Flatnews

Ufafanuzi kuhusu Itikadi ya Ujamaa wa Kidemokrasia kwa Mujibu wa ACT-Wazalendo

na Kitila Mkumbo Katika makala hii ninaendelea kutoa ufafanuzi kuhusu baadhi ya dhan a na misingi inayotumiwa na Chama cha...



na Kitila Mkumbo
Katika makala hii ninaendelea kutoa ufafanuzi kuhusu baadhi ya dhana na misingi inayotumiwa na Chama cha ACT-Wazalendo. Leo ninafafanua kuhusu dhana ya ujamaa wa kidemokrasia.

Kabla sijaendelea, nichukue nafasi hii kushukuru kwa mrejesho chanya nilioupata kutoka kwa wasomaji kwa jinsi walivyoielewa dhana ya kiongozi wa chama, ambao ni mfumo mpya katika mifumo ya uongozi wa vyama vya siasa hapa Tanzania. 
Nisingependa kujiingiza katika malumbano na baadhi ya ‘wachambuzi’ katika Gazeti la Mawio ambao wamejipa mradi wa kupotosha kila dhana na jambo linalofanywa na mwanasiasa Zitto Kabwe na Chama cha ACT-Wazalendo.
 Badala ya kueneza itikadi na sera za chama chao, kama zipo, hawa ndugu zetu wameamua kujipa ukatibu uenezi wa Chama cha ACT-Wazalendo.
 Inabidi uongozi wa ACT-Wazalendo wawashukuru ndugu zetu wa Mawio kwa jitihada zao za kuitangaza ACT-Wazalendo na kuisaidia kujulikana kwa watanzania.
 Ni imani yangu kuwa watanzania wana uelewa wa kutosha na wataweza kutofautisha pumba na mchele katika maandishi wanayoyasoma. 

 Neno itikadi lilitumiwa kwa mara ya kwanza wakati wa mapinduzi ya Ufaransa na Antonie Destutt de Tracy (1754-1836), moja ya wanafalsafa wa mwanzo wa Ufaransa, na lilitumiwa kwa mara ya kwanza katika umma mwaka 1796.
 
 Kama dhana ya kisiasa, neno itikadi lilitumiwa kwa mara ya kwanza na Karl Marx mwaka 1846 katika kitabu chake kilichoitwa “The German Ideology”. 

 Waandishi wengi wameandika maana mbalimbali kuhusu itikadi. Lakini kwa urahisi na ufupi neno itikadi linamaanisha mfumo wa fikra wa kisiasa unaotoa msingi wa mapambano ya kisasa unaotumika kutetea msimamo fulani katika jamii na kupinga misimamo mingine. 
 
Itikadi ya kisiasa ndiyo hutoa taswira ya chama cha siasa na aina ya serikali ambayo wataunda mara watakapochaguliwa kuingia madarakani.
 Chama cha siasa bila itikadi sio chama cha siasa bali ni sawa na taasisi isiyo ya kiserikali inayofanya miradi ya maendeleo. 
Kwa maneno mengine chama cha siasa kisicho na itikadi inayoeleweka kwa umma ni sawa na debe tupu au mwili bila kichwa!

 Itikadi hugawanya katika mirengo miwili mikubwa, yaani mrengo wa kulia na mrengo wa kushoto. 
 
 Kihistoria, kundi la mrengo wa kulia huwakilisha watu wasioamini katika usawa, wakiamini kwamba haiwezekani kuwa na usawa katika jamii.
 Kundi la mrengo wa kushoto huwakilisha watu wanaoamini katika mapinduzi ya fikra na usawa katika jamii. 

 Tofauti ya msingi katika mirengo hii miwili ni kuhusu kazi ya serikali katika uchumi na namna ya kuendesha serikali. 
 
Watu wanaoamini katika mrengo wa kushoto (kabisa) wanaamini katika serikali kumiliki uendeshaji wa uchumi kwa asilimia mia moja.
 
 Kundi hili pia hawaamini katika demokrasia shirikishi na kwamba kazi ya kupata viongozi ni kazi ngumu inayopaswa kufanywa na kundi dogo la wateule ambao ni wafia nchi. 
 
Kwa usahihi wake kundi hili huwakilisha wakomunisti kama ilivyokuwa Urusi ya zamani na ambayo kwa kiasi bado ipo katika China hasa katika namna ya kupata viongozi. 

 Kulia kabisa wapo mabwenyenye wanaoamini asilimia mia moja katika nguvu ya soko huria na umiliki binafsi wa mali.
 Kwa mujibu wa kundi hili kazi kubwa ya serikali ni kuhakikisha ulinzi na usalama wa raia na mali zake na kukusanya kodi, na kwamba kila mwananchi anapaswa kupambana kadri ya uwezo wake katika kujitafutia riziki. 

 Hata hivyo, kwa kutambua ugumu wa kutekekeza dhana hizi mbili katika uasili na uhalisia wake, mirengo hii miwili imefinyangwa na kutoa mirengo mingine mitano, ambayo ni mrengo wa kushoto, mrengo wa kati kushoto, mrengo wa kati, mrengo wa kati kulia na mrengo wa kulia. 
Kwa upande wa mrengo wa kushoto na mrengo wa kati kushoto ndiko waliko wajamaa, wakati mrengo wa kati kulia na mrengo wa kulia ndiko waliko mabwenyenye au mabepari.
 Mrengo wa kati hujumuisha kundi la watu wanaoamini katika uliberali. 
Naamini wataalamu wa sayansi ya siasa wataweza kuvichambua vyama vyetu vya siasa katika mirengo hii ili kuwasaidia wananchi kujua chama gani kinasimama katika mrengo gani. 

