KIFICHO: WARIOBA ALINILISHA MANENO
https://samchardtz.blogspot.com/2014/06/spika-wa-baraza-la-wawakilishi-pandu.html
Spika wa Baraza la Wawakilishi, Pandu Ameir Kificho
Wakati
bado msimamo wa Wajumbe wa Bunge la Katiba wa kundi la Ukawa ukiwa
haufahamiki kama watarejea bungeni kuendelea na vikao hivyo mwezi Agosti
au la, mjadala wa katiba mpya umechukua sura mpya, baada ya Spika wa
Baraza la Wawakilishi Pandu Ameir Kificho, kuungana na viongozi wa CCM
kukibeza kikundi hicho.
Kwa kauli
hiyo, Spika Kificho anaungana na Mawaziri wa SMZ katika kubeza uamuzi
huo wa Ukawa, ingawa yeye akaenda mbali zaidi na kumtupia lawama
Mwenyekiti wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph
Warioba akieleza kuwa alimlisha maneno.
Kificho
kwa mara ya kwanza amechomoza katika mkutano wa hadhara wa CCM
uliofanyika Uwanja wa Kwamabata eneo la Magogoni na kusema hakukuwa na
uamuzi wa pamoja wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, kupendekeza Serikali
tatu. Akasema dai hilo lilichomekwa na Tume ya Jaji Joseph Warioba
iliyokusanya maoni ya watu kuhusu katiba.
Kificho
amewaeleza wananchi kuwa yeye amezaliwa ndani ya Afro Shiraz (ASP),
akalelelewa na kukulia CCM, hivyo hathubutu, hatathubu na hakuthubutu
kusaini waraka wa kutaka mamlaka huru ya Dola ya Zanzibar ndani ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kwa mara
nyingine Kificho anaonekana kusafisha upepo mchafu uliokuwa ukivuma na
kutaka kumpeperusha ndani ya chama chake huku baadhi ya wanachama na
viongozi wenzake, wakimtaja kama mtu aliyeshiriki kutaka kuwasaliti na
kuwazunguuka mbuyu.
Madai ya
awali ya viongozi wenzake akiwemo Mnadhimu wa Baraza la Wawakilishi
Zanzibar upande wa CCM Salmin Awadh Salmin, yanamtupia lawama Kificho na
kumpasha hakukuwa na kikao chochote kilichoketi na kupitisha azimio la
BLW kutaka Serikali tatu au mamlaka kamili ya Zanzibar nje Muungano
uliopo.
Mvutano
huo ulioibuka nje ya Bunge la Katiba, huenda ndiyo ulioambukiza mipasho,
piga nikupige ya maneno na kutupiana vijembe vikali kati ya wabunge wa
Bunge la Katiba wa CCM na CUF kabla ya kundi la Ukawa halijaamua
kuliacha bunge na kusema wamechoshwa na matusi, kejeli na ubaguzi.
Kificho
akihutubia mkutano wa hadhara, akasema amekuwa Mwakilishi wa CCM Jimbo
la Makunduchi kwa miaka saba, akawa spika miaka 19, akijinasibu kuwa ni
spika mzoefu baada ya Chifu Adam Sapi Mkwawa, kufika kwake alipo sasa
kumetokana na nguvu za CCM, hivyo hana jeuri ya kusaliti sera za chama
chake.
Akizungumza
kwa kujiamni na kujiosha, akamtupia shutuma Mwenyekiti wa Tume ya
Mabadiliko ya Katiba ya Jaji Warioba akisema kuwa ndiye aliyemwandalia
fitina hiyo.
Hata
hivyo, waraka ulioandikwa na kusainiwa na Spika Kificho umeandikwa na
kutaja bayana kuwa Azimio la BLW Zanzibar ni kuhitaji mamlaka huru ya
Dola, jambo ambalo limechukuliwa na wengi kama linalohitaji serikali
yenye mamlaka kamili Zanzibar.
