SERIKALI KUENDELEA KUTHAMINI NA KUSIMAMIA MAENDELEO YA WAZEE NCHINI
Na Eleuteri Mangi
https://samchardtz.blogspot.com/2014/05/serikali-kuendelea-kuthamini-na.html
Uzee na
kuzeeka ni dhana inayoelezea hatua ya mwisho ya makuzi ya binadamu
kuanzia utoto, ujana hadi kufika hatua ya mwisho ya makuzi ambayo ni
uzee.
Binadamu
ni miongoni mwa viumbe hai ambao hupitia hatua hizo katika makuzi yake,
mwanasikolojia Erick Erickson aliyeishi kati ya miaka ya 1902-1994
amebaisha kuwa binadamu hupita hatua nane za makuzi hayo ikiwemo hatua
ya uzee.(FS)
Kulingana
na Erickson, Uzee ni hatua ya nane na ya mwisho katika maisha ya
mwanadamu, hatua ambayo umri wake unaanzia na miaka 65 na kuendelea
amabapo hutawaliwa kwa hekima, busara na kupungukiwa na nguvu za kufanya
kazi ngumu kupita uwezo wao.
Katika nchi zilizoendelea kama Uingereza na Marekani, suala la uzee linahusishwa na umri wa kustaafu ambao ni miaka 65.
Katika
nchi nyingine umri wa kustaafu unatofautiana kijinsi, kwa mfano, nchini
Latvia wanaume wanastaafu wakiwa na miaka 55 wakati wanawake wanastaafu
wakiwa na umri wa miaka 60.
Hapa
Tanzania mtu anaitwa mzee kutokana na ama umri mkubwa, majukumu
aliyonayo na pia hadhi yake, kwa mfano mkuu mahali pa kazi au katika
ukoo.
Mwandishi
wa makala haya anatumia dhana ya wazee tulionao katika nchi yetu kuwa
aidha walikuwa wanafanya kazi za kuajiriwa au kujiajiri au ni wale
walioko vijijini ambao kuzeeka kwao ni matokeo ya kupungukiwa nguvu za
kufanya kazi.
Tanzania
pamoja na ukweli kwamba watumishi walio katika Serikali na Taasisi zake
wanastaafu wanapofikia miaka 60 na kwamba wazee wa vijijini na wale
waliojiajiri wanakoma kufanya kazi kutokana na kuishiwa nguvu, ukweli
unabaki kwamba binadamu mwenye umri wa miaka 60 anaonyesha dalili za
hatua hiyo.
Kama
mataifa ya dunia hii, Tanzania inajali na kutambua umuhimu wa wazee
ikiamini kuwa wao ni kisima cha hekima na busara katika Maisha ya
kijamii na taifa.
Ni ukweli
usiopingika kuwa "wazee ni hazina", jambo ambalo linatuaminisha palipo
na wazee haliharibiki jambo kwani wao ni rasilimali na ni hazina kubwa
ya maendeleo.
Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kwa kutambua
umuhimu wa wazee amekuwa na desturi ya kuwatumia mara kwa mara katika
kutekeleza majukumu yake kitaifa na kimataifa.
Rais Kikwete anamini juu ya usemi wa "wazee ni hazina" na amekuwa akiongea nao kila anapoona ni muda muafaka kufanya hivyo.
Ipo
mifano hai ya Rais Kikwete alipozungumza na wazee hao ikiwemo Mei 03,
2010 aliongea na wazee wa mkoa wa Dar es salaam juu ya mkutano wa
kimataifa kuhusu masuala ya uchumi uliofanyika nchini Mei 05 hadi 07,
2010.
Mwaka huo
huo aliongea na wazee wa Dar es salaam mnamo Julai 30, 2010 ambapo mara
hii Rais Kikwete alikutana Ikulu na wazee wakongwe wa kivita nchini na
wanachama wa Tanzania Legion and Club kuhusu masuala yao ikikumbukwa
kuwa wazee hawa walilitumikia taifa lao kwa umahiri mkubwa.
Wazee
hawa vili vile ni washauri wakuu na walinda amani. Hali hii inadhihirika
kunapotokea migogoro mabilimbali katika jamii nyingi ambapo wazee
hutumika kama hatua za awaali katika kusuluhisha na hatimaye kupata
ufumbuzi wa migogoro hiyo.
