MICHAEL WAMBURA KIKAANGONI TENA KWA WAKILI LUGAZIYA
http://samchardtz.blogspot.com/2014/06/michael-wambura-kikaangoni-tena-kwa.html
Atamrudisha Wambura tena?: Wakili Julius
Lugaziya (katikati) alipokuwa anatangaza maamuzi ya kumrudisha Wambura na leo
hii wanakutana tena kujadili rufani ya pili.
KWA mara ya pili kamati ya Rufani ya uchaguzi ya
TFF inakutana leo mchana kujadili rufaa iliyokatwa na mgombea wa Urais katika
uchaguzi wa Simba sc, Michael Richard Wambura akipinga kuenguliwa tena katika
kinyang`anyiro hicho.
Mwenyekiti wa kamati hiyo, Wakili Julius Mutabazi
Lugaziya amesema rufaa hiyo ipo mezani na majira ya saa 8 mchana watakaa na kuijadili,
huku akiweka wazi kuwa haki itatendeka kwa mrufani.
Mwishoni mwa wiki, Rais wa shirikisho la soka
Tanzania, TFF, Jamal Emil Malinzi alitangaza kusimamisha uchaguzi wa Simba
akiitaka kamati ya utendaji kuunda kamati ya maadili ili kusikiliza kesi zote
za maadili zinazoigubika klabu hiyo.
Igizo la Malinzi lilipingwa na kamati ya uchaguzi
ya Simba kwa kueleza kuwa hana mamlaka kikatiba kusimamisha uchaguzi , hivyo
uchaguzi uko pale pale yaani juni 29.
Hata hivyo, Rais wa Simba sc, Ismail Aden Rage
akiwa mjini Dodoma katika ukumbi wa Idara ya habari Maelezo alizungumza na
waandishi wa habari na kueleza kuwa amezunguza na Rais Malinzi akimuomba
uchaguzi ufanyike juni 29 ili kuinusuru klabu hiyo.
Rage alifafanua kuwa kamati ya maadili anayoagiza
Malinzi iundwe na kamati ya utendaji haitatenda haki kwasababu robo tatu ya
wajumbe ni watuhumiwa wa maadili.
Kujitafutia majaji wa kuwahukumu wao wenyewe haki
haitatendeka, hivyo akamuomba Malinzi masuala hayo yarudhishwe kamati za TFF.
Kwa mujibu wa maelezo ya Rage, tayari Malinzi
alisharidhia maombi hayo na kumtaka aandike barua ambayo tayari Rage
alishapeleka na kwasababu hiyo kamati ya Rufani imepata nguvu ya kuijadili
rufani ya Wambura.
Awali kamati ya maadili ya TFF ilitakiwa kukutana
wiki iliyopita kujadili malalamiko ya wanachama wa Simba kuhusu baadhi ya
wagombea kwenda kinyume na maadili kikatiba hasa wakati huu wa uchaguzi, lakini
kutokana na agizo la Malinzi haikuwezekana tena.
Wakili Lugaziya amesema kutokana na maelewano ya
Rage na Malinzi kuna uwezekano uchaguzi utafanyika juni 29 na ndio maana
wanakutana kujadili rufani ya Wambura.
“Rufani imekuja, nikawaambia wenzangu nina muda
leo saa 8, hivyo tutakaa muda huo kujadili”. Alisema Wakili Lugaziya.
“Kama Wambura ana haki atapata, mara ya kwanza
sikumbeba, alikuwa na haki akapewa. Na sasa tutaangalia, kama atakuwa na haki
atapata, kama atakuwa hana atakosa”. Aliongeza Wakili Lugaziya.
Wambura alienguliwa mara ya kwanza na kamati ya
uchaguzi ya klabu ya Simba chini ya mwenyekiti wake, wakili Dkt. Damas Daniel
Ndumbaro kwasababu kubwa mbili ambazo ni kuipeleka Simba mahakamani na
kusimamishwa uanachama.
Lakini Wambura alikata rufaa akipinga maamuzi hayo
na kamati ya rufani ikamrudisha katika uchaguzi kwasababu Simba walimuacha
akifanya shughuli za klabu kama mwanachama hai ikiwemo kulipa ada baada ya
kutangaza kumsimamisha mwaka 2010.
Hata hivyo kamati ya Simba ililazimika kumuengua
tena kwa madai kuwa Wambura alizungumza maneno yanayoenekana ni kampeni baada
ya kurudishwa na wakili Lugaziya.