Kerry ziarani Mashariki ya Kati
http://samchardtz.blogspot.com/2014/06/kerry-ziarani-mashariki-ya-kati.html
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry amekuwa na mazungumzo na
Rais Abdel Fatah al- Sisi mjini Cairo na kuyahimiza mataifa ya Kiarabu
kutowagharamia wapiganaji wa Kisunni walioko mpakani mwa Syria na Iraq.
John Kerry Waziri wa Mambo ya nje wa Marekani (kushoto) na Rais Abdel Fatah al-Sisi wa Misri (kulia) mjini Cairo.(22.06.2014)
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry Jumapili (22.06.2014)
amekuwa na mazungumzo na Rais Abdel Fatah al- Sisi mjini Cairo na
kuyahimiza mataifa ya Kiarabu kutowagharamia wapiganaji wa Kisunni
walioko mpakani mwa Syria na Iraq.Kerry ni afisa wa ngazi ya juu wa Marekani kutembelea Misri tokea Sisi mkuu wa zamani majeshi aliyempinduwa Rais Mohamed Mursi kufuatia vuguvugu la maandamano ya umma mwaka jana ashinde katika uchaguzi wa rais nchini humo hapo mwezi wa Mei.
Akizungumza baada ya kukutana na Rais Sisi amesema kuwasaidia wapiganaji wa Kisunni hatimae kutakuja kuusambaza mzozo wa Iraq na kwamba kundi la Dola la Iraq na Sham ni tishio kwa Mashariki ya Kati nzima.
Ziara yake inakuja siku moja baada ya mahakama ya Misri kuthibitisha hukumu za kifo kwa wanachama 183 wa Udugu wa Kiislamu akiwemo kiongozi wao Mohamed Badie katika kesi ya pamoja kwa madai ya kuhusika na ghasia zilizopelekea kuuwawa kwa polisi mmoja.
Serikali ya Rais Barack Obama wa Marekani imesema ina shauku ya kushirikiana na serikali ya Sisi lakini imeelezea wasi wasi wake kutokana na kuenea kwa vitendo vya uvunjaji wa haki za binaadamu na udhibiti wa uhuru wa kujieleza nchini humo.
Wakati muhimu kwa Misri
John Kerry Waziri wa Mambo ya nje wa Marekani(kushoto) na mwenzake wa Misri
Sameh Shoukri (kulia) mjini Cairo.(22.06.2014)
Kerry amesema kabla ya kukutana na waziri mwenzake wa Misri
Sameh Shukri kwamba huu ni wakati muhimu wa mabadiliko nchini Misri
ambayo inakabiliwa na changamoto kubwa na kwamba kuna mambo yanayowatia
wasi wasi lakini wanajuwa namna ya kuyashughulikia.Kwa mujibu wa taarifa ya wizara ya mambo ya nje ya Misri Shukri amemwambia Kerry kwamba uhusiano kati ya Marekani na Misri unapaswa uwe chini ya msingi wa kuheshimiana na maslahi ya pamoja bila ya kuingilia kati masuala ya ndani ya nchi.
Afisa mwandamizi wa wizara ya mambo ya nje wa Marekani amesema serikali ya nchi hiyo ilikuwa na wasi wasi juu ya mbinu za matumizi ya nguvu za kisiasa na kiusalama za serikali ya nchi hiyo ambapo amesema zinaigawa jamii ya Misri.
Marekani ambayo imekuwa ikiitegemea Misri kama mshirika wake wa karibu Mashariki ya Kati kwa miongo kadhaa kufuatia mkataba wa amani wa mwaka 1979 na Israel mshirika wa Marekani ilisitisha sehemu ya msaada wa kijeshi wa kila mwaka wa dola milioni 1.3 kwa Misri kufuatia kupinduliwa kwa Mursi.
Msaada wa kijeshi
Kama dola milioni 575 zilizokuwa zimesitishwa zimeanza kutolewa siku 10 zilizopita na zitatumika kugharamia mikataba ya ulinzi iliopo hivi sasa.Marekani pia imesema itaipatia nchi hiyo helikopta kumi za mashambulizi za aina ya Apache kuwasaidia wanajeshi kupambana na wanamgambo katika rasi ya Sinai.
Utawala wa Obama umesema wazi kwamba fedha zilizobakia ambazo zinahitaji ridhaa ya bunge zitatolewa mara patakapokuwepo ushahidi kwamba serikali ya Sisi inachukuwa hatua zaidi kuelekea demokrasia.
Afisa wa serikali ya Marekani amesema haiamini kwamba Udugu wa Kiislamu ulikuwa tishio kwa Misri na haikuona taarifa ya ushahidi unayoihusisha na makundi ya kigaidi.
Tishio la mzozo wa Iraq
Ziara ya Kerry pia itamfikisha Jordan wakati vikosi vya serikali nchini Iraq vikijaribu kuwarudisha nyuma waasi wa itikadi kali wa Kisunni walioteka miji kadhaa vimefanya mashambulizi ya anga kwa mji wa Tikrit na kuuwa watu saba.
Kushambuliwa kwa mabomu kwa mji huo ukiwa ni mmojawapo ya miji kadhaa ambayo serikali imepoteza udhibiti wake tokea waasi walipoanzisha mashambulizi yao hapo Juni tisa yanakuja siku moja baada ya wapiganaji wa Kishia kuandamana mjini Baghdad kuonyesha uwezo wao dhidi ya wapinzani wao wa Kisunni.
Juhudi mpya za kidiplomasia za Marekani zina lengo la kuwaunganisha viongozi wa Iraq waliogawika na kuwatokomeza waasi ambao mashambulizi yao ya karibuni yamepelekea maelfu ya watu kupoteza makaazi yao, kuifadhaisha jumuiya ya kimataifa na kumuweka Waziri Mkuu Nuri al-Maliki chini ya shinikizo linaloongezeka.
Wakati viongozi wa Marekani hawakumtaka moja kwa moja al Maliki ajiuzulu kwa kusema kwamba ni haki ya wananchi wa Iraq kuchaguwa viongozi wao, hawakuficha hisia zao kwamba waziri mkuu huyo wa Kishia amevuruga fursa ya kuijenga upya nchi yake tokea vikosi vya Marekani vilipoondoka nchini humo mwaka 2011.