TAMKO LA ASKOFU KUHUSU MLIPUKO WA BOMU KANISANI MWANZA
http://samchardtz.blogspot.com/2014/05/tamko-la-askofu-kuhusu-mlipuko-wa-bomu.html
SIKU
moja baada ya kulipuka kwa bomu katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri
Tanzania (KKKT) Usharika wa Imani, Dayosisi ya Mashariki Ziwa Victoria,
Askofu wa kanisa hilo, Andrew Gulle, ameitaka serikali kutumia nguvu
zake kupambana na watu wanaohatarisha amani na usalama wa nchi.
Askofu Galle alisema waliohusika na tukio hilo ni magaidi, na kwamba
vyombo vya dola vinapaswa kutumia uwezo wake wote kuhakikisha matukio ya
aina hiyo hayaendelei kutokea nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa jana, alisema matukio ya
kulipuliwa kwa mabomu katika nyumba za ibada, hususan za Wakristo
yanaanza kushamiri, huku vyombo vya dola vikishuhudia.
Hata hivyo,
alisema ingawa tukio hilo limewasikitisha na kuwaumiza waamini wengi,
aliwataka watulie, wasiogope wala wasitishike na mashambulizi
yaliyotendeka wala kulipiza kisasi, bali waache suala hilo
lishughulikiwe na vyombo vya serikali.
“Ninatoa wito kwa Wakristo
wetu wote wawe watulivu, wasiogope wala wasitishwe na mashambulizi
haya, na kusitokee fujo wala kulipiza visasi, bali sisi tuzame na
kuongeza nguvu katika maombi na kumtegemea Mungu,” alisema.
Katika
hatua nyingine, uchunguzi umebaini kuwa bomu hilo lililotengenezwa
kienyeji, lililotegwa kanisani hapo Ijumaa wiki iliyopita, liliwekwa
ndani ya bahasha na kufungwa kama zawadi na kuwekwa kwenye mfuko wa
nailoni.
Imedaiwa mhudumu wa kanisa hilo, Benadetha alichukua
mfuko huo ili aone kilichokuwemo, na ndipo akalipukiwa na bomu
lililomjeruhi.
