KAZI IMEANZA:. UCHAGUZI MKUU WASUSIWA HUKO KILOSA-MOROGORO ;WANANCHI WANADAI HAWATAPIGA KURA..HILI HAPA TUKIO ZIMA
Kaya 200 zenye watu zaidi ya 1,500 waliothirika na mafuriko mwaka jana na kuishi katika mahema katika kijiji cha mateteni, wilayani K...
https://samchardtz.blogspot.com/2015/10/kazi-imeanza-uchaguzi-mkuu-wasusiwa.html
Kaya 200 zenye watu zaidi ya 1,500 waliothirika na mafuriko mwaka jana
na kuishi katika mahema katika kijiji cha mateteni, wilayani Kilosa,
mkoa wa Morogoro wameazimia kutoshiriki kupiga kura katika uchaguzi
mkuu utakaofanyika Jumapili ijayo.
Kaya hizo zimefikia uamuzi huo kwa kile walichoeleza kuwa, serikali
imeshindwa kuwapa makazi ya kudumu hivyo kuendelea kuishi maisha magumu
kwenye mahema yaliyochakaa na wengine kulazimika kulala nje kwa kukosa
makazi.
Akizungumza kwa niaba ya wathirika wenzake, Saston Bwile, alisema baada
ya ya kukumbwa na mafuriko mwaka jana, serikali kupitia viongozi
mbalimbali akiwamo Waziri Mkuu Mizengo Pinda na Rais Jakaya Kikwete
walitoa ahadi mbalimbali za kuwasaidia lakini mpaka sasa hakuna
iliyotekelezwa.
Alisema Rais Kikwete alipowatembelea katika eneo hilo aliiagiza serikali
ya wilaya ya Kilosa kuwapa viwanja vya kujenga makazi mapya kutokana na
nyumba zao kubomoka na nyingine kusombwa na maji lakini ahadi hiyo
haijatekelezwa.
Naye Salma Rashidi ambaye pia ni muathirika wa mafuriko hayo anayeishi
katika mahema, alisema wameamua kutoshiriki uchaguzi huo kutokana na
kuendelea kuishi kwa mateso ikiwamo kuathiriwa na upepo mkali hasa
watoto wao.
Alisema upepo makali hasa majira ya usiku umewaathiri watoto wachanga
wanane ambao wameugua ugonjwa wa nimonia kutokana na kulala nje na mama
zao.
Naye kiongozi wa kijiji cha Mateteni, Iddi Ally, alisema wananchi hao
wameamua kugomea uchaguzi mkuu kutokana na serikali kushindwa kutimiza
ahadi zake hivyo wamekata tamaa kutokana na maisha magumu wanayoishi.
Alisema kutokana na hali hiyo, baadhi ya waathirika wamelazimika kurudi
katika makazi yao ya awali ingiwa si salama kutokana na kuchoshwa na
maisha magumu katika kambi hiyo, huku baadhi wakiishi kwa kulima vibarua
ili kupata fedha za kujikimu.
Alisema licha ya jitihada mbalimbali za wao kama viongozi kufuatilia
ahadi hizo ikiwamo Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, mpaka
sasa hakuna majibu ya kupata viwanja ingawa eneo hilo limezungukwa na
mashamba pori makubwa ambayo hayajawahi kuendelezwa.
CHANZO: NIPASHE
