KIBADENI ATANGAZA KUSTAAFU UKOCHA, AANZISHA AKADEMI IITWAYO
http://samchardtz.blogspot.com/2014/11/kibadeni-atangaza-kustaafu-ukocha.html

Kocha wa zamani wa Simba na Ashanti United, zote za jijini Dar es Salaam, Abdallah ‘King’ Kibadeni ametangaza kuachana rasmi na kazi ya ukocha na kuamua kuanzisha kituo cha kulelea vijana wenye vipaji vya michezo ‘akademi’.
Akizungumza na, jijini Dar es Salaam leo Kibadeni mwenye rekodi pekee ya kufunga mabao matatu katika mechi moja (hat-trick) katika mechi ya watani wa jadi, Simba na Yanga, amesema amechukua uamuzi wa kuachana na ukocha ili kuepuka malumbano na kuzongwa na viongozi pindi timu inapokuwa na matokeo yasiyoridhisha.
“Nipo hapa Sinza (Dar es Salaam), nilifanya ‘operation’ (upasuaji) ya jisho tarehe 6 mwezi huu (Novemba). Nina mipango maalum kujenga akademi Chanika. Akademi hiyo itaaitwa KISA yaani Kibadeni Soka Academy ambayo pia itakuwa na michezo mingine mbali na soka.
“Itakuwa na vijana wenye umri kuanzia miaka 12 hadi 18 na nitakuwa na watu wengine watakaonisaidia katika shughuli hiii. Tutakuwa na timu pia yenye vijana wenye umri usiozidi miaka 23.
“Nitakuwa ninasaka vijana wenye vipaji na kulea wale ambao nitaletewa na klabu. Kwa elimu yangu ninaona kuna umuhimu wa kufanya hivyo maana Taifa limenisaidia kusoma sehemu mbalimbali, nina elimu ya kutosha kwa sasa. Ninaona sihitaji kulumbana na viongozi wa timu nikiwa kama kocha. Bora nifanye shughuli nyingine.
“Eneo nililonalo linatosha kujenga hata viwanja viwili vitatu vikubwa kwa ajili ya soka, mpira wa kikapu na michezo mingine. Ninamuomba Mungu anijalie nipone haraka niendeleze mpango huu,” amesema Kibadeni.
Kabla ya kutua Ashanti United mzunguko wa pili msimu uliopita wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL), Kibadeni aliiongoza Simba akiwa kocha mkuu lakini akatimuliwa kibabe pamoja na aliyekuwa msaidizi wake, Jamhuri Kihwelu ‘Julio’, timu hiyo ya Msimbazi ikiwa nafasi ya nne katika msimamo wa VPL ikizidiwa pointi nne tu na waliokuwa vinara wa msimamo, Yanga.
Baadaye aliletwa kocha Mcroatia Zdravko Logarusic ambaye alishinda mechi tatu tu mzunguko wa pili huku timu ikifungwa na JKT Ruvu, Azam, Mgambo Shooting, Coastal na Ashanti United.