BENKI YA EXIM KUPIGA JEKI HUDUMA ZA AFYA YA UZAZI NA MTOTO
https://samchardtz.blogspot.com/2014/06/benki-ya-exim-kupiga-jeki-huduma-za.html
Baadhi
ya kina mama nje ya hospitali ya Bombo mkoani Tanga wakiwa na miamvuli
waliyosaidiwa na Benki ya Exim Tanzania ikiwa ni sehemu ya mpango wa
Benki hiyo wa kugawa miamvuli bure kwa kina mama wazazi katika kuunga
mkono jitihada za serikali kuboresha afya nchini. Benki ya Exim
imejikita katika mpango huo ili kuwasaidia kina mama kujikinga na adha
ya jua kali na mvua pale wanapohudhuria kliniki na watoto wao.
Afisa
Masoko wa Benki ya Exim Fatma Kilinda (mwenye fulana nyeupe) akigawa
miamvuli kwa kina mama nje ya hospitali ya Bombo mkoani Tanga
iliyotolewa na Benki hiyo ikiwa ni sehemu ya mpango wa Benki hiyo wa
kugawa miamvuli bure kwa kina mama wazazi katika kuunga mkono jitihada
za serikali kuboresha afya nchini. Benki ya Exim imejikita katika mpango
huo ili kuwasaidia kina mama kujikinga na adha ya jua kali na mvua pale
wanapohudhuria kliniki na watoto wao.
============ ======= ==========
Benki ya Exim kupiga jeki huduma za afya ya uzazi na mtoto
Na Mwandishi Wetu, Tanga
KATIKA jitihada za kusaidia mpango wa serikali wa kuboresha afya ya
uzazi na mtoto nchini Tanzania, Benki ya Exim Tanzania imebainisha
kuendelea kutoa misaada katika sekta hiyo kwenye maeneo ambayo
yanaonekana kutoingia kwenye mpango wa uboreshaji wa sekta hiyo ya afya
ya uzazi na mtoto.
Benki hiyo ikiwa inaamini katika kauli mbiu yake kuwa "Ugunduzi ni
maisha", imejikita katika mpango wa kusambaza miavuli bure kwa akina
mama wanaohudhuria kliniki katika hospitali mbalimbali ya nchini.
Akizungumza
muda mfupi baada ya kutoa miavuli kadhaa kwa kina mama mbali mbali nje
ya hospitali ya Bombo katika mkoani Tanga, Meneja wa Benki ya Exim Tawi
la Tanga, Bw. Deogratius Makwaia alisema kuwa benki ya Exim imeamua
kuelekeza sehemu ya fedha zake zilizotengwa kwa ajili ya shughuli za
kijamii kununua miavuli kwa kina mama na watoto wao ambao baadhi yao
hawana uwezo wa kununua miamvuli hiyo.
"Ni kweli kwamba Serikali, mashirika ya maendeleo na wadau wengine
wanapiga jeki sekta ya afya ya uzazi na mtoto ikiwa ni eneo lenye
kipaumbele katika sekta ya afya. Hata hivyo, wakati wa kupanga,
tuligundua kwamba fedha nyingi uelekezwa kwenye ujenzi wa vituo vya
afya, kununua vifaa na dawa, lakini kusahau kusaidia vitu vingine
muhimu ambavyo mama na mtoto uvihitaji baada ya kuondoka katika kituo
cha afya.
"Baada ya utafiti wetu katika hospitali kadhaa nchini kote,
tuligundua kwamba akina mama wengi wanaohudhuria kliniki za wajawazito
ukumbana na wakati mgumu pindi mvua zinaponyesha au wakikumbana na jua
kali wakitokea sehemu mbali kuhudhuria kiliniki na watoto wao.
"Ukosefu
wa makazi kwa akina mama hawa na watoto wao, inaweza kuwa ndiyo sababu
inayochangia kwa baadhi yao hasa katika maeneo ya vijijini –
kutohudhuria huduma za kiafya mara kwa mara ambayo utolewa bure.
"Mpango
wa Benki ya Exim wa kutoa miamvuli kwa kina mama na watoto, umeanzishwa
ili kusaidia wale kina mama ambao hawana uwezo wa kumudu gharama za
miamvuli kujikinga dhidi ya mvua na jua kali ambalo linaweza kuwa na
madhara kwa afya zao," alisema Makwaia.
Aidha, alisema kuwa Benki ya Exim itaendelea kuiunga mkono serikali katika utekelezaji wa miradi mingine ya maendeleo nchini.
"Utamaduni
wa kurejesha sehemu ya pato letu kwa jamii umekuwa ni kipaumbele chetu
kikubwa. Hilo linatokana na Benki ya Exim kuendelea kukua na kwa mwaka
jana ilipata faida ya shilingi bilioni 20. Nina hakika kwamba uongozi
wetu umekuwa ukifanya bidii za kutosha kurejesha pato hili kwa jamii
kama njia ya kuboresha hali ya maisha ya wananchi pale ambapo Benki
inafanya shughuli zake, kama vile kusaidia ukuaji wa kiuchumi,"
aliongeza Makwaia.