Jeshi la Urusi lawekwa katika tahadhari ya mapambano
http://samchardtz.blogspot.com/2014/06/jeshi-la-urusi-lawekwa-katika-tahadhari.html
Rais Vladimir Putin wa Urusi ameviweka vikosi vyake vilioko Urusi ya
kati katika "tahadhari kamili ya mapambano" na kuwaamuru wanajeshi
65,000 katika eneo hilo kujiandaa kwa kufanya luteka za kijeshi za wiki
moja.
Wanajeshi wa Urusi.
Waziri wa ulinzi wa Urusi Sergei Shoigu amesema mazoezi hayo ya kijeshi
ya angani na ardhini katika maeneo ya milima ya Volga na Ural
yatafanyika kuanzia Jumamosi Juni 21 hadi Juni 28.Jumuiya ya Kujihami ya NATO imesema mapema wiki hii kwamba Urusi imerudia tena kurundika wanajeshi wake kwenye mpaka na Ukraine ambapo waasi wanaotaka kujitenga wamekuwa wakipambana na vikosi vya serikali kwa wiki kadhaa katika mzozo uliogharimu maisha ya watu 300 na kuwapotezea makaazi wengine 34,000.
Luteka hizo za kijeshi zinakuja siku moja baada ya Rais Petro Poroshenko wa Ukraine kutangaza wiki moja ya usitishaji wa mapigano na waasi wanaoiunga mkono Urusi mashariki ya nchi hiyo ikiwa ni sehemu ya mpango wa amani wa vipengele vinne ambao pia unajumuisha msamaha na ahadi ya kufanyika kwa marekebisho ya katiba.
Serikali ya Urusi imeishutumu mpango huo wa Poroshenko kuwa ni "amri" ambao hautopelekea kupatikana kwa ufumbuzi wowote ule na waasi wameukataa wito wake wa kuwataka wasalimishe silaha zao.
Mapigano mapya
Kumekuwepo na ripoti za mapigano Jumamosi ambapo waasi wanaotaka kujitenga wanaoiunga mkono Urusi wamevishambulia vituo vya Ukraine karibu na mpaka na Urusi na kambi moja ya kijeshi na pia kujaribu kuivamia kambi ya anga wakati wa usiku.
Rais Petro Poroshenko akiwasalimia wanajeshi katika kambi ya kijeshi katika mji wa Svyatogorsk mashariki ya Ukraine.(20.06.2014)
Mapigano hayo yamekuja saa chache tu baada ya kuanza kwa
usitishaji wa mapigano wa vikosi vya Ukraine Ijumaa saa nne usiku na
kuuweka mpango huo wa Rais Poroshenko mashakani.Msemaji wa vikosi vya serikali amesema waasi wanaotaka kujitenga walitumia mizinga na kufanya mashambulizi ya kuvizia dhidi ya vituo vya Ukraine vya Izvareno na Uspenska vilioko mpakani na kuwajeruhi wanajeshi tisa wa Ukraine.
Waasi wanaoudhibiti mji wa Slaviansk pia walivishambulia vikosi vya Ukraine katika mji wa Karachun kwa mizinga na kwa kuvurumisha maguruneti.
Mashambulizi ya waasi yazimwa
Msemaji huyo wa serikali Vladyslav Seleznyov amesema mashambulizi yote hayo yamezimwa na kwamba hakuna maafa kwa upande wa wanajeshi wa Ukraine wakati idadi ya wapiganaji wa waasi waliouwawa inayakinishwa.
Vikosi vya Ukraine pia vimezima mashambulio mawili yaliofanywa na takriban wapiganaji hamsini wenye silaha nzito mapema asubuhi katika kambi ya anga ya Avdiyivka ambayo ina makombora yanayofyatuliwa kutoka ardhini kwenda angani hakuna maafa yaliyoripotiwa kwa upande wa wanajeshi wa Ukraine katika mashambulizi hayo.
Waasi ambao waliviteka vituo muhimu katika miji mikubwa ukiwemo wa Donetsk na kuunda "jamhuri za wananchi" wakisema wanataka kujiunga na Urusi wamesema Ukraine imekiuka yenyewe mpango huo wa kusitisha mapigano.
Pavel Gubarev kiongozi mashuhuri wa waasi amekaririwa akisema aidha wanajeshi wa Ukraine hawamtii Poroshenko au rais huyo anadanganya.
Waasi wazidi kuvinjari
Katika mji wa Donetsk takriban wapiganaji 100 wa Jamhuri ya Wananchi wa Donetsk iliojitangazia kujitenga walikula kiapo cha utii katika ishara ya wazi ya kuukata mpango wa amani wa Poroshenko.
Katika hafla iliofanyika kwenye uwanja wa Lenin mjini humo, wapiganaji hao wenye silaha wengine wakiwa na vibandiko usoni wameahidi kuihami Jamhuri ya Watu wa Donetsk hadi tone la mwisho la damu.
Walipiga mayowe kwa pamoja "Tunaapa,tunaapa,tunaapa".
Wanajeshi wa ulinzi wa mpakani wa Ukraine katika wiki za hivi karibuni walivisalimisha vituo kadhaa vya mpakani kufuatia mashambulizi ya waasi wanaotaka kujitenga.
Serikali ya Ukraine imeishutumu Urusi kwa kufanikisha uingizaji wa silaha na wapiganaji wa kujitolea kuingia Ukraine kwa kupitia mpaka wake na nchi hiyo.
Urusi yatakiwa itowe ushirikiano
Waziri wa Mambo ya nje wa Ujerumani Frank- Walter Steinmeier
(kushoto) na mwenzake wa Uturuki Ahmet Davutoglu (kulia) katika mkutano
na waandishi wa habari Istanbul. (20.06.2014)
Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Frank -Walter Steinmeier
akizungumza akiwa ziarani mjini Istanbul Uturuki amesema ni muhimu sasa
kwa Urusi kutowa ushirikiano wake kwa mpango huo wa kusitisha mapigano
kwa kutumia ushawishi wake kwa waasi na kuongeza kwamba ulinzi wa mpaka
kati ya Ukraine na Urusi hauna budi kuimarishwa.Rais Poroshenko yuko katika harakati za kidiplomasia kushinikiza kukubalika kwa mpango wake huo lakini changamoto kubwa itakuwa ni kupata ridhaa ya Rais Vladimir Putin wa Urusi.
Uhusiano kati ya nchi hizo mbili uko katika hali mbaya sana wakati Ukraine ikiishutumu Urusi kwa kuchochea machafuko mashariki ya nchi hiyo.