Wakubwa waunga mkono kazi ya Jopo la Rais Kikwete
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa Linalopendekeza Jinsi Dunia inavyoweza kukabiliana n...
https://samchardtz.blogspot.com/2015/07/wakubwa-waunga-mkono-kazi-ya-jopo-la.html
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa
Linalopendekeza Jinsi Dunia inavyoweza kukabiliana na majanga yajayo ya
magonjwa ya milipuko, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, Jumatano, Julai
15, 2015, ameongoza vikao vya Jopo hilo ambalo kazi yake imeungwa mkono
na nchi 21 ambazo zilichangia mapambano dhidi ya ugonjwa wa Ebola.
Miongoni
mwa mikutano ambayo Rais Kikwete ameiongoza katika Makao ya Umoja wa
Mataifa (UN) mjini Geneva ni pamoja na yeye na wanajopo wenzake kutoa
maelezo kuhusu maendeleo ya kazi yao kwa nchi ambazo zilichangia
mapambano dhidi ya ugonjwa wa Ebola katika nchi za Guinea, Liberia na
Sierra Leone.
Nchi
hizo ambazo zimeonyesha kuunga mkono kazi ya Jopo hili katika mkutano
huo ni Venezuela, Umoja wa Ulaya (EU), Uholanzi, Finland, Shirikisho la
Russia (Russian Federation), Norway, China, Ubelgiji, India, Ujerumani,
Marekani, Uswisi, Canada, Brazil, Denmark, Uingereza, Israel, Benki ya
Maendeleo ya Afrika (AfDB), Umoja wa Afrika (AU), Benki ya Dunia (WB),
Jamhuri ya Korea na Japan.
Pamoja
na kwamba wajibu mkuu wa Jopo hili siyo kuchunguza ugonjwa wa Ebola na
madhara yake, bado ugonjwa huo ni msingi mkuu wa kazi ya Jopo hilo
ambalo wajibu wake ni kutumia uzoefu wa Ebola kutoa mapendekezo ya jinsi
dunia inavyoweza kukabiliana na majanga ya magonjwa ya milipuko katika
siku zijazo.
Ugonjwa
wa Ebola ambao ulilipuka katika nchi hizo tatu za Afrika Magharibi
mwishoni mwa mwaka 2013 mpaka sasa umeua watu 11,000 katika nchi hizo na
kusababisha mshtuko mkubwa duniani.
Hiyo
ilikuwa mara ya 24 kwa ugonjwa huo kulipuka katika Afrika tokea
ulipolipuka kwa mara ya kwanza mwaka 1976, miaka karibu 40 iliyopita,
katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) wakati huo ikiitwa Zaire.
Hata hivyo, katika milipuko ya kwanza 23, ugonjwa huo uliua watu wachache zaidi kuliko mlipuko wa 24.
Jopo
hilo limeambiwa kuwa tofauti na matarajio ya dunia kuwa ugonjwa huo
ulikuwa unamalizika katika nchi hizo hasa katika Liberia, umeanza kupata
kasi tena na nchi hizo tatu zinakisiwa kuwa na wagonjwa karibu 70.
Jopo
hilo lenye Wajumbe sita liliteuliwa Aprili, mwaka huu, na Katibu Mkuu
wa Umoja wa Mataifa, Mheshimiwa Ban Ki Moon na kufanya vikao vyake vya
mwanzo Mei, mwaka huu, katika makao makuu ya UN, mjini New York,
Marekani.
Mbali
na kukutana na nchi zilizochangia mapambano dhidi ya Ebola, Rais
Kikwete na Jopo lake limepata nafasi ya kumsikiliza aliyekuwa Mkurugenzi
wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Kanda ya Afrika, wakati ugonjwa huo
unalipuka Dkt. Luis Gomes Sambo wa Angola ambaye aliwaeleza wajumbe
historia ya ofisi ya kanda hiyo iliyoko mjini Brazzaville, Jamhuri ya
Congo, katika kukabiliana na ugonjwa huo.
Aidha,
Wajumbe wa Jopo wamemsikiliza Mkurugenzi mpya wa Kanda, Dkt. Matshidizo
Rebecca Moeti ambaye amezungumza kwa njia ya mkutanomtandao
(teleconference) kutoka mjini Brazzaville. Dkt. Moeti alianza kazi yake
Januari Mosi, mwaka huu, 2015.
Vile
vile, Wajumbe wa Jopo wamesikiliza jitihada za Jamhuri ya Rwanda
kukabiliana na magonjwa ya mlipuko kupitia kwa Waziri wa Afya wa nchi
hiyo, Agnes Binagwaho ambaye naye alizungumza kwa mkutanomtandao kutoka
Kigali, Rwanda.
Nje
ya vikao hivyo, Rais Kikwete amekutana na kufanya mazungumzo na Katibu
Mkuu Mstaafu wa UN, Mheshimiwa Kofi Annan. Katika mkutano huo kwenye
Hoteli ya Intercontinental, viongozi hao wawili wamezungumzia masuala
mbali mbali ya kimataifa, ikiwamo hali ya Burundi.
Rais
pia amekutana kwa mazungumzo na Mtendaji Mkuu wa Kituo cha South Centre
ambacho kina makao yake mjini Geneva, Dkt. Martin Kohr. Kituo hicho
kilianzishwa chini ya uongozi wa Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, kwa nia
ya utekelezaji wa Ripoti ya Kamisheni ya Nchi Zinazoendelea (South-South Commission), ambayo iliongozwa na Mwalimu.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
16 Julai, 2015