Obama awahimiza viongozi chipukizi wa Afrika kujenga misingi imara
https://samchardtz.blogspot.com/2014/07/obama-awahimiza-viongozi-chipukizi-wa.html
Rais wa Marekani Barack Obama amewahimiza viongozi chipukizi barani
Afrika kujenga mustakabali imara na wa kujitegemea wa siku za usoni kwa
ajili ya bara lao katika misingi ya haki za kijamii na inayozingatia
sheria
Rais huyo wa Marekani aliwaambia kiasi ya vijana 500 na wanaharakati kutoka Afrika wanaokutana mjini Washington kwa mkutano kuhusu viongozi bora wa baadaye kuwa amani,ufanisi na haki ambavyo ni masuala muhimu ambayo ulimwengu unataka kuyatimiza hayawezi kupatikana bila ya kuwepo bara Afrika imara, lenye ufanisi na linaloweza kujitegemea.
Viongozi wa nchi za Afrika kukutana na Obama
Wiki ijayo, Obama atakuwa mwenyeji wa viongozi hamsini wa nchi za Afrika katika mkutano mkubwa zaidi kuwahi kuandaliwa na rais yeyote wa Marekani mjini washington.Rais wa Zimbabwe Robert Mugabe,wa Sudan Omar al Bashir na wa Eriteria Issaias Afeworki hawatahudhuria.
Alipoulizwa na mwanachama wa taasisi ya Washington inayotoa mafunzo kwa viongozi chipukizi wa Afrika ni kipi Afrika inaweza kufanya,Obama ametilia msisitizo umuhimu wa kuheshimu sheria,haki za kijamii na haki za binadamu.
Kiongozi huyo wa Marekani amekiri kuwa nchi yake imelazimika mara kwa mara kushughulikia mizozo na changamoto katika sehemu nyingine duniani ambazo zinagonga vichwa vya habari lakini akasisitiza sharti kuwepo haja ya kutambua na kutumia fursa chungu nzima zilizopo hivi leo barani Afrika kuinuka na kukua.
Aidha Obama amewataka viongozi hao wa kesho kupambana na ufisadi,kuheshimu haki za wanawake kwa kupambana na mila za ukandamizaji kama vile ukeketaji na kuimarisha mfumo wa kuzingatia na kuheshimu sheria.
Kwa mara ya kwanza tangu kuingia madarakani,Obama ameshutumu vikali ukandamizaji wa wanawake kwa kuendeleza tamaduni zilizopitwa na wakati katika baadhi ya nchi barani Afrika na kuwataka viongozi kuwapa wanawake uwezo.
Wanawake wa Afrika wepewe uwezo
Obama amesema mwanamke wa kiafrika anao mchango mkubwa anaoweza kutoa katika jamii iwapo tu atapewa uwezo wa kutosha kumuwezesha kudhihirisha uwezo wake katika kujenga mustakabali wa siku za usoni barani Afrika.
Rais huyo wa Marekani amesema mojawapo ya ajenda katika mkutano wa kilele kati ya viongozi wa Marekani na wa Afrika kuanzia tarehe nne hadi sita wiki ijayo itakuwa suala hilo la kuwapa wanawake uwezo.
Alitangaza pia kuanzishwa kwa darasa la kutoa mafunzo kwa kundi la viongozi wanaoinukia kutoka Afrika watakaopewa mafunzo kuhusu uongozi kwa wiki sita nchini Marekani ili kuwa mifano bora ya viongozi wenye maadili barani Afrika na kuongeza kuwa mpango huo wa mafunzo utapanuliwa na kubadilishwa jina na kuitwa baada ya aliyekuwa rais wa Afrika Kusini Hayati Nelson Mandela.
Vituo vinne vya mafunzo kwa viongozi vijana vitaanzishwa nchini Ghana, Kenya,Senegal na Afrika Kusini ili kutoa mafunzo zaidi barani humo mbali na yale kuhusu uongozi pia yatatolewa pia mafunzo kuhusu ujasiriamali kwa vijana wanaotaka kuanzisha biashara.