Kwa
kuwajali, kuwalinda na kuwathamini, Umoja wa Mataifa umetenga siku ya
tarehe Oktoba Mosi ya kila mwaka kuwa ni Siku ya Wazee Duniani.
Siku hii imetengwa kufuatia uamuzi wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu Wazee katika azimio Na.46 la mwaka 1991.
Nafasi
hii imetengwa ili kuyawezesha mataifa kutafakari nafasi ya wazee katika
jamii kwa kuzingatia mahitaji, matatizo na ushiriki wao katika maisha ya
kila siku.
Tanzania
ambayo ni nchi mwanachama wa Umoja wa Mataifa, imekuwa ikiadhimisha siku
hii kitaifa kila mwaka ambapo mwaka huu ilifanyikia wilaya ya Korogwe
mkoani Tanga.
Kwa
kawaida siku ya Wazee Duniani huadhimishwa kwa kuzingatia ujumbe maalumu
wa mwaka ambao ni dira na kichicheo chenye dhana ya uhamasishaji kwa
wananchi.
Lengo
kubwa ni kuwawezesha kupata ufahamu na hatimaye kuweka mikakati ya
utekelezaji wa masuala muhimu yaliyoamuliwa Kitaifa na Kimataifa.
Maadhimisho
ya mwaka jana yaliongozwa na kauli mbiu iliyotafsiriwa na wazee wenyewe
iliyosema "Matarajio ya Wazee ni Heshima, Usalama na Maisha Bora"
tafsiri waliyoitoa kutoka kauli mbiu iliyotolewa na Umoja wa Mataifa
"The future we want: what elder persons are saying".
Kama
taifa hatunabudi kujikumbusha na kutafakari maneno ya busara
yaliyotamkwa na aliyekuwa Kaibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Koffi Anan,
"Huwezi kufurahia usalama bila maendeleo, hatuwezi kufurahia maendeleo
bila usalama na hatuwezi kufurahia hivyo vyote bila kuheshimu haki za
binadamu"
Katika
kuadhimisha siku ya Wazee Duniani, kuna mambo ambayo Tanzania kama taifa
imefanya juhudi na itaendelea kufanyia kazi kama kauli mbiu ya mwaka
huu inavyojieleza.
Nchi yetu imekuwa ikizingatia misingi ya sheria na utawala bora na hivyo kudumisha amani, heshima na kujali maisha ya watu wake.
Katika
kuadhimisha siku ya Wazee Duniani mwaka huu, Makamu wa Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mohamed Gharib Bilal, alisema kuwa nia ya
Serikali ya kupambana na vitendo vya uvunjifu wa amani katika nchi yetu
bado ipo palepale.
Dkt.
Bilal alisisitiza, "Nawasihi Watanzania wote tushirikiane bega kwa bega
na Serikali katika kujenga, kulinda na kudumisha amani kwa wazee".
Katika kuadhimisha Mwaka wa Kimataifa wa Wazee (1999) Serikali ilifanya maamuzi ya kuwa na Sera ya Taifa ya Wazee.
Maamuzi
ya kuwa na Sera hii ni kielelezo cha dhamira hai na dhati ya Serikali ya
kuweka masuala ya wazee katika agenda ya maendeleo ya nchi yetu.
Serikali
inatambua kwamba wazee wetu wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwa
ni pamoja na umaskini, kutotosheleza kwa huduma za afya, pensheni na
kutoshirikishwa katika maamuzi muhimu yanayohusu maendeleo ya nchi yao.
Pamoja na
hali hii, Serikali inatambua kwamba wazee ni raslimali na nguvu mpya
katika maendeleo ya nchi. Jitihada zitaendelea kuwekwa kuhakikisha
kwamba wazee wanatambuliwa na wanapata fursa ya kushiriki katika
shughuli za maendeleo ya nchi yao sanjari na wananchi wengine.
Kuwapo kwa Sera ya Taifa ya Wazee ni hatua ngeni kwa nchi nyingi, Tanzania ikiwa moja wapo.
Katika
bara la Afrika, Tanzania imekuwa nchi ya pili kuwa na Sera ya aina hii
baada ya Mauritius. Endapo kutatokea upungufu katika matamko na
utekelezaji wa Sera yenyewe Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii itakuwa
tayari kufanya marekebisho pale yanapohitajika.
