WALE WATANI WA SOKA LA BONGO LEO NI LEO "YANGA Vs SIMBA"
Mahasimu wa kandanda nchini Simba SC na Yanga SC watapambana kesho Jumapili katika uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Ni mchezo wa mzungo w...
https://samchardtz.blogspot.com/2015/03/wale-watani-wa-soka-la-bongo-leo-ni-leo.html
Mahasimu wa kandanda nchini Simba SC na Yanga SC watapambana kesho Jumapili katika uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Ni mchezo wa mzungo wa pili wa ligi kuu Tanzania Bara,
Vodacom Premier League msimuhuu. Katika mchezo wa mzunguko wa kwanza, Oktoba, 2014 ‘ Watani hao wa Jadi’ walitoka suluhu-tasa. Yanga wanaingia uwanjani wakiwa vinara wa ligi kuu na alama nane mbele ya mahasimu wao walio nafasi ya nne.
NYOTA HAWA 11 NINGEWAPANGA KIKOSI CHA KWANZA SIMBA SC, Golikipa mzoefu, IVO Mapunda anastahili kuanza upande wa Simba kwa kuwa Yanga watashambulia sana mwanzoni mwa mchezo kutokana na hali waliyonayo ya kimchezo safu yao ya mashambulizi. Ivo ni kipa mjanja, wakati timu yake inapokuwa katika presha huweza kupoteza muda kijanja kwa kisingio cha kuumia.
Tangu ametua Simba akitokea Gor Mahia, Disemba, 2013, Ivo atakuwa anacheza mchezo wa pili wa ligi kuu dhidi ya timu yake ya zamani, huku akitaraji kupangwa kwa mara ya nne katika lango la Simba dhidi ya Yanga kesho Jumapili.
Kwa mara ya kwanza, Ivo aliidakia Simba wakati ‘ wekundu hao wa Msimbazi’ waliposhinda 3-1 dhidi ya Yanga katika mchezo wa Nani Mtani Jembe, 2013, alisimama tena langoni katika gemu ya marejeano ya mahasimu hao katika ligi kuu, April, 2014 katika gemu iliyomalizika kwa sare ya kufungana Simba 1-1 Yanga, na mara ya mwisho aliidakia Simba walipoishinda Yanga 2-0, Disemba, 2014 katika Nani Mtani Jembe. Kwa maana hiyo, IVO tayari yuko vizuri kisaikolojia huku Yanga wakiamini ‘ taulo lake lina uchawi’
Hassan Kessy katika ‘ beki 2′, Mohamed Hussein ‘ Tshabalala’ upande wb ‘ beki3′ watafaa zaidi ili kuweza kuwazuia washambuliaji wa pembeni wa Yanga, Mrisho Ngassa na Saimon Msuva. Sehemu ya ulinzi wa kati kamb ningekuwa katika nafasi ya kocha, Goran Kopunovic ningewapanga walinzi ‘ wawili Waganda’, Juuko Murishid na Joseph Owino ambao wanaweza kuwadhibiti washambuliaji wa Yanga ‘ wanaoifahamu’ Simba, Amis Tambwe na Danny Mrwanda. Hili Simba wapate matokeo watatakiwa kwanza kujipanga vizuri katika nafasi ya ulinzi kwa sababu Yanga wako vizuri katika mashambulizi na idara nyingine.
JONAS MKUDE, SAID NDEMLA, AWADH JUMA & SIMON SSERUNKUMA hii ndiyo safu ya kiungo iliyonza katika ushindi wa 2-0 ambao Simba waliupata mbele ya Yanga, Disemba, mwaka uliopita. Wachezaji hao watano wote wakiwa ‘ fit’ ningewapanga kwa mara nyingine ili kujaribu kuuvunja muhimili wa timu ya Yanga ambao ni sehemu ya kiungo. Salum Telela alicheza kwa dakika chache katika game ya mwisho ya mahasimu hao, kwa sasa ndiye ‘ injini ya kuzuia na kupanga mashambulizi’ katika timu ya Yanga.
TELELA , NIYONZIMA, MSUVA, NGASSA….
