Flatnews

HALI ETE ZANZIBAR: MAKUNDI YA ASKARI YAJIANDAA KUVAMIA OFISI KUU ZA CHAMA CHA WANANCHI (CUF)

                               MAKUNDI ya askari wanaotajwa kama kutoka vikosi vya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar wakichanganyika na vija...


                               Askari wa Vikosi vya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar wakiwa katika moja ya poresheni zao
MAKUNDI ya askari wanaotajwa kama kutoka vikosi vya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar wakichanganyika na vijana wasiokuwa na mafunzo halisi ya kiaskari wamekuwa wakihaha kutaka kuvamia ofisi kuu za Chama cha Wananchi (CUF) mjini hapa. Anaandika Jabir Idrissa, Zanzibar … (endelea).
Uongozi wa chama hicho umeiambia MwanaHALISI Online leo kwamba baada ya askari hao wanaoitwa kwa umaarufu kwa jina la “Mazombi,” kushindwa kuvamia ofisi za Makao Makuu zilizoko mtaa wa Vuga, katikati ya Mji Mkongwe, juzi, jana usiku walijaribu kuvamia Makao Makuu yaliyopo mtaa wa Mtendeni.
Taarifa zilizotolewa na Ofisi ya Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano ya Umma wa CUF, zimesema askari wengi walifika Mtendeni usiku wa manane na kuwateka walinzi waliokuwa nje ya ofisi.
Walihangaika kutaka kuwalazimisha kufungua mlango lakini waliwekewa ngumu kwa walinzi walioko nje kusema hawana mamlaka hayo kwa kuwa wao walisema, “mamlaka yetu ni kulinda nje.”
Mwandishi wa habari hizi alifahamishwa kuwa mazombi waliokuwa wamebeba silaha za moto na za jadi, mara kadhaa walisukuma mlango mkuu wa jengo la makao makuu bila ya mafanikio.
Waliamua kupayuka wakitoa amri kwa walinzi waliokuwa ndani ya jengo kuwa wafungue au watavunja, lakini hawakuzingatiwa.
Watu wanaoishi jirani na makao makuu ya CUF, ambao walikuwa wakifuatilia kilichoitwa na baadhi yao kama “sinema ya usiku” wamesema walishuhudia mazombi wakipiga kelele kutaka wafunguliwe mlango.
“Niliwasikia wanataka walioko ndani watoke watano watano, lakini kutokea ndani nikawa nasikia mtu akisema hatoki mtu na atakayevunja na kuingia atakula naye sahani moja,” amesema shuhuda.
“Nasema hatoki mtu na atakayeingia ndani atakuwa mali yangu,” shuhuda amesema akimnukuu mtu aliyekuwa ndani ya ofisi hizo.
Zogo lilitulia pale walipofika askari wa kikosi cha kuzuia ghasia (FFU) ambao taarifa zinasema waliamrishwa na IGP Ernest Mangu aliyepigiwa simu kutoka mjini hapa kuarifiwa kuhusu tukio hilo.
Taarifa za ndani zinasema IGP Mangu alichukua hatua baada ya kupata taarifa kutoka kwa uongozi wa juu wa CUF kwa kuwa haukuamini kama wangepata msaada wa maana kwa Kamishna wa Polisi Zanzibar (CPZ), Hamza Omar Makame.
Askari wa FFU walifika ndani ya magari mawili na kuharakia kuwatimua. Mazombi walipobaini sauti za magari yakienda kwa kasi walipata hofu na kuitana na kukubaliana kuondoka.
Siku mbili zilizopita, mazombi ambao wamekuwa wakisababisha usumbufu kwa wananchi kwa kuwavamia majumbani na kuwapiga, walikwenda ofisi za Vuga na kujaribu kuzivamia waingie ndani, lakini hawakufanikiwa. Ofisi zote zinalindwa na walinzi wa chama chenyewe, wakiwemo wenye mafunzo ya kijeshi kwa kuwa wapo waliofukuzwa kazi vikosi vya serikali.
