Flatnews

BARABARA UBUNGO KUFUNGWA


KAMPUNI ya ujenzi ya Strabag International GmbH inayojenga barabara ya Mradi wa Mabasi yaendayo Haraka (Dart) imetangaza kufungwa kwa baadhi ya njia katika eneo la taa za Ubungo, Dar es Salaam kuanzia leo usiku hadi keshokutwa kwa ajili ya kuruhusu ujenzi.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Ofisa Uhusiano wa Dart, Yahya Mkumba, alisema kazi hiyo itahusu ujenzi katika makutano ya barabara za Morogoro, Sam Nujoma na Nelson Mandela katika eneo hilo.(Martha Magessa)
Kutakuwa na awamu mbili za ufungaji wa njia kuanzia leo saa 4 usiku hadi keshokutwa saa 12 asubuhi; kwa ajili ya kutoa nafasi kwa ujenzi unaoendelea.
Akielezea zaidi, alisema katika awamu ya kwanza, ujenzi huo utahusisha eneo la upande wa kulia la makutano ya barabara ya Sam Nujoma na Morogoro ambalo litafungwa.
“Hali hii itasababisha magari yanayotoka maeneo ya Buguruni na Tabata kuelekea maeneo ya Mwenge kutoweza kutumia njia ya Sam Nujoma watakapofika taa za Ubungo,” alisema.
Alifafanua kuwa magari hayo yatalazimika kufuata alama zitakazowaelekeza kupita katika barabara za mradi zinazojengwa hadi barabara ya Shekilango ambapo wataweza kukutana tena na Sam Nujoma kwa kutumia barabara ya Igesa.
Pia magari yatakayokuwa yanatoka Sinza kupitia barabara ya Igesa hayataweza kwenda eneo la Ubungo yatakapofika katika makutano ya barabara za Igesa na Sam Nujoma.
Alifafanua kuwa magari yanayotumia Barabara ya Morogoro kutoka maeneo ya Mbezi na Kimara, yatalazimika kuchepuka kulia na kutumia barabara za mabasi ya mwendo wa haraka yatakapofika eneo la Kibo ambapo patakuwa na kizuizi.
Mkumba alisema katika awamu ya pili ya ujenzi huo, eneo la upande wa kushoto la makutano ya barabara za Morogoro na Nelson Mandela litafungwa kesho kuanzia saa nne usiku hadi keshokutwa saa 12 asubuhi.
Katika awamu hii, alisema, watumiaji wa magari yatakayokuwa yanatokea eneo la Mwenge kutumia barabara ya Sam Nujoma yatalazimika kuchepuka kushoto kukamata barabara ya Igesa kisha Shekilango.
Pia magari yatakayokuwa yanatoka Barabara ya Mandela na kutaka kwenda mjini kwa kutumia njia ya Morogoro yatalazimika kuchepuka kushoto na kwenda kugeukia eneo la Kibo ili kukamata barabara ya Morogoro.
“Tunaomba radhi kwa usumbufu wowote utakaotokea,” alisema Mkumba na kuongeza kwamba anaamini kutakuwa na usumbufu ambao hata hivyo utakuwa ni wa muda. Mradi wa Mabasi yaendayo Haraka unaoendelea, unatarajiwa baada ya kukamilika utaondoa adha ya foleni katika Jiji la Dar es Salaam na kuleta ufanisi wa usafiri.
CHANZO:HABARILEO

Post a Comment

emo-but-icon

item