Flatnews

ABDI BANDA: NINAKWENDA SIMBA SC, TANZANIA IJIFUNZE KUTOKA KWA NIGERIA

 


 4
 Abdi enzi hizo akisaini kuitumikia klabu ya Coastal Union ya Tanga
Na Baraka Mbolembole
Kiungo-mlinzi wa timu ya Taifa ya Vijana, U20, na timu ya Taifa ya Tanzania, Abdi Banda ameweka wazi kuwa yupo katika mazungumzo na klabu ya soka ya Simba SC, na endapo watafikia maafikiano atajiunga na mabingwa hao wa zamani wa Tanzania Bara. Banda, ameichezea timu ya Coastal Union kwa misimu miwili, huku msimu wake wa kwanza akicheza kama mchezaji wa timu ya pili. Alianza kucheza ligi kuu katika mzunguko wa pili wa msimu wa 2012/13, mara baada ya Coastal kumsaini akitokea timu nyingine ya Tanga, na mahasimu wa Coastal, timu ya Africans Sports. Mtandao huu utakuwa ukiwaletea mahojiano ya moja kwa moja na wachezaji wa Kitanzania kila siku za wiki, na leo tumeanza na kiungo huyu namba sita, ambaye pia ana uwezo wa kucheza kwa ufasaha nafasi ya ' beki tatu'. Je, Abdi atajiunga na Simba? Maswali na majibu mengi utayapata hapa..
SWALI; Abdi, msimu uliopita ulikuwa na changamoto nyingi, kitu gani umejifunza kama mchezaji?
BANDA; Nimejifunza jinsi ya kulinda kiwango changu kwa kucheza katika timu. Nimegundua kuwa, timu ikifanya maandalizi inafanya vizuri na inakuwa na haki ya kufanya vizuri, kuliko timu inayobahatisha. SWALI; Unamaanisha kuwa, Coastal Union iliangushwa na maandalizi yao? BANDA; Kabla ya kuanza kwa msimu timu ilijiandaa, na ilikuwa na malengo mazuri tu, lakini mara baada ya msimu kuanza timu ilishindwa kulinda nia ya kuchukua ubingwa, ilifikia hatua timu ikapotea kabisa. Tuliangusha lengo kuu.Tulitakiwa kujipanga mwanzo hadi hatua ya mwisho.
SWALI; Kucheza kwako kwa miaka miwili katika timu ya Coastal Union umejifunza kitu gani?
BANDA; Nimejifunza kuwa mpira wa Tanzania unahitaji vitu vingi, Kwanza, ni mchezaji mwenyewe kuwa na malengo kabla ya ligi kuanza, unajiuliza ' nilifanya nini msimu uliopita, na wapi nimekosea'. Nimejifunza kwamba nilipaswa kujipanga na kweli nimejipanga. Uwezo wangu umeonekana, na bado sijafikia mwisho wa uwezo.
SWALI; Ni kweli, Coastal ilikuwa ikifanya maandalizi makubwa katika michezo dhidi ya Yanga na Simba tu?
BANDA; Tulianguka kwa mengi, mwanzo tulikuwa na maandalizi mazuri lakini taratibu hali hiyo ikatoweka. Tulikuwa tukifanya maandalizi makubwa katika michezo dhidi ya Simba na Yanga. Viongozi wanakuwa ‘ bize’ kwa wiki mbili hadi tatu kabla ya mechi hizo, wakati mechi dhidi ya Mgambo wanafanya maandalizi ya siku mbili. ILikuwa ni tatizo, timu ilikpoteza umakini kila mahali. Tulikosa maandalizi ya ligi na kuwa na maandalizi ya mechi Fulani tu.
SWALI; Umekuwa ukifunga magoli ya mbali nini siri ya uwezo wako huo?
BANDA; Mchezaji lazima uwe na vitu, sifa na uwezo wa kufanya vitu binafsi uwanjani kwa maslai ya timu. Mimi ninaamini nacheza mpira, na wachezaji wapo wengi, ila najivunia kuwa na nguvu. Nina nguvu katika miguu yangu na hiyo imekuwa faida kubwa kwangu na maumivu kwa wapinzani wangu. Nafanya sana mazoezi ya miguu, huku nikijiamini nina uwezo wa kupiga mashuti ya mbali. . Kikubwa ni kufanya mazoezi ya mara kwa mara.
 SWALI; Unacheza vizuri katika nafasi ya kiungo na ile ya ulinzi wa kushoto. Sina shaka kuhusu uwezo wako katika matumizi ya mguu wa kushoto, je, unafanya jitihada gani kuboresha mguu wako wa kulia?
BANDA; Hakuna, mchezaji aliyekamilika. Najitahidi sana kubaki katika nafasi yangu, mguu wangu wa kulia hauna nguvu sana kama ule wa kushoto. Hakuna tatizo, kwa kuwa nacheza katika nafasi yangu.
SWALI; Nini, silaha yako kubwa unapokuwa uwanjani?
BANDA; Kumiliki mpira, kupiga pasi za mwisho, na kupiga pasi ndefu.
SWALI; Umecheza, Coastal kwa misimu miwili, vipi, utaendelea kucheza hapo au kuna mahali unafikiria kwenda ili kujiendeleza zaidi kiuchezaji?
BANDA; Kama uwezo wangu umekubalika, nipo tayari kuondoka Coastal.Haiwezekani kila siku mchezaji unabaki timu moja.
SWALI; Kuna uvumi kuwa unakwenda kujiunga na Simba SC, ni kweli, na kipi kinaendelea sasa?