Taarifa hizi zinakuja wakati ikifahamika kuwa askari hao walivamia ofisi kuu za Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) na kutapanya makaratasi waliyoyakuta.
Kwa mujibu wa vyanzo vya habari, askari hao wamekuwa wakitafuta nyaraka zinazohusu matokeo ya uchaguzi wa rais, lengo likihisiwa kuwa ni kuyapeleka kwa uongozi wa juu wa CCM.
Kulikuwa na taarifa kwa siku kadhaa kwamba CCM ilituma mawakala wake wa Idara ya Usalama wa Taifa kisiwani Pemba ili kuwapata mawakala wa uchaguzi upande wa CUF na kuwasainisha fomu za matokeo yasiyokuwa sahihi.
Chanzo cha habari ndani ya Serikali na CCM kimesema baada ya kutofanikiwa kumpata hata wakala mmoja, CCM ilifuta mpango wa kutaka kuchezea matokeo ili kulazimisha Tume imtangaze Dk. Ali Mohamed Shein kuwa ndiye mshindi, na ikaagiza kutumika kwa nguvu ambapo ndiyo akashuhudiwa Mwenyekiti wa ZEC, Jecha Salim Jecha akitangaza taarifa ya kufuta uchaguzi akidai “umeharibika.”
Jecha ambaye amelalamikiwa kukimbia kazi kwa siku mbili mfululizo, Oktoba 26 na 27, alitangaza Oktoba 28 kufutwa kwa uchaguzi wote Zanzibar na kwamba utarejewa.
Wanaojua wanasema alichukuliwa kwa nguvu na kupelekwa Ofisi Kuu za ZEC Maisara, mjini hapa, na kurekodiwa akisoma tamko linalotajwa kuwa hakuliandika yeye wala ofisa yeyote wa Tume.
Tayari Mwenyekiti Jecha amerudi kazini lakini jana aliripotiwa kuanza vibaya kikao na makamishna kwa kuwa alifanya ushawishi kuwa wamuunge mkono kwa hoja yake hiyo ya kufuta uchaguzi.
“Unaloniuliza ni kweli. Alifika ofisini na kukutana na wenzake lakini akaanza vibaya kwa kuwashawishi makamishna wamuunge mkono. Walimkatalia kwa sababu wameshindwa kupata kifungu cha sheria cha kuridhia ufutaji wa uchaguzi,” amesema mtoa taarifa ndani ya Tume ya Uchaguzi.
Wanasheria wametaka Jecha achukuliwe hatua za kisheria kwa kuundiwa tume ya majaji kuchunguzwa kuhusu kitendo alichokifanya ambacho wanaamini ni “uvunjaji wa katiba wenye kuashiria kusababisha machafuko nchini.”
Kadhia yote hii imetokana na kitendo cha Jecha aliyetoa tangazo lake akiwa ameshatoa matokeo asilimia 70, siku ya mwisho akisubiriwa kumaliza ili atangazwe mshindi wa urais.
Jumatatu ya Oktoba 26, Mgombea urais wa CUF, Maalim Seif Shariff Hamad, aliwaambia waandishi wa habari kuwa mwelekeo wa kura ulionesha amepata kura nyingi kiasi cha asilimia 52.87 dhidi ya 47.13 za Dk. Shein na kutaka Tume isicheleweshe kutangaza matokeo.
Alisihi CCM wakubali na akamuomba Dk. Shein naye aridhie kama alivyoridhia yeye mwaka 2010, kukubali matokeo ya kushindwa uchaguzi, ili washirikiane kujenga nchi.
Kumekuwa na jitihada zinazoongozwa na Jumuiya ya Kimataifa hapa kutaka kurejesha utaratibu wa kukamilisha kazi ya kujumuisha na kutangaza matokeo ya kura zilizobaki katika majimbo 22, baada ya majimbo 32 kutangazwa tayari na Jecha mwenyewe kupitia kituo cha utangazaji wa matokeo kilichofadhiliwa na ofisi ya Umoja wa Mataifa nchini Tanzania.

Related

NEWS 3311392410993987029

Post a Comment

emo-but-icon

item