KAMERA ZA CCTV KUFUNGWA MITAANI Z'BAR
http://samchardtz.blogspot.com/2014/06/kamera-za-cctv-kufungwa-mitaani-zbar.html
MAENEO
mbalimbali visiwani Zanzibar, yamepangwa kuwekwa kamera za CCTV,
kukabili matukio ya uhalifu. Waziri wa Habari, Utangazaji, Utalii na
Michezo, Said Ali Mbarouk amesema mchakato wa utafiti wa kuweka kamera
hizo, umekamilika na kipaumbele ni eneo la Mji Mkongwe.
Mbarouk
alisema hayo wakati akijibu hoja mbalimbali za wajumbe wa Baraza la
Wawakilishi, waliochangia makadirio mapato na matumizi ya bajeti ya
Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2014/2015 katika Baraza Wawakilishi.(Martha Magessa)
Alisema
kampuni mbili, zilipewa kazi hiyo ya kuweka kamera za CCTV katika maeneo
mbalimbali , ambapo kipaumbele ni Mji Mkongwe wa Zanzibar.
“Mheshimiwa
Naibu Spika, kampuni hizo tayari zimewasilisha taarifa yake serikalini
kwa ajili ya uchambuzi wa kina na ripoti yake itatangazwa kwa wananchi,”
alisema.
Alisema
uwekaji wa kamera za CCTV ni muhimu kwa ajili ya kukabili matukio ya
uhalifu vitendo vya uhalifu ambavyo huathiri maisha ya watu na maendeleo
ya sekta ya utalii.
Mwakilishi
wa Mji Mkongwe, Ismail Jussa Ladhu alitaka kufahamu mikakati ya kuweka
kamera za CCTV za kurekodi matukio mbalimbali , ikiwemo ya uhalifu
katika eneo la Mji Mkongwe. Jussa alisema kama mradi huo wa kuweka
kamera ungekamilika na kufanya kazi, matukio mengi ikiwemo kumwagiwa
tindikali kwa raia wawili wanawake kutoka Uingereza, kungedhibitiwa na
wahusika wangekamatwa.
Awali,
Mbarouk alisisitiza suala la kuimarishwa kwa amani na utulivu nchini na
alitaka jamii kuachana na vitendo vya uhalifu ambavyo ni tishio kwa
maisha ya watu. Alisema matukio mbalimbali ikiwemo ya hivi karibuni la
kulipuliwa bomu eneo la Darajani, kunatishia amani ya nchi pamoja na
wageni kutembelea Zanzibar.
“Sekta ya
utalii inategemea sana amani na utulivu na ikivurugika tu, basi hakuna
mgeni atakayezuru Zanzibar katika mazingira ya vurugu na fujo,” alisema.
Uvaaji
baibui Wakati huo huo, Mwakilishi wa Viti Maalumu, Asha Bakari Makame,
alisema kutokana na kuwepo matukio ya ugaidi, suala la watu kupekuliwa
zaidi, hususani wanawake waliovaa baibui ni jambo la kawaida.
Alisema
yapo matukio ya wanawake, kutumia vibaya mavazi hayo, kutokana na
wengine kuficha sura zao kwa lengo la kufanya uhalifu huo. “Mimi sipingi
matumizi ya kivazi cha baibui...lakini kufuatia kuibuka kwa matukio ya
uhalifu na vitendo vya ugaidi, wanawake waliovaa mabaibui wanalazimika
kupekuliwa,” alisema.
Alisema
mbinu za uhalifu zimeongezeka siku hizi hali ambayo pia wanaume wanaweza
kutumia vazi hilo kwa ajili ya kutekeleza uhalifu. Vazi hilo ambalo ni
maarufu kwa wakazi wa mwambao wa pwani ya Afrika ya Afrika, hususani
Zanzibar, lilizua mjadala jana kwenye Baraza la Wawakilishi baada ya
baadhi ya wajumbe wanawake, kulalamika kwamba wanaofanya kazi kwenye
vyombo vya habari vya Serikali ya Zanzibar, wanalazimishwa kuvua mavazi
hayo wanapoingia kazini.
