MKOSAMALI ATIBUA BUNGE
https://samchardtz.blogspot.com/2014/06/mkosamali-atibua-bunge.html
MBUNGE wa
Mhambwe, Felix Mkosamali (NCCR-Mageuzi), amezua mjadala mkali bungeni
kwa kuishambulia Serikali ya CCM akidai kuwa mawaziri wake wamekuwa
wakitoa majibu mepesi yasiyo na mashiko.
Mkosamali
alitoa kauli hiyo jana wakati akiuliza swali la kuitaka serikali ieleze
ni lini itapeleka muswada bungeni kwa ajili ya kutunga sheria ambayo
itatoa nafasi ya kila mbunge kulindwa kisheria kama ilivyo kwa viongozi
wengine.
Katika
swali hilo, Mkosamali alisema kuwa kutokana na wabunge kufanya kazi
ngumu ya kuwafichua mafisadi, wanafanya kazi katika mazingira magumu,
hivyo wanatakiwa kupatiwa ulinzi kisheria.
Hata
hivyo, Mkosamali alicharuka zaidi pale Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri
Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, alipojibu swali lake,
lakini akadai majibu hayo hayana mashiko.
“Wakuu wa
wilaya na mikoa si watu wadogo wadogo kama Mkosamali anavyosema, ni
viongozi wanaosimamia na kutekekeza shughuli za jamhuri kwa mujibu wa
sheria na yale wanayoyafuata wakuu wa wilaya na mikoa yapo katika
masharti yao ya kazi.
“Hawa
wanaopata ulinzi, yako kwenye masharti yao ya kazi, Bunge ni mhimili
unaojitegemea, hata mara moja serikali hatuwezi kuamua mambo yanayowafaa
wabunge, kwahiyo hili jambo mimi kama kamishna na makamishina tuliopo
hapa tumelisikia kwa sababu ni jukumu la mhimili kushauriana na serikali
juu ya masharti ya kazi na mambo mbalimbali,” alisema.
Kutokana na majibu hayo, Mkosamali aliendelea kuwashambulia viongozi hao akidai wanafanya kazi zao kwa kujipendelea wenyewe.
“Inashangaza
kuona mawaziri wa Serikali ya CCM wanavyojibu majibu mepesi mepesi
ambayo hayana mashiko, ikumbukwe kuwa wabunge wanafanya kazi kubwa ya
kufichua uhalifu ikiwa ni pamoja na kuwasema mafisadi.
“Hapa
mimi nimetaka kuelezwa ni lini serikali italeta muswada wa kurekebisha
sheria kwa ajili ya kumpatia mbunge ulinzi, lakini cha kushangaza
mawaziri wanasema kuwa watakaa ili wazungumze waone kama hali hiyo
inawezekana,” alisema.
Awali
katika swali la msingi, Mbunge wa Kasulu Mjini, Moses Machali
(NCCR-Mageuzi), alitaka kujua kutokana na kuwepo kwa vitendo vya
kuvamiwa viongozi mbalimbali, wakiwemo wabunge wakiwa mitaani na hata
majumbani mwao na watu wasiojulikana, serikali kwa sasa haioni umuhimu
wa kuwapatia wabunge na viongozi wengine askari wa kuwalinda dhidi ya
watu wabaya.
Akijibu
swali hilo, Naibu Waziri wa Maji, Amos Makala, kwa niaba ya Waziri wa
Mambo ya Nadani ya Nchi, alisema katika kutoa ulinzi wa viongozi, Jeshi
la Polisi linazingatia sheria ya Jeshi la Polisi sura Na. 322 ya mwaka
2002 pamoja na PGO Na. 291 na 316.
Alisema
kuwa viongozi wanaostahili ulinzi wa jeshi hilo ni Rais wa Jamhuri,
Makamu wake, Rais wa Zanzibar, Waziri Mkuu, Makamu wa Kwanza na wa Pili
wa Rais wa Zanzibar, mawaziri wakuu wastaafu pamoja na viongozi
mbalimbali kulingana na umuhimu wao.