HAWA NDIO WANAUME WANAOMNYAMAZISHA ROONEY NA TAIFA LAKE KWA REKODI ALIYOIWEKA JUZI
Wiki hii vyombo vingi vya habari vya Uingereza na mataifa yote yaliyo chini ya jumuiya ya madola yalitawaliwa na habari moja pekee...
https://samchardtz.blogspot.com/2015/09/hawa-ndio-wanaume-wanaomnyamazisha.html
Wiki hii vyombo vingi vya habari
vya Uingereza na mataifa yote yaliyo chini ya jumuiya ya madola
yalitawaliwa na habari moja pekee. Nadhani kwa unayefuatilia michezo
utakuwa una fahamu kuwa stori ya Wayne Rooney kufikisha magoli 50 na
hatimaye kuwa mfungaji bora wa
muda wote kwenye taifa lake ndiyo
iliyotawala hadi watu kusahau habari za Lowasa na Magufuli. Binafsi
nilidhani Rooney hakupaswa kujisifia kwani kuna watu wa kizazi chake
kutoka nchi zingine ambao wamefanya makubwa na wanatarajiwa kuitikisa
dunia kwa kufunga magoli mengine mengi ndani ya miaka ijayo kama
Mwenyezi atawaepusha na majeraha.
Rooney ana miaka 12 kwenye uzi wa
timu ya taifa lake huku akiwa na magoli 50. Huu ni wastani wa magoli 4
kwa mwaka huku yeye akiwa na faida ya kuitwa mara zote tangu 2003 na
kutofungiwa mara kibao kama akina Suarez. Rooney kwa sasa ana miaka 29
na kutokana na kutotabirika kwa kiwango chake inawezekana akacheza
misimu 4 ijayo kwenye taifa lake hivyo kuwa na magoli 16 na hatimaye
kustaafu akiwa akiwa na magoli yasiyozidi 65. Naamini baada ya kutoka
Urusi kwenye kombe la dunia mwaka 2018, Rooney atastaafu.
Pia Rooney atakwenda Urusi akiwa
tayari yupo hoi katika idara ya ushambuliaji na huenda akaenda kama
kiungo na sio mshambuliji, hii ni kutokana na uwepo wa vijana kama akina
Kane, Sturidge na Sterling. Kutokana na Waingereza kujisifia kwa
kitendo cha Rooney leo nakupa ushahidi wa wachezaji 5 wa kizazi cha
Rooney ambao wamefanya makubwa na takwimu zinaonesha watafanya makubwa
sana miaka ijayo kabla hawajastaafu na kudhihirisha taifa la Uingereza
lina mpira wa
magazetini na kwenye ngazi ya kimataifa bado sana……..
magazetini na kwenye ngazi ya kimataifa bado sana……..
LIONEL MESSI
Ni mshambuliaji wa Klabu ya
Barcelona, kwa sasa ana miaka 28. Alianza kuonekana kwenye uzi wa timu
ya taifa ya Argentina tangu mwaka 2005 hivyo hadi sasa ana miaka 10
kwenye timu yake ya taifa. Kwa sasa ana jumla ya magoli 49 katika
michezo 105 aliyocheza. Ukipiga hesabu hapo jamaa ana wastani wa kufunga
magoli 5 kila mwaka. Kwa kiwango chake ni wazi kuwa jamaa bado ana
miaka 6 ya kucheza kwenye timu ya taifa, kwa wastani huu wa magoli 5 kwa
mwaka, Messi atafunga magoli yanayokadiriwa kufika 30 kwenye miaka yake
ijayo ya kucheza soka hivyo kustaafu akiwa na magoli takribani 80.
Kama hatoandamwa na majeraha
inawezekana Messi akaonekana kwenye timu ya taifa lake akiwa na miaka 34
japokuwa hatopewa nafasi ya mara kwa mara ila bado ataitwa kama mkongwe
wa kikosi. Takwimu hizi zinazidi kumdidimiza Rooney na Uingereza
kubakia kama taifa la kawaida sana kisoka.
NEYMAR JUNIOR
Ni mshambuliaji wa zamani wa
Klabu ya Santos ila kwa sasa anakipiga pale FC Barcelona. Neymar ameanza
kuonekana kwenye timu ya Selecao tangu mwaka 2010. Kwa sasa ana miaka
23 ila tayari amecheza michezo 67 pekee huku akifunga magoli 46. Kwa
hesabu za haraka ni kwamba jamaa ana wastani wa magoli 9 kila mwaka. Ni
wastani mkubwa sana kwa kizazi cha leo kwani kutokana na uwezo wake
mkubwa, Neymar bado ana miaka takribani 10 ya kuonekana kwenye uzi wa
Njano na Bluu. Kwa wastani wake wa magoli 9 kwa mwaka, Neymar
anakadiriwa kutupia magoli
yasiyopungua 90 miaka ijayo.
yasiyopungua 90 miaka ijayo.
