Mwanamke Auawa kwa Kupigwa Risasi na Polisi Kwa Bahati Mbaya
http://samchardtz.blogspot.com/2014/10/mwanamke-auawa-kwa-kupigwa-risasi-na.html
Mwanamke
mmoja mkazi wa Kijiji cha Iglansoni, ameuawa kwa kupigwa risasi
kichwani kwa bahati mbaya na askari polisi waliokuwa katika jitihada za
kumkamata mtuhumiwa wa ujambazi.
Aliyeuawa ni Joyce
Maragabu (65), ambaye anadaiwa kupigwa risasi na askari hao waliokuwa
wakijihami na kundi la watu waliotaka kuwavamia ili wasimkamate mhalifu.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa
Singida, Geofrey Kamwela, alisema askari hao walikuwa wanataka
kumkamata, Nkida Gwisu, anayetuhumiwa kumshambulia mtu mwingine, lakini
kwa bahati mbaya risasi hiyo ikampiga kichwani mwanamke huyo aliyekuwa
anafua nguo nyumbani kwake.
Kamwela alisema, tukio hilo lilitokea juzi Oktoba 16, saa 6 mchana.
Alisema askari polisi
wawili ambao hakuwataja majina yao wa kituo kidogo cha polisi Ihanja,
walifika katika kitongoji hicho ili kutoa ulinzi mnadani, lakini baadaye
walipewa taarifa kuhusu mtuhumiwa huyo kumshambulia mmoja wa
wanakijiji.
Alisema wakati wakiwa
katika jitihada ya kumtafuta mhalifu huyo, alitokea mwananchi mmoja
aliyedai kumfahamu mtuhumiwa huyo, hali iliyorahisisha kazi ya kumkamata
na kumweka chini ya ulinzi.
Hata hivyo, alisema
baadaye mtuhumiwa huyo alianza vurugu, hali iliyosababisha kundi kubwa
la watu kwenda eneo hilo wakiwa na silaha za jadi ikiwamo mawe, pinde,
mishale, fimbo na mapanga, na kuanza kumshambulia mmoja wa askari polisi
aliyemshikilia mhalifu huyo.
Alisema kuwa katika hali
ya kutaka kumwokoa mwenzake, askari aliyekuwa na bunduki alifyatua
risasi moja ya moto hewani, lakini hata hivyo wakiwa kwenye purukushani,
ndipo risasi moja ilifyatuka na kumpiga kichwani mwanamke huyo.
Kamwela alisema baada ya
tukio hilo, wananchi waliokuwa na hasira waliichoma moto pikipiki ya
askari hao, yenye namba za usajili PT 3242 –Yamaha na kuiteketeza.
Alisema kutokana na
vurugu hizo, askari hao walijeruhiwa vibaya baada ya kupigwa na kundi
hilo na tayari jeshi hilo linawashikilia askari hao kwa mahojiano
zaidi.
Chanzo:Nipashe
