TANZANIA KUIKABILI KENYA BEACH SOCCER AFRIKA
Timu ya Taifa ya Tanzania ya mpira wa ufukweni (beach soccer) imepangiwa kucheza na Kenya katika raundi ya kwanza ya michuano ya ...
https://samchardtz.blogspot.com/2015/01/tanzania-kuikabili-kenya-beach-soccer.html
Timu
ya Taifa ya Tanzania ya mpira wa ufukweni (beach soccer) imepangiwa
kucheza na Kenya katika raundi ya kwanza ya michuano ya Afrika kwa ajili
ya fainali za Afrika za michuano hiyo zitakazofanyika Aprili mwaka huu
nchini Shelisheli.
Mwenyekiti
wa Kamati ya Beach Soccer, Ahmed Idd Mgoyi amesema jijini Dar es
Salaam, leo kuwa Tanzania itaanzia ugenini ambapo mechi ya kwanza
itachezwa kati ya Februari 13 na 15 mwaka huu nchini Kenya.
Mechi
ya marudiano itafanyikaa nchini kati ya Februari 20 na 22 mwaka huu.
Iwapo timu ya Tanzania itasonga mbele, katika raundi ya pili itacheza na
Misri ikianzia nyumbani kati ya Machi 13 na 15 mwaka huu.
Mgoyi
alisema maandalizi ya Tanzania kushiriki kwenye mashindano hayo
yameanza ambapo timu ya Tanzania Bara itacheza na Zanzibar ikiwa ni
sehemu ya mchakato wa kupata kikosi kimoja kitakachoingia kwenye
michuano hiyo ya Afrika.
Alisema
benchi za ufundi la timu ya Tanzania litaongozwa na John Mwansasu
wakati Msaidizi wake ni Ali Shariff 'Adolf' kutoka Zanzibar, na Meneja
wa timu hiyo ni George Lucas. Wote hao walishiriki kwenye kozi ya ukocha
wa beach soccer iliyoendeshwa mwaka jana nchini na Shirikisho la
Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA).
Kocha
Mwansasu atatangaza timu ya Tanzania Bara, Januari 19 mwaka huu, na
mazoezi ya pamoja na timu ya Zanzibar yatafanyika Januari 24 na 25 mwaka
huu.
Wachezaji
wa timu ya Tanzania Bara watatokana na michuano ya beach soccer
iliyofanyika mwaka jana ikishirikisha timu za vyuo vya elimu ya juu vya
Mkoa wa Dar es Salaam.