BAJETI KUU YA SERIKALI ITASOMWA LEO BUNGENI DODOMA....WATANZANIA WASUBIRIA BIDHAA ZITAKAZOPANDA NA KUSHUKA, WAFANYAKAZI NAO WASUBIRIA MISHAHARA MIPYA
https://samchardtz.blogspot.com/2014/06/bajeti-kuu-ya-serikali-itasomwa-leo.html
Watanzania
leo wanaelekeza macho na masikio yao mjini Dodoma, kusikiliza Hotuba ya
Bajeti ya Serikali, inayotarajiwa kusomwa saa 10 kamili bungeni na
Waziri wa Fedha, Saada Mkuya Salum.
Tayari
Waziri Saada alishaeleza kuwa makadirio ya Bajeti ya Serikali kwa mwaka
wa fedha wa 2014/15, unaoanza Julai mwaka huu, yatakuwa Sh trilioni
19.6 kutoka makadirio ya Sh trilioni 18.2 ya Bajeti inayoisha muda wake.
Vipaumbele
vya Bajeti hiyo, kwa maana ya miradi itakayozingatiwa zaidi, ni iliyo
katika Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) unaohusisha sekta sita za
Kilimo, Elimu, Maji, Utafutaji rasilimali fedha, Nishati, Uchukuzi na
Uboreshaji wa Mazingira ya kufanyia biashara na Mpango wa Maendeleo ya
Miaka Mitano.
Akisoma
mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo kwa mwaka 2014/2015, Waziri wa Nchi
Ofisi ya Rais, Mahusiano na Uratibu, Stephen Wassira, alisema
mapendekezo ya mpango huo, yana vipaumbele vitano.
Cha kwanza
ni miundombinu, kikifuatiwa na kilimo, viwanda vinavyotumia malighafi za
ndani na kuongeza thamani, maendeleo ya rasilimali watu na ujuzi na
uendelezaji wa shughuli za utalii, biashara na fedha.
Katika
hotuba hiyo, Watanzania wengi watakuwa makini kusikiliza bidhaa na
huduma zitakazoongezwa kodi, jambo linalotarajiwa kuongeza bei ya bidhaa
za huduma husika katika soko.
Katika
bajeti inayoishia, Serikali iliongeza kodi kwenye magari makuukuu, bia,
vinywaji vikali na baridi ambavyo kodi imekuwa ikiongezwa kila mwaka na
kuwaathiri watumiaji.
Kutokana na
hali hiyo wanywaji pombe na sigara baada ya bajeti ya mwaka juzi ya
2012/2013, walilazimika kutumia fedha nyingi ili kupata huduma hizo kwa
kiwango kile kile katika mwaka huu wa bajeti unaoisha.
Bidhaa zisizokuwa za mafuta ambazo zilifanyiwa marekebisho na kuongezwa kodi ni mvinyo, pombe, vinywaji vikali, na sigara.
Ushuru pia uliongezwa kwenye magari yasiyokuwa ya uzalishaji na yenye umri wa miaka 10 kutoka asilimia 20 mpaka asilimia 25.
Lengo la
Serikali katika hilo, lilikuwa kupunguza uagizaji wa magari chakavu ili
kulinda mazingira na kupunguza ajali za mara kwa mara.
Katika bajeti hiyo, vijana wa bodaboda walicheka baada ya Serikali kusamehe ushuru wa barabara kwa pikipiki hizo za biashara.
Moja ya
kivutio kikubwa cha Bajeti inayowasilishwa leo, ni matarajio ya
wafanyakazi kuhusu utekelezaji wa ahadi ya Rais Jakaya Kikwete,
aliyoitoa katika sherehe za Mei Mosi mwaka huu, ya kuongeza mshahara wa
kima cha chini na kupunguza kodi ya mshahara (PAYE).
Rais Kikwete
alisema Serikali itaendelea kuongeza mshahara wa kima cha chini na
kubainisha kuwa mwaka 2005 alipoingia madarakani, alikuta mshahara wa
kima cha chini ni Sh 65,000 na kukipandisha taratibu hadi kufikia Sh
240,000 cha sasa.
Kuhusu
kupunguza PAYE, Rais Kikwete alisema kusudi la Serikali ni kupunguza
kodi hiyo ya mshahara kutoka asilimia 13 inayotozwa sasa, ifikie katika
kiwango cha tarakimu moja.
Kuhusu
misamaha ya kodi ambayo mwaka huu imekuwa gumzo bungeni, huku wabunge
wengi wakitaka ipunguzwe, Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba,
alinukuliwa akisema wafanyabiashara na vigogo wanaokwepa kodi kwa
kujificha kwenye mwavuli wa misahama, hawako salama.
“Tutafuatilia
kikamilifu kwa kuwa wapo watu wanaingiza bidhaa wanapewa msamaha,
lakini ukija kwenye huduma za jamii unakuta bidhaa hizo zinauzwa
kibiashara,” alisema.
Mwigulu pia alizungumzia ukwepaji kodi na matumizi mabaya ya fedha za Serikali na kufafanua kuwa, yatadhibitiwa.
“Bahati
nzuri niliyonayo, sikuzaliwa na chembe ya woga, kwa hiyo kwenye hili
hakuna mkubwa wala mdogo, hakuna mtu atagusa fedha ya umma kwa kukwepa
au kwa kutumia vibaya kodi ambayo ilishakusanywa halafu akapona
asiguswe,” alisema.
Mwigulu
alisema katika Bajeti ya Serikali ya 2014/2015, yapo mambo ya msingi
matano, ambayo yatasimamiwa kikamilifu ili kuhakikisha utekelezaji wake
unakuwa tofauti na zilizopita.
Mbali na
kuondoa misamaha ya kodi, pia makusanyo ya ndani yatatiliwa mkazo zaidi
ili kujenga uwezo wa kujitegemea wenyewe badala ya kutegemea wahisani.
Jambo la
tatu alisema ni kuhakikisha Serikali inapeleka fedha kwenye mahitaji
muhimu na kwa wakati, ili fedha za maendeleo zitumike kama
ilivyokusudiwa.
Jambo la nne
litakalozingatiwa kwa mujibu wa Mwigulu, ni usimamizi wa fedha
zinazopatikana kwani pamoja na makusanyo kidogo, lakini pia kuna
uvujaji.
“Tunataka
fedha inayopatikana na kupangiwa kazi fulani itumike kwa shughuli
iliyokusudiwa. Tutahakikisha tunasimamia na kudhibiti matumizi yake,” alisema.
Naibu Waziri
huyo wa Fedha alisema eneo la tano ambalo litaangaliwa ni fedha ambazo
hazitokani na kodi, bali zinachangwa na wananchi na wadau wengine katika
utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Alisema eneo
hilo ni muhimu mbalo Serikali inaona kuna haja ya kulisimamia vizuri,
ili kuhakikisha fedha za wananchi zinatumika vizuri.