Kutokana na majeraha na umri
kusogea hivyo kiwango kushukuka tuna ‘assume’ Neymar atafunga nusu ya
magoli hayo, 45. Magoli haya bado ni mengi sana, kitu ambacho Waingereza
wataendelea kukiota hadi kesho na kudhihirisha wamezidiwa kisoka na
mataifa mengine duniani.
THOMAS MULLER.
Ni mchezaji anayecheza kwa jihadi
sana uwanjani. Kwa sasa yupo pale Bayern Munich na kwa upande wangu
huyu ndio mchezaji bora wa Bayern kwa sasa kutokana na moyo wake wa
kujituma na kucheza kwa jihadi. Muller ana miaka 25 na alianza kuonekana
kwenye timu ya taifa tangu 2010. Hadi sasa amecheza michezo 65 huku
akitupia magoli 30. Jaribu kupiga hesabu utagundua jamaa ana wastani wa
kutupia magoli 6 kila mwaka. Umri wake utamruhusu kucheza miaka 8 ijayo
kama hatopata majeraha. Kwa wastani huu ni wazi Muller anatarajiwa
kufunga magoli yasiyopungua 48 na hatimaye kustaafu akiwa na magoli
yasiyopungua 80.
Kutokana na uwezo wake naamini
Muller atayafikia haya magoli mapema kabla hajatundika daluga. Muller
pia anatarajiwa kuvunja rekodi ya Miroslav Klose ya kuwa mfungaji wa
kombe la dunia wa muda wote. Kitendo hiki kitazidi kuonesha kuwa
Ujerumani ni taifa lililoiacha mbali Uingereza katika ngazi ya
kimataifa.
LUIS SUAREZ
Ni mshambuliaji namba 9 hatari
kwa sasa duniani ukimuacha Kuni Aguero. Huyu jamaa alifungiwa mechi
kibao kutokana na tabia yake isiyotabirika. Suarez kwa sasa ana miaka 28
na ameshacheza michezo 82 huku akifunga magoli 43. Alianza kuonekana
kwenye timu yake ya taifa tangu mwaka 2007. Ukikokotoa vizuri utagundua
jamaa ana wastani wa kufunga magoli 5 ila wastani huu utakuwa ni wa
kumuonea kwani amekosa mechi kibao kutokana na kufungiwa na FIFA. Kama
tabia mbovu na majeraha havitomuandama, ni wazi kuwa Suarez ana miaka 6
ya kucheza Uruguay kama walivyofanya nyota wengine wa Uruguay hapo
nyuma.
Kutokana na wastani wake wa
kutupia magoli 5 kwa mwaka, Suarez anakadiriwa kufunga magoli
yasiyopungua 30 kipindi kijacho hivyo kufikisha magoli karibu 80. Kama
atakuwa vizuri kiafya, rekodi hii itatimia kwani huyu jamaa ni hatari
sana akicheza kati. Hali hii itazidi kudhihirisha kuwa Waingereza wana
mpira wa magazeti na kwenye ngazi ya kimataifa wanazidiwa na taifa dogo
kabisa kama hili.
CRISTIANO RONALDO
Hii ni mashine ya kutoa magoli.
Jamaa anafunga pale anapoamua kufunga. Ni hatari sana hasa pale
anapocheza na timu yangu na huwa nachukia sana akipewa pasi kwani
ameshanichania ‘mikeka’ kibao. Kwa sasa yupo Real Madrid na ana miaka
30. Ameshacheza michezo 122 tangu 2003 kwenye timu ya taifa lake huku
akitupia magoli 55. Kwa hesabu za kugawanya utagundua huyu jamaa ana
wastani wa magoli karibu 5 kwa mwaka. Ronaldo bado ana miaka 4 ya
kucheza timu ya taifa kama hatotangaza kustaafu mapema. Kutokana na
wastani huu ni wazi CR7 anatarajiwa kufunga magoli yasiyopungua 20 baada
ya kombe la dunia nchini Urusi.
Kutokana na moyo wake wa kujituma
na nidhamu nzuri aliyonayo, nina imani fundi huyu atatimiza magoli 70
hadi 80 kwenye taifa lake na kumkalisha Rooney na taifa lake ambalo soka
lao limebaki kwenye magazeti.