Hata
hivyo, Naibu Waziri wa Habari, Utangazaji, Utalii na Michezo, Bihindi
Khamis Hamadi alisema uvaaji baibui kwa wanawake, wanapokuwa kazini ni
upendeleo na si utaratibu wa kazi.
Alisema utaratibu wa kazi na masharti yake, upo wazi kwamba vazi hilo haliruhusiwi kuvaliwa sehemu ya kazi.
“Mheshimiwa
Naibu Spika yapo malalamiko mengi kutoka kwa wafanyakazi wa Serikali
kwamba wanazuiliwa kuvaa mabaibui katika sehemu ya kazi...ukweli
unabakia kuwa, vazi la baibui kazini haliruhusiwi na kinachofanyika ni
mazoea tu kwa wanawake hao,” alisema.
Alikiri
pamoja kwamba ni sehemu ya utamaduni wa wananchi wa Zanzibar, wanawake
wanapoingia kazini na mavazi hayo, hutakiwa kuyavua na kuyahifadhi
katika sehemu maalumu hadi wanapoondoka kazini.
Serikali
yazima ugaidi Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, jana aliliambia Bunge mjini
Dodoma kwamba matukio ya uhalifu yanayotokea Zanzibar, ikiwemo kumwagia
viongozi tindikali na utumiaji wa mabomu ya kurusha kwa mkono,
yalipangwa kuwa mengi zaidi, lakini Serikali imeyadhibiti. Alisema hayo
alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Betty Machangu (CCM).
Pinda
alisema baada ya matukio hayo Zanzibar, Serikali ilijipanga vizuri
ikiwemo kutumia vyombo vya kimataifa, kujua chanzo cha matukio hayo na
katika harakati hizo, walibaini kulikuwa kutokee matukio mengi zaidi,
Serikali ikayazuia.
Katika
swali lake kwenye kipindi cha Maswali ya Papo kwa Hapo kwa Waziri Mkuu,
Machangu alitaka kauli ya Serikali kuhusu kuibuka kwa vikundi vya
kihalifu vya vijana na vingine vyenye tabia ya kigaidi.
Alitaja
baadhi ya vikundi hivyo ni Panya Road, Kiboko Msheli, Komando Yosso na
Toto Tundu, na vingine vilivyotokea Mtwara ambavyo vilikuwa vikipewa
mafunzo vichakani na kwamba yako madai, baadhi walipelekwa Somalia.
Machangu
pia alitaka kufahamu kauli ya Serikali kuhusu matukio ya Zanzibar kuhusu
mauaji ya padre na kumwagiwa tindikali kwa mashekhe.
Katika
ufafanuzi wake, Pinda alisema Machangu amechanganya mambo mawili katika
swali lake, moja la ugaidi na lingine la uhalifu wa kawaida.
Katika
suala la uhalifu la vikundi hivyo kupora vitu na kukimbia, Polisi
imeshafanyia kazi. “Pale Dar es Salaam hali sasa ni shwari. Naomba
vijana wajiepushe na vitu vitakavyowakutanisha na mkono wa dola,”
alisema.
Pinda
ametoa kauli hiyo, wakati mwishoni mwa wiki iliyopita mtu mmoja
alifariki dunia na wengine saba kujeruhiwa baada ya kurushiwa bomu na
watu wasiojulikana katika eneo la Darajani, muda mfupi baada ya
kuhudhuria mawaidha yaliyokuwa yakitolewa na Shekhe Kassim Mafuta Kassim
(38) mkazi wa Pongwe mkoani Tanga.
Aliyefariki
dunia kwa bomu hilo ni Muhammed Khatib Mkombalaguha. Tukio hilo la
mlipuko ni la nne kutokea mwaka huu. Mengine ni yaliyotokea Kanisa la
Evangelist lililopo maeneo ya Fuoni Machi 2, Kanisa la Anglikana,
Mkunazini, Februari 24 na mlipuko mwingine ulitokea kwenye hoteli ya
kitalii ya Mercury ilioko Forodhani. Vilevile, Zanzibar imeandamwa na
matukio ya kumwagiwa watu tindikali pamoja na kushambuliwa kwa risasi.
Habari hii imeandikwa na Joseph Lugendo, Dodoma na Khatib Sulemain, Zanzibar.
CHANZO:HABARILEO