BANDA; Mazungumzo yapo. Mimi kama mchezaji na kwa kipindi kama hiki maneno hayo  lazima yawepo. Kama uwezo wangu umeonekana nipo tayari kusonga mbele. Haiwezekani kila siku mchezaji kucheza klabu moja tu. Mazungumzo ya kujiunga na Simba yanaendelea, tutakapofikia mwafaka kila kitu kitawekwa wazi.
SWALI; Unajisikiaje kutakiwa na Simba?
 BANDA; Mchezaji anapokua kiakili, kimawazo na uwezo ni lazima ufikirie kwenda mbele zaidi. Kutoka, Africans Sports, Coastal hadi Simba itakuwa hatua kubwa kwangu. Kucheza timu kama Simba ni hatua lakini kunakuwepo na changamoto kubwa ya presha ya mashabiki, na hapo ndipo mchezaji unatakiwa kuonyesha ni kiasi gani umekomaa kimpira, kiakili na kimawazo. Kwangu itakuwa kawaida tu, nitacheza kama navyocheza sasa na nipo tayari kwa changamoto mpya.
 SWALI; Kuna wachezaji wengi wazuri walitoka klabu nyingine na kujiunga na Simba wakiwa na viwango vya juu, ila wameishia kucheza kwa viwango vya chini. Je, tutarajie hivyo kwa upande wako?
 BANDA; Katika maisha kila mtu anakuwa na kitu anachotafuta. Tuseme ukweli, wachezaji wengi wa Kitanzania tumelelewa katika mazingira magumu sana. Huwezi kujua, Mtu mwingine akifika pale anajenga hali ya kuridhika na kiasi anachokuwa anakipata kwa kuwa hajawahi kukishika katika maisha yake na kujiona kuwa ameshamaliza. Nitaendelea kuwa, Abdi Banda yuleyule kitabia, sitaridhika zaidi ya kuongeza juhudi na maarifa. Simba si mahala kwa mwisho kwangu, nina ndoto na fikra za kucheza mbele zaidi.
SWALI; Tayari umeshaichezea timu ya Taifa, na leo ( jana) umeiwakalisha timu ya Taifa ya vijana, U20, Ngorongoro Heroes, unachukuliaje kucheza michezo ya kimataifa?
 BANDA; Mpira wa kimataifa si rahisi, unakwenda uwanjani ukiwa humjui mpinzani wako hiyo ni moja ya sababu ya kusema mchezaji amekomaa, kucheza mechi za kimataifa ni tofauti kabisa unapokuwa ukicheza katika ligi kuu yetu. Kadri mchezaji unapokuwa unaongeza idadi ya mechi za kimataifa basi ni lazima uonyeshe umekomaa  kiuchezaji na kuonekana umefikia malengo fulani. Kucheza mechi za kimataifa ni moja kati ya sifa ambazo nazitaka katika maisha yangu ya soka.
SWALI; Ngorongoro wamefungwa leo ( jana) na Nigeria. Timu ilionekana kucheza vizuri, lakini ikaadhibiwa na umakini mdogo wa wachezaji na kujikuta mkipoteza mchezo kwa magoli 2-0, je, kuna nafasi ya kukomboa magoli hayo katika mchezo wa ugenini na kufuzu kwa hatua inayofuata?
 BANDA; Kitu ambacho sisi Watanzania tunakosa ni maandalizi. Maandalizi nikimaanisha kuwa ni lazima tukubali hasara. Tunasema tunahitaji U20, ya leo ndiyo iwe timu ya Taifa, U23 katika kipindi cha miaka miwili, mitatu ijayo kisha ije kuwa timu ya Taifa katika miaka ya mbele. Tanzania hakuna hata mwaka mmoja ambao tunaamini kwamba timu ya ' Taifa ni hii hapa'.Kila siku tunatafuta timu mpya ya Taifa, tunapanga hivi, mara vile.
 Mfano mzuri kwetu ni hawa, Nigeria waliotufunga leo ( jana). Miaka miwili iliyopita walichukua ubingwa wa U17, wamekuzwa vizuri wakawa pamoja, wameongeza wachezaji wawili, watatu na baadae wanataka iwe timu yao ya U23. Tutaweza kushinda vipi na timu kama hii, kwa maandalizi haya hata tukikutana katika U23, miaka mitatu ijayo watatushinda tu. Na, hawajaishia hapo wana mawazo kuwa baada ya miaka kadhaa ijayo iwe timu yao ya Taifa. Ni vigumu kusonga mbele, ila tutakwenda kupambana, mechi bado haijamaridhika.
Kitu gani ungependa kuwaambia wapenzi wa soka Tanzania kuhusu timu zao za Taifa?
BANDA; Wana haki ya kutuzomea, ila wafikirie wanakuwa wakifanya hivyo kwa wachezaji wanaotoka wapi. Leo, mtu anaizomea timu ya Taifa wakati ina wachezaji ambao hawachezi hata ligi ligi kuu. Mashabiki tunajua wanachoshwa na matokeo yetu, ila ni lazima watambue kuwa maandalizi yaliyopo katika timu za TAifa za Vijana ni hafifu sana, watuache tucheze mpira, wasiwe na haraka ya kupata mafanikio wakati ukweli bado hatujafanya uwekezaji katika timu za vijana.
ASANTE, na kila la heri katika mchezo wako.
BANDA; Nawe, pia shukrani sana.
0714 08 43 08

Post a Comment

emo-but-icon

item