JKT RUVU KIBOKO YAO, WANANDINGA ZAIDI YA 600 WAJITOKEZA KUJARIBU BAHATI YAO MBELE YA MINZIRO
https://samchardtz.blogspot.com/2014/05/jkt-ruvu-kiboko-yao-wanandinga-zaidi-ya.html
Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
WACHEZAJI zaidi ya 600 wamejitokeza kufanyiwa
majaribio na kocha mkuu wa JKT Ruvu, Fredy Felix Minziro kwenye viwanja wa
Mlalakuwa jijini Dar es salaam.
Ikiwa katika harakati za kujiimarisha kuelekea
msimu mpya wa ligi kuu soka Tanzania bara, JKT Ruvu imealika wachezaji kutoka
maneno mbalimbali ili kujaribu bahati zao katika kikosi cha kwanza na kikosi
cha vijana.
Meneja wa JKT Ruvu, Kaptein John Sibaya amesema
zoezi hilo lina mafanikio makubwa kwasababu wachezaji zaidi ya 600 wamejitokeza
na benchi la ufundi linajitahidi kwa kila namna kuwajaribu wote.
“Kila mchezaji anacheza kuonesha uwezo wake. Kocha
wetu Minziro anawaangalia na kuchagua wanaofaa katika mipango yake”. Alisema
Kaptein Sibaya.
Sibaya aliongeza kuwa bado wanahitaji kuona vijana
wengi wanajitokeza na mtu akisikia idadi hiyo asiogope bali afike Mlalakuwa ili
kujaribu bahati ya kusajiliwa na JKT Ruvu.
Nao maafande wenzao wa Ruvu Shooting walitumia
mfumo huo wa kutafuta wachezaji wapya chini ya kocha mkuu, Mkenya Thom Alex
Olaba.
Wakati timu hizo zinatafuta wanandinga wapya kwa
mfumo wa majaribio, Kagera Sugar wamesema kusajili kwa kufanya majaribio ya wachezaji
kuna faida ndogo sana.
Kocha msaidizi wa klabu hiyo, Murage Kabange
ameuambia mtandao huu kuwa siku ya majaribio kila mchezaji anajiandaa vizuri,
lakini baadaye anaweza kuigharimu timu.
“Unajua unapoenda kwenye usaili unajiandaa vizuri
kuwashawishi wanaokufanyia usaili. Mnaweza kumuona mchezaji anafaa na
mkamsajili, lakini baadaye asiwepo katika mipango”.
“Sisi tunasajili kwa nafasi. Tunachagua wachezaji
wakati ligi inaendelea na baada ya ligi kumalizika tunasajili wanaotufaa”. Aliongeza
Kabange.