HAUSIGELI ASAKWA WIZI WA MTOTO
RPC Mara akiwa na mtoto aliyeibiwa(kushoto) ni mama wa mtoto huyo.
https://samchardtz.blogspot.com/2015/01/hausigeli-asakwa-wizi-wa-mtoto.html
MFANYAKAZI wa
ndani anayefahamika kwa jina la Paulina Sobe anatafutwa na Jeshi la
Polisi kwa tuhuma za kuhusika na wizi wa mtoto wa bosi wake, Diana
Meshack, mwenye umri wa miaka miwili, huko Musoma mkoani Mara, tukio
lililotokea Januari 3 mwaka huu.Kamanda wa Jeshi hilo mkoani Mara, ACP Philip Kalangi, aliliambia
gazeti hili kuwa kwa kushirikiana na askari wa Kanda Maalum ya Kipolisi
Tarime/Rorya,wamefanikiwa kuwakamata watu wawili walioshirikiana na
hausigeli huyo kumuiba mtoto.
ILIKUWAJE?
Chanzo kilicho karibu na familia hiyo
kinasema kuwa Januari 3 mwaka huu, msichana huyo wa kazi alionekana na
majirani akiondoka na mtoto huyo na kwenda naye kusikojulikana na tokea
wakati huo hakuonekana tena.
HALAFU?
Lakini mara tu baada ya kuondoka
nyumbani hapo, mama wa mtoto huyo, Gadioza Meshack alipokea simu kutoka
kwa watu wasiojulikana, waliomtaka kuwapa shilingi milioni 3 ili
wamrudishe binti yake, vinginevyo wangeenda kumuuza kwa watu wanaonunua
watoto.
Kamanda wa Jeshi mkoa wa Mara, ACP Philip Kalangi.
ASHINDWA, ALIFIKISHA POLISI
Kamanda Kalangi
alisema baada ya mama huyo kulifikisha suala hilo Polisi, wao kwa
kushirikiana na kampuni za mitandao ya simu, walianzisha msako wa
kuwasaka watu hao na kufanikiwa kuwanasa Januari 7 mwaka huu katika
kijiji cha Kitamwi, kilichopo mpakani mwa nchi jirani ya Kenya.
“Tulifanikiwa kuwakamata Vicent Magesa (19) na Erick Range, wote wakazi
wa Getabwaga nchini Kenya, wakiwa na mtoto huyo ambaye pia tulimkuta
akiwa salama,” alisema Kamanda Kalangi.
MAMA AELEZA ILIVYOKUWA
Akisimulia mkasa wa
kuibwa kwa mtoto wake, Gadioza Meshack alisema Januari 3 mwaka huu,
kabla ya kwenda kazini kwake,alimuacha mtoto akiwa na mfanyakazi huyo
aliyempa shilingi 15,000 ya kulipa bili ya maziwa na 10,000 ya
matumizi.
“Nalishukuru Jeshi la Polisi kwa kufanya jitihada za kupatikana kwa
mtoto wangu licha ya kwamba yule mfanyakazi aliyeondoka naye
hajapatikana, ila naamini kutokana na kazi kubwa iliyofanywa ya kumpata
mtoto hata yeye atapatikana,” alisema mama huyo.
Aliwataka wazazi
kuwa makini na watu wanao wachukua kwa lengo la kulea watoto kwani
wengine sio wazuri na baadhi hubadilika kwa kushawishiwa.