Flatnews

MAONI: Aibu ya timu za Madola ni Watanzania wote


Tanzania inawakilishwa na wanamichezo 44 wa judo, riadha, ngumi, kuogelea, mpira wa meza, kunyanyua vitu vizito na baiskeli, walikaa kambini kwa miezi mwili tu baada ya kupata ufadhili wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikano wa Kimataifa.



Michezo ya Jumuiya ya Madola imemalizika jana  jijini Glasgow, Scotland huku Tanzania ikitoka mikono mitupu.
Tanzania tulipeleka wanamichezo katika michezo  riadha, ngumi, baiskeli, kuogelea, mpira wa mezana Judo.
Msafara wa Tanzania katika michezo ya madolaulijumuisha watu 60 wakiwamo wanamichezo ambao lengo lao kubwa lilikuwa ni kuleta medali mbalimbali nchini.
Lakini maandalizi kwa ajili ya mashindano hayo kwa wanamichezo yetu yalikuwa duni kulinganisha na michezo Madola ilivyo mikubwa.
Tanzania inawakilishwa na wanamichezo 44 wa judo, riadha, ngumi, kuogelea, mpira wa meza, kunyanyua vitu vizito na baiskeli, walikaa kambini kwa miezi mwili tu baada ya kupata ufadhili wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikano wa Kimataifa.
Tulizungumzia sana suala la maandalizi miezi mingi kabla wanamichezo wetu hawajaenda Glasgow kwa ajili ya michezo hiyo ya Madola, kwa sababu wanamichezo wa Tanzania wanaposhiriki michezo ya kimataifa huwa wanabeba dhamana ya Watanzania wote na wanapofanya vizuri ni heshima ya nchi na wanapofanya vibaya ni aibu ya Tanzania.
Michezo hii ya Madola hujumuisha nchi mbalimbali wa wanachama wa Jumuiya ya Madola, hivyo Serikali ilitakiwa kuhakikisha wanamichezo wetu watakaoiwakilisha Tanzania kwa ajili ya kuleta heshima wanaandaliwa mapema na katika kiwango cha juu.
Nchi mbalimbali ziliandaa wanamichezo wao kwa ajili ya kuhakikisha zinatwaa medali nyingi katika mashindano hayo na zilifanikiwa kwa sababu zilitwaa medali nyingi.
Katika hali iliyotushangaza Tanzania tuliingiza wanamichezo wetu kambini katika dakika za mwisho hivyo hakukuwa na dalili ya kufanya vizuri katika michezo ya Madola kwa sababu ya maandalizi yetu ya zimamoto.
Mara kwa mara tumekuwa tukishuhudia maandalizi ya zimamoto wanayofanyiwa wanamichezo wetu kila mwaka inapobaki mwezi mmoja au wiki mbili kabla ya mashindano kuanza wakati tulikuwa na muda mrefu wa kuwafanyia maandalizi mazuri vijana wetu wanaoenda kuiwakilisha Tanzania.
Tanzania ilifanya vibaya michezo ya Olimpiki 2012,  na hivi sasa tumevurunda katika michezo ya Madola 2014.
Tunakumbuka miezi sita kabla ya kuanza kwa michezo ya Madola tulikuwa tukiikumbusha serikali na TOC kuwaandaa wanamichezo wetu mapema kwa kuwaingiza kambini kwa ajili ya maandalizi na kuwapatia mechi za kirafiki za kutosha.
Mara nyingi kushindwa kwa Tanzania katika michezo ya kimataifa huonekana mapema na hutokana na mwenendo mzima wa kambi za maandalizi ya wanamichezo wetu hivyo wanamichezo wetu kushindwa katika michezo hii ni uzembe wa serikali na vyama vya michezo na siyo uzembe wa wanamichezo.
Tunapenda kusema tunahuzunishwa sana na maandalizi duni ya timu zetu za taifa ukiacha timu ya soka, pia hatuoni umuhimu wa timu hizo kuitwa za taifa wakati wananchi, makampuni, serikali hawazisaidii timu hizi za taifa.
Tunaamini timu yetu ya taifa iwe ya riadha, ngumi au mchezo mwingine, inapofanya vizuri kila Mtanzania hujisikia raha, kwa hiyo upo umuhimu wa haraka wa timu za taifa  kusaidiwa vifaa na fedha.
Tunajua kwamba Watanzania wamechoka kuwa wasindikizaji  kwa sababu wanamichezo wao kufanya vibaya kila kukicha ni wajibu wetu kila moja kwa nafasi yake kutoa mchango wa hali na mali ili kufanikisha maandalizi ya timu hizi zitazokwenda kupeperusha bendera nchi DR Congo 2015 na Brazil 2016.
Waswahili wanasema Ng'ombe anenepi siku ya mnada, hivyo ni wajibu wa BMT, TOC na vyama   kuwahimiza wadhamini kutoa udhamini wao mapema kwa lengo la kusaidia maandalizi ya timu zetu kuwa kwenye kiwango bora kuliko ilivyokuwa sasa.

Post a Comment

emo-but-icon

item