CCM wacheza shere Katiba mpya
http://samchardtz.blogspot.com/2014/08/ccm-wacheza-shere-katiba-mpya.html

VUGUVUGU la kutaka Bunge Maalum la Katiba lisitishe shughuli zake, limezidi kushamiri baada ya baadhi ya wajumbe kuanza maandalizi ya kuandika barua kwa Rais Jakaya Kikwete, wakimwomba alisitishe kwa madai kwamba wajumbe wanacheza shere pasipo dalili za kuzaa katiba mpya.
Miongoni mwa wajumbe hao wengi kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM), wamelidokeza Tanzania Daima kuwa wanasubiri Rais Kikwete amalize ziara yake nchini Marekani ili wamfikishie ujumbe huo.
Walibainisha kuwa wamefikia hatua hiyo baada ya kubaini uwezekano wa kupatikana kwa Katiba mpya ni mdogo ingawa baadhi ya wenzao wanataka liendelee kwa ajili ya kuchuma posho.
Wamedokeza kuwa vikao vya Bunge Maalum, vinavyoendelea haviwezi kufanikisha Katiba mpya kwa kuwa uamuzi hautafikiwa kutokana na theluthi mbili ya kura inayotakiwa kila upande kuwa vigumu kwa Zanzibar.
Kwamba, kwa mujibu wa sheria ya mabadiliko ya katiba namba 26 na Katiba ya mwaka 1977 toleo la 2005 ibara ya 98, inaweka masharti ya kupitisha jambo linalogusa masuala ya muungano.
Masharti hayo ni kuwa ili uamuzi wa kupitisha jambo husika uwe halali ni lazima ipatikane theluthi mbili ya kura za wajumbe wote kutoka Zanzibar na idadi hiyo hiyo kwa Tanzania Bara.
Kama masharti hayo hayatotimizwa Bunge haliwezi kuandika Katiba inayopendekezwa itakayopelekwa kwa wananchi kupigiwa kura ya maoni.
Wasiwasi wa kutopatikana kwa theluthi mbili unatokana na wajumbe wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), kususia vikao vya Bunge hilo wakipinga CCM kuipindua rasimu iliyotokana na maoni ya wananchi.
Uamuzi huo wa UKAWA hasa kwa wajumbe kutoka Zanzibar (CUF), unadaiwa kuweka njia panda upatikanaji wa Katiba mpya kwakuwa bila ushiriki wao theluthi mbili kwa Zanzibar haipatikani.
Hofu ya kutopatikana kwa theluthi mbili ndiyo iliyomfanya Naibu Katibu Mkuu wa CCM (Bara), Mwigulu Nchemba, aliyetaka Bunge lijifanyie tathimini kama lina ulazima wa kuendelea na vikao vyake.
Mwigulu alisema lifanye tathimini hiyo ili kujua kama litakuwa na uwezo wa kupata theluthi mbili ya kura za uamuzi zinazotakiwa kila upande na kama hazitopatikana lisitishwe.
Anasema likiendelea na vikao vyake bila kufanya tahimini hiyo kuna uwezekano mkubwa mwisho wa safari wasiwe na uwezo wa kuamua, hivyo kupoteza mabilioni ya fedha za Watanzania.
Kauli hiyo ya Mwigulu, imeonekana mwiba mkali kwa wenzake wa CCM ambao wanamshambulia kuwa alipaswa kuitoa ndani ya vikao vya chama na si bungeni, wanadai kuwa yeye ni kiongozi mkubwa wa chama, hivyo hatakiwi kuzungumzia mambo yanayokipasua nje ya vikao vya ndani.
Idadi kubwa ya wajumbe wanaomshambulia Mwigulu, wanahofia kusitishwa kwa Bunge hilo kutawafanya wakose posho ya sh. 300,000 wanayoipata wanapohudhuria vikao ambapo sh. 230,000 ni ya kujikimu na 70,000 ya kikao.
Tayari baadhi ya wajumbe wameshafanya hesabu katika siku 84 watakazokaa Dodoma watapata sh. milioni 25.6
Watakaa siku hizo baada ya Rais Jakaya Kikwete kuridhia pendekezo la uongozi wa Bunge Maalum la kuwaongezea siku 60 za kumalizika kazi waliyoianza Februari mwaka huu.
Hata hivyo siku hizo 60 hazihusishi Jumamosi, Jumapili na siku za sikukuu tofauti na ilivyokuwa mwanzo ambapo Jumamosi ilikuwa ni sehemu ya siku za kazi.
Hoja ya Mwigulu imeanza kupata mashiko mapya baada ya kujitokeza kwa makada wenzake wanaotaka mchakato huo uahirishwe.
Wanaomuunga mkono Mwigulu sasa wanawashambulia wenzao wanaong’angánia vikao viendelee wakijua havitazaa matunda yaliyotarajiwa.
“Hapa hakuna kitu kinachofanyika, ni upotezaji wa fedha za umma, tunafanya vikao vitakavyokwama mwishoni, tusitishe kwanza mpaka tutakapopata muafaka,”alisema mmoja wabunge wa CCM.
Aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko Jaji Joseph Warioba, naye ameshaweka wazi kuwa kuendelea kwa Bunge hilo ni kutafuna fedha za wananchi kama uamuzi utakaofanywa hautakidhi masharti yanayotakiwa.
Warioba alitaka lisitishwe ili yatafutwe maridhiano yakayojenga uhalali na kukubalika kwa Katiba itakayotunga.
Hofu ya kukosekana kwa theluthi mbili imelifanya Bunge Maalum kubadili kanuni ya 35 iliyokuwa ikiruhusu kujadiliwa kwa sura mbili zinazofana kisha kupigiwa kura ibara kwa ibara.
Sasa kanuni hiyo imebadilishwa na kuruhusu kujadiliwa kwa sura 15 au zaidi kwa pamoja na kupigiwa kura, hili nalo limeleta mkwamo katika baadhi ya kamati na hivyo wajumbe kuamua kuburuza ibara zote bila kupiga kuwa ya kuzipitisha.