Kwa
Serikali, watumishi wa umma na jamii nzima, Sera ya wazee kwa taifa letu
ni mwongozo katika kuandaa mipango, utekelezaji na tathmini utoaji
huduma kwa wazee.
Hivyo,
Serikali itaendelea kuwaenzi wazee wetu kwa heshima, usalama na maisha
bora suala ambalo ni msingi na nguzo kwa maendeleo yetu. Maisha bora
yatakuja kama tutawawezesha makundi maalumu katika jamii wakiwemo wazee.
Kwa
kupitia takwimu zilizotolewa na Ofisi ya Takwimu ya Taifa kuhusu sense
ya watu na makazi iliyofanyika Agosti 26, 2012 zinaonesha kuwa kuna
jumla ya wazee Tanzania ni 2,507,568 sawa na asilimia 5.6 ya Watanzania
wote.
Jumla hii inaundwa na wazee wanakiume 1,200,210 sawa na asilimia 5.5 na wanakike 1, 307, 358 sawa na asilimia 5.7
Tofauti na sense ya watu na makazi ya mwaka 2002 ambapo wazee wazee walikuwa asilimia 4.0
Tasira
hii inaonesha kuwa idadi ya wazee nchini imeongezeka kwa tofauti ya
asilimia 1.6, tofauti hii inaonesha taswira na mwelekeo kuwa kuwa idadi
ya wazee chini wataendelea kuongezeka mwaka hadi mwaka.
Itakumbukwa
kuwa tangu mwaka 2002, Tanzania ilipoungana na mataifa mengine duniani
kutia saini ya Mkataba wa Kimataifa wa wazee ilikuwa ni kielelezo tosha
cha kuwathamini wazee na hivyo kuanza kubuni, kuweka mipango mbalimbali
yenye lengo la kuboresha maisha yao
Katika
maadhimisho siku ya Wazee Duniani mwaka huu, Kwa upande wake Naibu
Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dkt. Seif S. Rashid, ametaja kuwa
baadhi ya mipango ambayo Serikali imetekeleza ni pamoja na kuwepo kwa
Sera ya Taifa ya Wazee iliyotungwa 2003 kwa ajili ya kusimamia mipango
na mikakati mbalimbali inayolenga wazee na hivyo kutambuliwa kwao kama
kundi pekee na ushiriki wao katika mipango ya maendeleo ya taifa.
Naibu
Waziri Rashid alikiri na kusisitiza kuwa Serikali itaendelea
kushirikiana na taasisi za hari, hii ni katika hatua ya kuboresha huduma
zitolewazo katika makazi 41 yanayowatunza wazee wenye shida na wasiona
ndugu wa kuwatunza hapa nchini.
Akitoa
msimamo wa Serikali Naibu Waziri alisema, "Thamani ya mchango wa wazee
inatambuliwa na Serikali hasa inapoendelea kuboresha utaratibu wa utoaji
matibabu kwa wazee wote bila malipo".
Eneo hili linaendelea kuboreshwa ili huduma kwa wazee zitolewe bila vikwazo vyovyote.
Kwa
kuzingatia Waraka wa Serikali uliotolewa Februari mosi, 2007, Serikali
imetoa msamaha wa kodi ya majengo wanayoishi wazee na yasiyokuwa ya
biashara.
Ili
kulinda usalama wa wazee, Serikali kwa kushirikiana na Wadau wa
Maendeleo imeendelea kuchukuahatua kali za kisheria kwa wale wote
wanaobainika kujihusisha na mauaji ya wazee.
Vile vile, Serikali itaendelea kuelimisha jamii juu ya madhara yatokanayo na vitendo viovu dhidi ya wazee.
Kwa
kutambua mchango mkubwa na umuhimu wa wazee, Serikali imewashirikisha
wazee katika kutoa maoni yao katika Rasimu ya Katiba ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania kuhusu masuala yao.
Katika
kuwaenzi wazee, ni dhahiri kama taifa litaendelea kunufaika na michango
yao, hivyo hatuna budi kuweka mazingira mazuri zaidi ya kuishi ili
waendelee kuchangia katika maendeleo ya taifa.
Kuwepo
kwa taifa lenye amani ni matokeo ya misingi mizuri walioijenga wazee
wetu tangu hapo awali kwa kuwajali, kuwaenzi watu wote bila kujali umri
na hali zao za maisha katika hatua mbalimbali kama zilivyoainishwa na
Mwanasikolojia Erick Erickson.