WANAFUNZI WA CHUO KIKUU IRINGA WAsaidia watoto yatima tosamaganga
https://samchardtz.blogspot.com/2014/05/wanafunzi-wa-chuo-kikuu-iringa-wasaidia.html
WANAFUNZI wa Chuo Kikuu cha Iringa (IUCO) wamechangishana kiasi cha Sh Milioni moja na kukitumia kununua vitu mbalimbali walivyotoa kwa watoto yatima na wenye shida wa kituo cha Teresia Sister cha Tosamaganga, nje kidogo ya mji wa Iringa.
Akikabidhi misaada hiyo mkufunzi wa sheria wa chuo hicho Penina Manyanki amesema: "kutoa ni moyo, na unapotoa kwa makundi ya watu waliosahaulika unayapa faraja na kuyaondoa katika dhana ya kujiona wao ni tofauti na binadamu wengine.
Alisema watoto wanaolelewa kituoni hapo na vingine vyenye sifa kama hiyo ni taifa la kesho linalohitaji kupata haki zake zote kama ilivyo kwa watoto wengine na akayaomba mashirika na watu binafsi kujitokeza kutoa misaada kama hiyo.
Akizungumza kwa niaba ya mkuu wa kituo, Sister Mlezi wa Kituo hicho, Hellen Kihwele aliwashukuru wanafunzi hao akisema inawapa faraja na kuwapunguzia gharama kubwa za uendeshaji wa kituo hicho.
Sister Hellen alisema watoto wanaolelewa katika kituo hicho ni wale wenye miezi miwili hadi miaka sita.
Alitaja changamoto za mara kwa mara zinazowakabili kuwa ni pamoja na ukosefu wa chakula, madawa na mavazi na akasema jukumu la kuwasaidia sio la kituo au wafadhili kutoka nje pekee, bali ni la watanzania wote.