walikataa.”
Kwake, kama mmoja kati ya watu wa kabila la Otomari, alama hizo “hazina maana”. Utamaduni unawezwa kuendelezwa kwa njia nyingine, anasema, kupitia kwa lugha, densi, unyago na usanifu.
Watu wengi wa kabila la Otomari bado wanakubali kutiwa alama, wakiwemo wanawake kadhaa wachanga ambao wakati mwingine huchanjwa kwenye migongo yao na tumboni wanapobalekhe ili ‘‘kuonyesha ujasiri wako,” anasema Edith (aliyeonyeshwa kwenye picha). Mifumo huwa sawa mara kwa mara na michoro inayochorwa kwenye mijengo ya mitaani.
Katika nchi jirani ya Nigeria, suala la haki za watu wachanga limesababisha baadhi ya majimbo kupiga marufuku zoezi hilo kwa watoto wote.
Hata hivyo, hii sio hatua inayowapendeza watu wote wa Benin. ‘Hatukiuki haki za watoto, tunawaonyesha watoto walikotoka na kile watakachopitia maishani,” anasema Telesphore Sekou Nassikou, mhariri mkuu wa kituo kimoja cha redio mjini Natitingou iliyoko kaskazini magharibi mwa taifa hilo.
Kwake, makovu hayo hupitisha ujumbe: ‘‘Tahadhari, kuna uchungu katika dunia hii, na utahisi uchungu katika maisha yako. Hata hivyo uchungu huo utaisha iwapo utavumilia.”