Flatnews

Wazee walikoroga mdahalo wa Katiba Mpya

 


 

Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Kitila Mkumbo akitoa mada kwenye kongamano lililokuwa likijadili mchakato wa Katiba Mpya, lililofanyika kwenye Ukumbi wa Nkrumah, Dar es Salaam jana. Picha na Venance Nestory 
Na Andrew Msechu na Elias Msuya

Posted  Jumatatu,Agosti4  2014  saa 9:12 AM
Kwa ufupi
Baada ya mwenyekiti wa mjadala, Profesa Francis Mhilu kueleza kuwa ni muda wa kupata busara za wazee, alimwita mzee George Mgodawivaha aliyesifu jitihada za Rais Jakaya Kikwete kuhakikisha kuwa Katiba Mpya inapatikana, lakini mambo yaliharibika pale alipoanza kumshambulia aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba.


Dar es Salaam. Wazee walioalikwa kutoa busara zao katika mdahalo wa Katiba jana walilikoroga baada ya kutoa maoni ambayo yaliwakera wasikilizaji waliokuwa katika Ukumbi wa Nkrumah wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), hivyo wakawazomea na kuwatimua jukwaani.
Baada ya mwenyekiti wa mjadala, Profesa Francis Mhilu kueleza kuwa ni muda wa kupata busara za wazee, alimwita mzee George Mgodawivaha aliyesifu jitihada za Rais Jakaya Kikwete kuhakikisha kuwa Katiba Mpya inapatikana, lakini mambo yaliharibika pale alipoanza kumshambulia aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba.
“(Rais) alimwamini sana huyu mheshimiwa Joseph Warioba ambaye katika rasimu hii hakuitendea haki nchi,” alisema Mgodawivaha ambaye baada ya kumaliza sentensi hiyo alizomewa na sehemu ya wasikilizaji wakimtaka aache kupoteza muda.
Kelele zikazidi, ilibidi aondoke kwenye mimbari na kwenda kuketi. Baada ya ‘busara’ za Mgodawihava kukataliwa, mwenyekiti wa mdahalo alimwita, Dk Emmanuel Makaidi (Mwenyekiti wa NLD), ambaye alianza kwa mbwembwe za kuishambulia CCM kuwa yeye hajawahi kuwa sehemu yake tangu kabla ya uhuru.
Alisema alikuwa kwenye chama cha Congress, chini ya Zuberi Mtemvu na kuwa tatizo lililopo ni kuwa watu wanaoharibu nchi ndiyo leo wanaoambiwa waitengeneze.
“Hatuna Tanganyika yetu halafu mnatuambia nini, Wasira (Stephen, Waziri Ofisi ya Rais, Uhusiano na Uratibu), sijui anatuambia nini hapa wakati nchi ishawekwa rehani,” alisema Dk Makaidi, kauli iliyosababisha upande mmoja wa wasikilizaji kuanza kuzomea, huku akisisitiza kuwa anataka kumalizia hoja zake.
Hata hivyo, alikwama kuendelea baada ya kelele kuzidi na kuishia kuondolewa jukwaani kabla ya kuitwa vijana kutoa maoni yao.
Akizungumza baada ya madahalo huo, Mgodawihava alisema Jaji Warioba alikosema kuweka kwenye Rasimu serikali tatu na badala yake angeliwaachia wananchi wenyewe waamue kama ni mbili au tatu.
Wakati mdahalo unakaribia mwisho, wazungumzaji, Wasira na Tundu Lissu (Chadema) wakiwa wamehitimisha mada zao, sehemu kubwa ya wajumbe waliamua kuondoka baada ya kutolewa nafasi kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi kufunga mdahalo na alitumia nafasi hiyo kujibu hoja za Ukawa.
Baadhi ya wajumbe walimzomea lakini yeye akawaambia waendelee kumzomea kwa kuwa alikwishazoea hali hiyo. Akizungumza baadaye, Lukuvi aliweka bayana kuwa Bunge halitaahirishwa.
Alimnyooshea kidole Lissu kuwa ndiye “kimzizi cha Ukawa” akifafanua kuwa kama kuna mchawi wa Ukawa, basi Lissu ndiye mchawi namba moja, akimaanisha kuwa yeye ndiye mshawishi mkubwa wa mambo ambayo umoja huo unayapigania.
KWA STORI KAMILI BOFYA HAPA 

Post a Comment

emo-but-icon

item