 Chama cha ACT-Wazalendo kinasimamia katika mrengo wa kati kushoto na kinaamini katika misingi ya Ujamaa wa kiDemokrasia (Democratic Socialism). Ujamaa wa kiDemokrasia kwa mujibu wa ACT-Wazalendo unajengwa katika ngao tano. 
Mosi, cha cha ACT-Wazalendo kinaamini kwamba undugu na udugu ni hifadhi ya jamii ya asili kwa Afrika, na hivyo kila mtanzania na kila mwafrika ana jukumu la kumsaidia mwenzake anayekabiliwa na tatizo au janga popote alipo bila kutarajia malipo ya aina yoyote.
 Kwa kuzingatia ukweli kwamba bara la Afrika bado li dhaifu katika kuwekeza katika mifumo rasmi ya kijamii (social security systems) na ambapo ni watu wachache mno wenye hifadhi ya jamii rasmi, kudumisha undugu na udugu ndiyo njia pekee na ya uhakika katika kuhakikisha kwamba kila raia anakuwa na msaada pale anapokabiliwa na janga. 
Kwa hiyo ACT-Wazalendo inasisitiza ujenzi wa moyo wa kusaidiana miongoni mwa wananchi kiAfrika, 
kidugu na kindugu. Kwa mfano, badala ya kuwapora abiria wanaopata ajali barabarani, tungependa kuona jamii ya watanzania inayowasaidia abiria hawa ili warudi katika hali zao za kawaida badala ya kuwaongezea maumivu. Huu ndiyo uAfrika na ndiyo maana ACT-Wazalendo inasisitiza kila mara kwamba turudi katika misingi utanzania na uAfrika wetu. 

 Ngao ya pili ni imani kwamba serikali ina haki na wajibu wa kutengeneza sheria na kanuni zenye kulenga kuleta usawa wa kibinadamu na fursa za maendeleo katika jamii. Aidha, Serikali ina haki na wajibu wa kusimamia moja kwa moja sekta nyeti katika jamii zenye maslahi mapana ya kiusalama na kiuchumi kwa nchi.
 Pamoja na kutambua na kuthamimini mchango wa sekta binafsi katika uchumi na maisha ya kijamii kwa ujumla, ACT-Wazalendo inaamini kwamba serikali inawajibika kupitia mfumo wa kisheria kuhakikisha kwamba kila mwananchi anakuwa na fursa sawa za kujiletea maendeleo na kupata huduma muhimu za kijamii, na kwamba serikali ina wajibu wa msingi wa kuwakinga wananchi kupitia mfumo wa sheria dhidi ya athari zitokanazo na soko huria.

  Ngao ya tatu ya ujamaa wa kidemokrasia kwa mujibu wa ACT-Wazalendo ni imani kwamba viongozi na watumishi wa umma wana wajibu wa kuhakikisha kwamba wanaishi na kuenenda katika misingi inayolinda heshima ya ofisi za umma na kwamba hawatumii nafasi zao kwa manufaa yao binafsi na jamaa zao.
 Ili kuwasaidia na kuwawezesha viongozi na watumishi wa umma kuenenda katika misingi ya uadilifu, kuna haja ya kuwekewa miiko na maadili maalum ya viongozi.
 Ni kwa sababu hii kila kiongozi wa ACT-wazalendo katika chama au serikali atawajibika kusaini na kutekeleza tamko rasmi la viongozi kuhusu maadili na miiko yao.
 Maadili na miiko ya uongozi imeelezwa katika kijitabu kitakachochapishwa siku za usoni na katika fomu maalumu ambayo viongozi watasaini. 

 Ngao ya nne ni kwamba ACT inatambua kuwa sisi wananchi wa Tanzania ndiyo raslimali kubwa ya nchi, na kwamba nchi yetu imejaliwa raslimali nyingi ambazo zikivunwa na kutumika vizuri zinaweza kuboresha maisha na kuchangia katika maendeleo ya jamii na Taifa kwa ujumla. 
Hivyo basi, shabaha kuu ya ACT ni kuhakikisha kuwa utajiri wa nchi unatumika kuboresha maisha ya watu na kuchochea uwezo wao katika kuchangia kujenga uchumi shirikishi ambapo kila mtu ana fursa sawa za maendeleo.

 Ngao ya tano ni imani kwamba demokrasia ndiyo msingi wa maendeleo, umoja na maelewano katika jamii ya watu waliostarabika. Demokrasia ni msingi wa tano katika misingi kumi inayoongoza Chama cha ACT-Wazalendo.
 Katika hili, ACT-Wazalendo inaamini kwamba msingi mama wa demokrasia ni kuhakikisha kuwa sauti za watu zinasikika na kuzingatiwa katika mipango ya maendeleo ya nchi. 
Tunaamini kwamba ni wananchi pekee wenye uhalali wa kuamua nani awaongoze na aina ya viongozi wanaowataka. 
Kama chama, dhana ya demokrasia inakwenda zaidi ya chaguzi za mara kwa mara. Dhana ya demokrasia kwa ACT ni sehemu ya mfumo wa uendeshaji wa chama ambapo kila mwanachama anayo nafasi na fursa ya kuchangia katika maamuzi ya chama na nchi, na anayo haki ya kuomba kuchaguliwa katika ngazi yoyote ya uchaguzi bila kikwazo. 

 ACT-Wazalendo kinaungana na vyama vingine zaidi ya 140 vinavyounda umoja wa vyama vya kijamaa duniani.

Related

NEWS 4519008822392348478

Post a Comment

emo-but-icon

item