Kificho
anasema kilichomo kwenye waraka huo ni hitaji la kufanyika marekebisho
na mageuzi makubwa ya msingi ili kuipa Zanzibar nyenzo za kujijenga
kiuchumi na kujitegemea ijiendeshe kwa kusimamia mambo yasiokuwa ya
Muuungano kwa uwazi na si kupigania mamlaka huru ya Dola .
Pia
ameeleza kuwa katika moja ya waraka huo kulikuwa na kosa la kitaalamu
katika uandikaji na tafsri ya kila anayeusoma kutoa fasiri aitakayo,
lakini si kusudio la BLW au lake kutaka mamlaka huru ya Dola.
Imeelezwa
kuwa wawakilishi watano ndiyo waliojadili na kutia saini zao kwenye
waraka huo na Kamati ya Kudumu ya Uongozi ya BLW ikakwepwa.
Wajumbe
hao ni pamoja na Waziri wa Katiba na Sheria Abuboubakary Khamis
(Mgogoni) ,Spika Kificho, Hamza Hassan Juma (Kwamtipura), Katibu wa BLW
Zanzibar Yahya Khamis Hamad na Mgeni Hassan Juma (Viti Maalum).
Hata
hivyo Mwakilishi Hamza Hassan Juma (Kwamtipura) Makame Mshimba Mbarouk
(Kitope )Asha Bakari Makame( Viti maalum), Mwakilishi Mohamed Raza
(Uzini), aliyekuwa Mwakilishi wa Kiembesamaki (amefukuzwa CCM) Mansour Yussuf
Himid, Waziri wa Fedha Omar Yussuf Mzee ni kati ya vigogo wa CCM
waliosimama kidete kukosoa masuala kadhaa ndani ya Muungano kabla ya
Bunge la Katiba kuanza na Ukawa kuzaliwa.
Katika
semina iliyoitishwa na Baraza la Wawakilishi, wajumbe hao kwa kiasi
kikubwa walisimama na kueleza kuwa kimsingi hawakuridhika na waraka huo.
Hayo na mengine wakati yakijiri na kupita katika siasa za
Zanzibar, Msemaji wa CUF Salum Abdallah Bimani, ameeleza kuwa haikuwa
mwafaka kwa Spika Kificho kupanda kwenye majukwaa ya kisiasa na
kuzungumzia msimamo wa BLW na kumtupia lawama Jaji Warioba.
Bimana
anasema kama ataendelea kupanda majukwani na kukanusha msimamo wa BLW,
hawatasita kumrushia paka wa kisasa na kuweka kila kitu hadharani ikiwa
ni pamoja na kuanika waraka wake aliousaini kwa niaba ya taasisi
anayoiongoza.
Analitaja
Baraza ni moja kati ya mihimili mitatu inayounda Serikali hivyo
hakupaswa kiongozi wa mhimili kusimama na kutoa msimamo wa kitaasisi na
kusema hatua hiyo inaweza kutafsiariwa ni ukiukaji wa taratibu za
kidsemokrasia na uvunjaji wa mipaka yake.
Hata
hivyo wakati tuhuma hiyo wa Bimani ikoinekana kumponda na kumbeza Spika
Kificho kwa madai hayo ya taasisi anayoiongoza ni kinyume na miiko ya
demokrasia na mgawanyo wa madaraka, Naibnu Katibu Mkuu wa UVCCM Zanzibar
Shaka Hamdu Shaka, amemtaka Bimani kwaanza aondoe boriti kwenye jicho lake ndipo atoa kibanzi kwenye jicho la mwenzake.
Shaka
anasema ingefaa sana kama Bimani angekuwa jasiri wa kumnyamazisha Makamu
wa Kwanza wa Rais Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad ambaye pia ana
dhamana ya taasisi ya serikali lakini akituimia kofia ya kisiasa kama
Katibu Mkuu akizungumzia masuala ya kisiasa na kuafiki msimamo wa Ukawa.
Vyovyote
itakavyokuwa, kimsingi na kiuhalisia kuna umuhimu pande mbili za kisiasa
kati ya wabunge wa bunge la katiba chama tawala na kundi la Ukawa kukaa
kitako , kutafakari, kuafikiana na kuridhiana ili Taifa lipate katiba
mpya mwakani.