Magufuli aahidi kivuko Kigamboni
http://samchardtz.blogspot.com/2014/08/magufuli-aahidi-kivuko-kigamboni.html

WAZIRI wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, amesema Serikali inatarajia kuongeza kivuko kipya kitakachogharimu sh. bilioni 3.7 kwaajili ya kuvusha watu Kigamboni.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam katika ziara ya ukaguzi wa kivuko cha Msangamkuu, daraja la Kigamboni na feri, Dk. Magufuli alisema kuwa kivuko hicho kitasaidia kutoa huduma upande wa Kigamboni na Feri ikiwa ni muendelezo wa kupunguza msongamano.
Kuhusu daraja la Kigamboni, aliwataka wakandarasi kuhakikisha linamalizika Juni mwakani, badala Julai kama walivyoomba.
Alisema kuwa ujenzi wa daraja hilo umekamilika kwa asilimia 60, ambapo mpaka sasa mkandarasi ameshalipwa sh. bilioni 117 kati ya sh. bilioni 214 za mradi huo.
Akizungumzia fidia ya wakazi wa Vijibweni, alisema tayari ameshalipwa jumla ya sh. bilioni 11.7 ili kupisha ujenzi wa barabara kutoka darajani.
Alisema daraja hilo litakuwa na njia sita za magari na mbili za watembea kwa miguu, ambapo pia ujenzi wa barabara za juu umeanza kufanyiwa kazi.
Pia alisema kuwa Oktoba mwaka huu, barabara za juu eneo la Tazara, barabara ya Mandela, Ubungo na Kamata zitaanza kujengwa lengo likiwa ni kuondoa msongamano ndani ya jiji.
Mkurugenzi wa Wakala wa barabara (Tanroads), Mhandisi Patrick Mfugale, alisema ujenzi wa daraja ulikutana na changamoto katika nguzo ya nane iliyopo katikati ya bahari.
“Ule mwanya ilibidi wahandisi wafanye uchunguzi, na ndipo walioungundua na kuufanyia kazi kwa kuujenga kwa chini kwa mita 84, lakini changamoto ya ardhi nayo ilichelewesha mradi huo, ila sasa hali ni nzuri na utakamilika kwa wakati,”alisema.
Kaimu Mkurugenzi wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF),Ludovick Mrosso, alisema kuwa mfuko huo utaendelea kushirikiana na serikali katika maendeleo.
BOFYA HAPA