kauli hii ya Ridhiwani si ya kuinyamazia.
http://samchardtz.blogspot.com/2014/06/kauli-hii-ya-ridhiwani-si-ya-kuinyamazia.html
Na Hudugu Ng'amilo
Katika
toleo la Gazeti la NIPASHE Juni 18, 2014, kulikuwa na habari
iliyoanzia ukurasa wa kwanza na kuendelea wa tano iliyobeba kichwa cha
habari: Ridhiwani kijana asiyekuwa na shukurani.
Habari
hiyo ilikuwa ikizungumzia matamshi ya Mbunge wa Chalinze (CCM),
Ridhiwani Kikwete, akiwaponda wanahabari nchini kuwa asilimia kubwa ni
makanjanja na kwamba wanapoandika habari wanasukumwa na weledi wa jinsi
wanavyofikiria vichwani na itikadi zao za kisiasa.
Ridhiwani
alitoa kauli hiyo Juni 8, mwaka huu wakati wa mahafali ya wanafunzi
ambao ni wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika vyuo vikuu vya
mjini Morogoro, yaliyofanyika katika ukumbi wa Bwalo la Umwema, mjini
humo.
Alisema
waandishi wengi hapa nchini wanasukumwa sana na utashi wa siasa zao,
jinsi wanavyofikiria vichwani mwao na itikadi ya siasa.Aliongeza kuwa
wakati mwingine hata jambo zuri likifanyika haliwezi kusifiwa badala
yake kazi yao kubwa ni kuandika mambo ya ovyo ovyo tu.
Mbunge
huyo alidai kuwa, asilimia kubwa ya waandishi nchini ni makanjanja na
wanapokaa kwenye meza zao wanaandika vitu tu, wanapikapika vitu,
akimaanisha wanaandika vitu vya kutunga.
Sisi
tumeshangazwa sana na kauli ya mbunge huyu kijana ambaye ni miezi
michache tu iliyopita amechaguliwa kushika nafasi hiyo kuwakilisha
wananchi wa Chalinze.
Tunasema
tumeshangazwa na kauli hiyo, kwa sababu Ridhiwani akiwa mwanasiasa
kijana, anapaswa kutambua umuhimu na mchango mkubwa wa waandishi wa
habari katika taifa hili ambalo linakabiliwa na changamaoto nyingi za
umasikini, badala ya kuwabeza.
Tunafahamu
kuwa ni ukweli usiopingika kuwa tasnia ya habari nchini inakabiliwa na
changamoto nyingi, lakini hiyo siyo sababu ya mtu kama Ridhiwani ambaye
ni mwanasiasa na tena Mbunge kutumia lugha ya kejeli na kudhalilisha
tasnia hiyo, badala ya kuwa sehemu ya kutafuta ufumbuzi wa changamoto
zilizopo.
Kama
amesahau, labda tumkumbushe Ridhiwani kwamba, ni vyombo vya habari na
waandishi wa habari ambao leo anawabeza, wametoa mchango mkubwa katika
kuchaguliwa kwake kuwa Mbunge wa Chalinze hivi karibuni tu.
Ridhiwani alikuwa akizunguka na waandishi wa habari huku na huko katika jimbo zima la Chalinze waweze kuandika habari zake.
Ni
waandishi wa habari hawahawa anaowabeza wamemsaidia kwa kiasi kikubwa
Mbunge huyu katika kampeni hizo, wakitangaza na kueneza sera za chama
chake na ahadi zake ili kuwashawishi wananchi wamchague, na kweli
alifanikiwa na sasa ni Mbunge.
Ni
Ridhiwani huyu huyu ambaye siku anaenda kuapishwa bungeni mjini Dodoma
baada ya kuchaguliwa, anadaiwa kubeba rundo la waandishi wa habari
kwenda kushuhudia kuapishwa kwake.
Leo
tunashangaa kuona akitoa lugha zinazotaka kuaminisha watu kuwa waandishi
wa habari ni watu wa ovyoovyo, wasiopaswa kuaminiwa katika jamii.
Ridhiwani
amebeba hulka ile ile ya baadhi ya wanasiasa ambao huwatumia waandishi
wa habari kufanikisha mambo yao, lakini wanapofanikiwa huanza kuonyesha
kiburi, dharau na kutoa kauli za kudhalilisha dhidi yao.
Kama
kweli Ridhiwani ana nia njema na waandishi wa habari, angekuwa mstari wa
mbele kutumia nafasi yake ya ubunge aliyoipata, kuibana na kuishinikiza
serikali kupeleka haraka bungeni muswada wa sheria ya vyombo vya habari
na sheria ya uhuru wa kupata habari viweze kusimamia sekta hii muhimu,
badala ya kutumia lugha za kejeli na kudhalilisha.
Tunamshauri
mwanasiasa huyu kinda atambue kwamba ndiyo kwanza ameanza kutembea
katika ulimwengu wa siasa, ajifunze kutafakari kabla ya kusema. Daima
kuweka akiba kwa kila jambo ni busara zaidi. Ridhiwani aache kuvimba
kichwa kwani kitapasuka mapema.
CHANZO: NIPASHE