Lipumba Amtahadharisha Rais Magufuli Kuhusu Dr. Shein Kuhudhiria Bungeni Leo
Wakati Rais John Magufuli akitarajiwa kuzindua na kulihutubia Bunge leo, ametahadharishwa kutoambatana na Rais wa Zanzibar, Dk Al...
https://samchardtz.blogspot.com/2015/11/lipumba-amtahadharisha-rais-magufuli.html
Wakati Rais John Magufuli akitarajiwa kuzindua na kulihutubia Bunge leo,
ametahadharishwa kutoambatana na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein
kwa maelezo kuwa si rais halali wa Zanzibar kikatiba.
Akizungumza na waandishi wa habari jana Dar es Salaam, Profesa Ibrahim
Lipumba alisema Zanzibar haina Rais, hivyo kiongozi huyo kushiriki Bunge
kwa nafasi hiyo ni kuvunja Katiba ya nchi.
Alishauri endapo kuna ulazima wa Rais wa Zanzibar kuhudhuria, Tume ya
Uchaguzi Zanzibar (ZEC) itangaze matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa urais wa
Zanzibar na rais aliyeshinda aapishwe.
Lipumba pia amemtaka Rais Magufuli kutumia nafasi yake ya Amiri Jeshi
Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama ya Tanzania kuishauri ZEC kurejea
matokeo ya uchaguzi uliofanyika Oktoba 25 na kumtangaza mshindi.
“Wazanzibari hawawezi kuruhusu uchaguzi kurudiwa, ” alisema Lipumba.
Alisema anashangazwa na hatua ya Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete
kuondoka madarakani na kumwachia Magufuli mgogoro wa Zanzibar. Alisema
Kikwete alipaswa kuhakikisha matokeo yanatangazwa na mshindi anaapishwa.
Alisema Kikwete alipoingia madarakani alionyesha kusononeshwa na mgogoro
wa Zanzibar na kuahidi kuupatia ufumbuzi wa kudumu lakini inashangaza
kuona akiondoka madarakani huku kukiwa na mgogoro mkubwa.
“Ninamuomba Rais Magufuli asilifumbie macho suala hili, awaeleze
wenzake wa CCM waache kumuwekea vikwazo katika kipindi chake hiki cha
kuliongoza Taifa,” alisema Profesa Lipumba.
Alisema kuiminya demokrasia Zanzibar ni kuwapa fursa watu wenye itikadi
kali kuwashawishi Wazanzibari hasa vijana kuamini kuwa hawawezi kupata
haki kwa kupitia sanduku la kura.
Alisema endapo kauli ya Wazanzibari kupitia kura zao haitaheshimiwa,
wananchi wake watapoteza imani kuwa hawawezi kupata mabadiliko kwa njia
ya kidemokrasia.
“Hili ni jambo la hatari sana, si kwa Wazanzibari pekee, bali kwa
Watanzania wote na ukanda mzima wa Afrika Mashariki…tusijenge mazingira
ya kuwapa fursa watu wanaotaka mabadiliko kwa njia haramu,” alisema Lipumba.
Alisema kitendo cha CCM kukataa matokeo ya uchaguzi wa Zanzibar kinaweza
kuliingiza Taifa kwenye mgogoro wa kisiasa na kiusalama, Magufuli
akatae kupelekwa huko,” alisema Profesa Lipumba.
Akizungumzia mtazamo wake juu ya Serikali ya Magufuli, Profesa Lipumba
alisema ameanza vizuri kwa kutamka nia yake ya kudhibiti matumizi mabaya
ya fedha za umma kwa kupiga marufuku safari za nje.
Alisema hatua hiyo ni ishara kuwa ataweza kuwatumikia Watanzania kwa moyo.
Alimtaka Rais Magufuli kutekeleza dhamiri yake ya kupambana na ufisadi
kwa kuwafungulia mashtaka na kuwafunga wote waliochota fedha katika
akaunti ya Tegeta Escrow.
“Ni vema pia akaunda baraza dogo la mawaziri na ajiwekee
vipaumbele vichache vyenye tija kwa Taifa na wananchi atakavyoweza
kuvisimamia kwa karibu,” alishauri Lipumba.