ANSGAR CUP-PERAMIHO: BAADA YA KUTIMUA BENCHI LA UFUNDI, AFYA FC YAICHABANGA KILAGANO’A’ GOLI 1-0
https://samchardtz.blogspot.com/2014/05/ansgar-cup-peramiho-baada-ya-kutimua.html
Kindumbwe
ndumbwe cha ANSGAR CUP-PERAMIHO, kimeendelea tena jana jioni ambapo
timu kutoka katika Kata za Kilagano na Peramiho zilikuwa zikioneshana
kazi kwa lengo la kupata pointi tatu muhimu.
Katika
mchezo wa kwanza uliopigwa mishale ya saa nane za mchana, timu ya AFYA
FC imepata ushindi wa kwanza tangu kuanza kwa mashindano hayo baada ya
kuifunga timu ya KILAGANO ‘A’ goli 1-0 goli lililofungwa na mshambuliaji
Moses Mgomela kunako kipindi cha kwanza kufuatia mpira wa pigo huru
(free kick).
Ushindi
huo wa AFYA FC umekuja mara baada ya Uongozi wa juu wa timu hiyo
kuwafukuza Makocha wa timu hiyo baada ya mwenendo mbovu wa mechi za
awali huku wachezaji wa timu hiyo wakijiongoza wenyewe kwa sasa.
Katika
dakika za awali za kipindi cha pili mchezo huo uliingiwa na sintofahamu
baada ya mwamuzi wa mchezo huo kuruhusu kipindi cha pili kuanza pasipo
golikipa wa AFYA FC Bwana John Mtuli kuingia uwanjani na hivyo kuibua
zogo miongoni mwa mashabiki wengi waliokuwepo uwanjani hapo.
Kwa
ushindi huo, timu ya AFYA imefikisha pointi nne baada ya kucheza mechi
tatu huku ikiwa imebakiza mechi mbili dhidi ya LIKUYU ‘B’ na
MPANDANGINDO, ambapo ili kujiweka katika mazingira ya kucheza nusu
fainali, inatakiwa ishinde mechi zote zilizobaki.
Ama
katika mchezo wa pili uliopigwa majira ya saa kumi za jioni, matumaini
ya wakazi wa PERAMIHO’A’ kwa timu yao ya RED STARS yamezidi kuingiwa na
shubiri baada ya timu yao hiyo kufungwa goli 1-0 na ZOMBA FC goli
lililofungwa kunako dakika ya 75 ya kipindi cha pili kwa mkwaju wa
penati baada ya mlinda mlango wa timu hiyo Daud Nyoni kumfanyia madhambi
mchezaji wa ZOMBA FC.
Kwa
matokeo hayo timu ya ZOMBA FC imefikisha pointi tisa baada ya kucheza
michezo minne, huku RED STARS ikibaki na pointi mbili baada ya kucheza
michezo mitatu na hivyo kutakiwa kufanya kazi ya ziada ili kuweza
kucheza hatua ya nusu fainali.
Wakati
huo huo Mashindano ya Njunde Cup yanataraji kuanza kutimua vumbi
Jumatano ya wiki hii katika Uwanja wa Tamasha huku timu kumi tayari
zimekwisha thibitisha kushiriki katika kindumbwendumbwe hicho.
Akizungumzia
na Peramiho Publications, Katibu wa Ligi hiyo Bwana SIXBERT KOMBA
ameweka bayana kuwa kila kitu kuhusu Ligi hiyo kipo katika utayari wake
huku akiwataka wakazi wa Peramiho kujitokeza kwa wingi uwanjani hapo kwa
lengo la kuwapa morali wachezaji wao.