Telela ni kiungo namba-6 mwenye uwezo wa kumiliki mpira, kuanzisha pasi sahihi za mashambulizi, na inapotokea yuko katika eneo la mashambulizi anaweza kupiga pasi ya mwisho au ‘ kiki ya umbali mrefu’ Haruna Niyonzima ni mchezesha timu mwenye uwezo wakufanya hivyo akitokea upande wowote wa uwanja.
Katika michezo mitatu iliyopita ya mahasimu hao, NIYO ameshindwa kutawala. Uwepo wa Awadh na Mkude upande wa kiungo cha Simba umekuwa ukichangia kwa kiasi kikubwa kutong’ara kwa Haruna. Lakini haitakuwa mara zote hivyo, Haruna wa sasa yuko safi kiakili na kimwili.
YANGA NI HATARI KATIKA MASHAMBULIZI, IMARA KATIKA KIUNGO NA ULINZI…
Awadh na Mkude ni watibuaji wazuri wa mipira katikati ya uwanja upande wa Simba, Telela ni mtu wa aina hiyo kwa Yanga huku akisaidiwa kwa kiasi kikubwa na viungo washambuliaji watatu, Niyonzima, Ngassa na Msuva. Simba si timu ya kubeza katika mashambulizi. Ikiwa na washambuliaji watatu wa kati, Elius Maguli, Danny Sserunkuma na kijana, Ibrahimu Ajibu bila shaka safu ya ulinzi ya Yanga itakuwa katika presha kwa mara nyingine.
Kwa uchezaji wa Kelvin Yondan na nahodha wa timu, Nadir Haroub, ningekuwa katika nafasi ya Goran, ningemchagua, Ajibu kuanza na kiungo-namba 10, Emmanuel Okwi.
Simon na Ndemla ni wachezesha timu wazuri hivyo ili mipira iwe salama katika safu ya mashambulizi, Ajibu kutokana na uwezo wake wa kukontrol mpira, kumiliki na hata kusababisha penalti katika lango la wapinzani atafaa zaidi badala ya Maguli na Danny ambao licha ya kuwa na nguvu na uwezo wa kufunga si wazuri katika ‘kontroo’.
AJIBU & OKWI MACHAGUO SAHIHI KATIKA MASHAMBULIZI SIMBA
Kwa maana hiyo, Danny & Maguli gemu haiwafai, hata nahodha na mlinzi wa kati, Hassan Isihaka mechi ya kesho haimfai.Kutokana na mazingira ya mechi ni bora, Goran angewapanga, Juuko na Owino. Isihaka hufanya ‘mistake nyingi’ na uwepo wa Tambwe na Danny hauitaji mlinzi mwenye makosa mengi ambayo wakati wowote yanaweza kuigharimu timu yake.
Kila mshambulizi huwa na uwezo wa kufunga magoli, hivyo ndivyo ilivyo kwa Maguli na Danny lakini hawana kontroo nzuri na kutokana na uchezaji wa Kelvin na Nadir wa kutumia nguvu nyingi Simba itawahitaji washambuliaji ‘ wajanja wajanja’ waliokamilika kama Okwi na Ajibu. Mbuyu Twite ataanza upande wa kulia katika beki 2 ya Yanga, wakati mtu wa kushambulia kwa mipira mirefu, Oscar Joshua ataanza katika beki 3. Yanga ni imara katika ngome, kiungo na safu ya mashambulizi.
WALIO BENCHI WANAWEZA KUGEUZA MAMBO….
Timu zote bado zina vikosi vikubwa na bahati iliyoje pande zote hazina majeraha . Kiungo wa Simba, Abdi Banda anaweza kuwa mtu wa hatari akitokea benchi, sambamba na vijana kama Ramadhani Singano, Ibrahimu Twaha, Danny, Maguli wakati Yanga itakuwa na wakali kama Mliberia, Kpah Sherman, Hussen Javu, Jerry Tegete, Nizar Khalfani, Juma Abdul.
Mechi za Simba na Yanga hazitabiriki lakini kama ‘ Simba itapangwa vibaya itachapwa’. Si rahisi Yanga kupoteza mchezo na labda huu ni wakati wao pekee wa kuisambaratisha Simba inayosuasua. Matokeo ya mazuri ya Simba yataletwa na upangaji bora wa kikosi cha nyota 11 wa kwanza kutoka kwa Goran, Hans Van der Pluijm timu yake inajipanga yenyewe.