Majambazi wampora meneja Kampuni ya Olam Sh47 milioni
http://samchardtz.blogspot.com/2014/08/majambazi-wampora-meneja-kampuni-ya.html
Askari polisi wakiwa kwenye doria. Picha ya Maktaba
Majambazi hao walifanya tukio hilo eneo la Tabata
TioT baada ya kumfuatilia kwa nyuma kijana huyo akitokea duka la Quality
Plaza alipokwenda kuchukua fedha hizo kutoka Benki ya DTB.
Dar es Salaam. Majambazi wenye silaha juzi
mchana walimpora meneja wa Kampuni ya Ununuzi wa Korosho na Ufuta ya
Olam, Jafari Mgumba takriban Sh47 milioni.
Katika tukio hilo la kushangaza baada ya kuporwa,
meneja huyo alitoweka eneo la tukio na polisi walipofika eneo hilo muda
mfupi baadaye walishindwa kuchukua hatua zozote hadi alipokwenda
mwenyewe baadaye kuripoti unyang’anyi huo.
Majambazi hao walifanya tukio hilo eneo la Tabata
TioT baada ya kumfuatilia kwa nyuma kijana huyo akitokea duka la Quality
Plaza alipokwenda kuchukua fedha hizo kutoka Benki ya DTB.
Hata hivyo, baada ya kuporwa fedha hizo, Mgumba
alitokomea bila kutoa taarifa polisi, hatua iliyosababisha kuunganishwa
na watuhumiwa. Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ilala, Maria Nzuki alisema
mlalamikaji huyo alishikiliwa na kuhojiwa kwa makosa mawili ili
kujiridhisha kama anahusika au hahusiki na tukio hilo.
“Alikuja na kujitambulisha kama mfanyabiashara wa
kununua mazao ya korosho na ufuta wa Kampuni ya Olam iliyopo Dar es
Salaam, lakini ikabidi tumshikilie kwa sababu ya kuchelewa kutoa taarifa
polisi pamoja na kutotumia askari kusindikiza fedha hizo, ulinzi ambao
hutolewa bure,” alisema.
“Kwa madai yake anasema alipoibiwa akakimbilia ofisini kwao kutoa taarifa halafu ndipo akaja kituoni,” alisema Kamanda Nzuki.
Tukio lilivyotokea
Tukio hilo lilitokea juzi saa 7:00 mchana jirani na Benki ya NMB, Tawi la Mandela Road.
Mwandishi wa habari alifika eneo la tukio na
kukuta idadi kubwa ya watu wakiwa na hofu baada ya majambazi hao
kufyatua risasi tatu hewani.
Kabla ya majambazi hao kupiga risasi hewani,
Mgumba alijaribu kupiga kelele za “wezi, wezi,”, lakini akatishiwa
bunduki na kulazimika kunyamaza.
Kutokana na kitendo hicho, watu waliokuwa eneo hilo walitimka kujiokoa na wengine wakilala chini ya vibanda vyao.
Mmoja wa wafanyabiashara katika eneo hilo,
aliyejitambulisha kwa jina la Ali alisema risasi zilipigwa baada ya raia
huyo kupiga kelele za mwizi.