Flatnews

SIMULIZI TAMU YA KHADIJA KOPA-9



ILIPOISHIA..
Mbele yake kasimama mwanaume wa Kipemba, yupo hapo kwa kuwa alikuwa akihitaji kuwa mpenzi wake na mwisho wa siku amuoe. Kwa Khadija, kumkubalia mwanaume kwa wakati huo ilikuwa ngumu kwani bado alikuwa na ndoto za kufika mbali kimuziki.
ENDELEA...Malkia wa mziki wa  taarabu, Khadija Omary kopa
“Si kwamba ninaogopa, bado kuna mengi ninatakiwa kuyafanya,” nilimwambia.
“Kwani nikikuoa hautaweza kuyafanya?”
“Hapana. Ninahitaji kuwa huru zaidi.”
“Nakuahidi kukupa uhuru, naomba nikuoe Khadija,” aliniambia mwanaume huyo.
“Haiwezekani.”
“Khadija, nimekuwa shabiki wako kwa kipindi kirefu na kila siku nimekuwa na ndoto za kuwa nawe, nikuoe na kukuweka ndani, naomba uwe nami,” aliniambia kwa sauti ya chini.
Kuna kitu ambacho kama binti niliambiwa sana, kila nilipokuwa nikijisahau, bibi na mama walikuwa wakinikumbusha kila siku kwamba wanaume hawakuwa watu wa kuwaamini kwa kila kitu wanachokisema.
Maneno yale yalinifanya kutokuwaamini kabisa na ndiyo maana kila nilipokuwa nikifuatwa na mwanaume yeyote, msimamo wangu ulikuwa palepale kwamba sikutaka kuingia katika mahusiano ya kimapenzi.
Huyo alikuwa wa kwanza lakini baada yake, walikuja wengi, maneno waliyoyaongea naweza kusema kwamba yalifanana kwa kila kitu. Huyu anakwambia kwamba anakupenda na anatamani uwe wake ili akuonyeshee jinsi anavyoweza kumjali mwanamke, kesho yake, atakuja mwingine na kukwambia vilevile, kama ukiwa mwepesi basi unaweza kumkubalia kila mtu.
“Haiwezekani,” nilisema huku nikitabasamu.
Inawezekana tabasamu langu liliwapa matumaini ya kuendelea kunifuatilia, sikuwa wa kukasirika, mwanaume alipokuwa akija na maneno yake, kawaida yangu nilikuwa nampa nafasi ya kumsikiliza, tena huku nikitoa tabasamu lililowapa matumaini makubwa lakini huwezi amini kwamba jibu langu lilikuwa msumari wa moto mioyoni mwao, yaani lilitofautiana na tabasamu langu lililojengeka usoni mwangu.
“Unajua nini Khadija, mimi nina hela, nimejenga hapa Zanzibar na pia nina mpango wa kwenda kujenga Bara, sasa kwa nini usikubali tu niwe nawe? Haupendi kuwa na raha? Haupendi kwenda kuishi Bara ndani ya jumba lako kubwa?” aliniambia mwanaume mwingine.
Walijipanga foleni kana kwamba wapo bombani, alipotoka huyu, kesho aliingia mwingine. Kiukweli, wengi waliokuja walianzia mbali kabisa, kwanza walianza na kuisifia sauti yangu lakini nilipokuwa nikiwashukuru, walibadilisha mada na kuingia upande mwingine wa mapenzi.
Kiukweli sikupenda lakini sikuweza kuwakataza, niliwapa nafasi lakini nilitakiwa kuwaonyeshea kwamba nilikuwa msichana mwenye msimamo.
Bado kichwa changu kilikuwa na mambo mengi, sikupenda kurudi nyuma, katika ile hatua ambayo nilikuwa nimeifikia, nilitaka nisonge mbele zaidi. Nilitaka kujulikana sana na hatimaye niwe angalau maarufu na nitengeneze fedha kwa ajili yangu na watoto wangu hapo baadaye panapo majaaliwa.
Wanaume waliendelea kunifuata lakini ilikuwa ni kama kutwanga maji kwenye kinu ukitaka yatwangike, kila maneno waliyokuwa wakiniambia, yaliingia sikio la kushoto na kutokea la kulia. Sikupenda kuingia kwenye ndoa, wakati mwingine niliamini kwamba muda wangu wa kuolewa ulikuwa bado, hivyo nilitakiwa kusubiri.

Post a Comment

emo-but-icon

item