Sakata la makato Ligi Kuu latinga Bungeni
Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo, Juma Nkamia SAKATA la makato ya fedha za map...
http://samchardtz.blogspot.com/2014/11/sakata-la-makato-ligi-kuu-latinga.html
Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo, Juma NkamiaAidha serikali imesema kwamba Chama cha Soka cha Dar es Salaam (DRFA) kinanufaika zaidi na mapato hayo bila kuyafanyia kazi.
Kauli hiyo ilitolewa jana bungeni na Naibu Waziriwa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Juma Nkamia alipokuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Tabora Mjini, Ismail Aden Rage (CCM) aliyetaka kujua kama serikali ina habari kuwa makato yanayokatwa kwa klabu za Ligi Kuu ni makubwa.
Akijibu swali hilo, Nkamia alisema DRFA inapata fedha nyingi zinazotokana na mapato ambazo hazijulikani zinakwenda wapi na zinafanya kazi gani na kuongeza kuwa: “ni lazima sasa tuchukue hatua”.
Alikiri kuwa makato yanayokatwa klabu hizo ni makubwa na kwamba aliwahi kukutana na viongozi wa Bodi ya Ligi, Shirikisho la Soka nchini (TFF) pamoja na wadau wengine wa soka ili kuangalia namna ambavyo makato hayo yatakavyopungua ili klabu zipate wanachostahili.
“Kwa mfano, katika fomu ile ya makato kuna makato ya aina mbili… kwa mfano DRFA katika mechi moja wanapata mapato mara mbili kwenye ile fomu ya mgawanyo…na hawana kazi yoyote nyingine wanayofanya zaidi ya kusubiri mapato... “Sasa timu za vijana wanaohangaika ni TFF na serikali… lakini mapato yale yanayokatwa ni makubwa kupita kiasi tumezungumza nao tuone ni jinsi gani ya kupunguza makato hayo…leo ni timu kubwa mbili tu ndiyo ambazo zinaweza kuingiza mapato mengi ni Yanga na Simba, Yanga ikicheza na Ndanda inaingiza mapato mengi sana kuliko Ndanda ikicheza na Stand United lakini makato yanayokatwa ni yale yale,” alisema Nkamia aliyewahi kuwa katibu mwenezi wa Simba miaka ya nyuma.
Alisema kwa sasa wanachoangalia ni namna gani makato hayo yanayotokana na mapato yapungue ili klabu hizo zijiendeshe zenyewe.
Kwa muda mrefu suala la makato ya milangoni limekuwa likilalamikiwa na klabu za Ligi Kuu huku mazungumzo yakifanyika mara kwa mara bila kupata suluhu.
Katika hatua nyingine, Nkamia aliipongeza Yanga kwa kujiunga na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) huku wachezaji wake wakiwa mbioni kupatiwa mikopo ya nyumba kupitia mfuko huo.
“Wachezaji wengi nchini waliozaliwa kwa kucheza mpira wana maisha mabaya sana, Jela Mtagwa ni miongoni mwao aliishi katika maisha ya tabu hususan alipokuwa akiugua,” alisema Nkamia.