Madiwani kwa Lowassa wasusa.....Kata zao zakosa Wagombea, Wasema Wanasubiri Tamko la Lowassa
Kasi ya wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kuomba nafasi za udiwani na ubunge katika Jimbo la Monduli, inasuasua na tayari...
https://samchardtz.blogspot.com/2015/07/madiwani-kwa-lowassa-wasusakata-zao.html

Kasi ya wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kuomba nafasi za udiwani na ubunge katika Jimbo la Monduli, inasuasua na tayari chama hicho kimeitisha kikao cha dharura cha Kamati ya Siasa kitakachokutana leo kukuna vichwa kutafuta ufumbuzi wa hali hiyo.
Katibu
wa CCM Wilaya ya Monduli, Elisante Kimaro, alisema jana kuwa kusuasua
kwa wanachama kuchukua fomu za kuomba kugombea nafasi hizo kunatokana na
kushuka kwa morali ya wanachama baada ya Mbunge wa zamani, Edward
Lowassa, aliyekuwa akiwania kuteuliwa na chama chake kugombea urais,
kukatwa jina lake.
“Zoezi la uchukuaji wa fomu za udiwani linasuasua, lilianza juzi na siku ya mwisho ni Julai 19, mwaka huu saa 10 jioni.
“Zoezi
hili ni gumu sana, hata hivyo bado ni mapema sana kutoa taarifa, lakini
morali ya wanachama kuchukua fomu za kuomba kugombea imepungua,” alisema.
Alisema
ameitisha kikao cha dharura cha Kamati ya Siasa chenye wajumbe 16
kuzungumzia suala hilo ili kwa pamoja wahamasishe wanachama kugombea.
“Tunawahimiza wanachama wajitokeze kuchukua fomu za kugombea nafasi hizo,” alisema na kuongeza: “Hili jimbo ni ngome ya CCM na wala sina shaka na hilo.”
Alisema
kusuasua huko kunatokana na baadhi ya madiwani waliomaliza muda wao
kufanya propaganda ya kuwazuia wanachama kwenda kuchukua fomu kwa madai
kwamba wasubiri kwanza kauli ya mbunge wao.
“Baadhi
ya madiwani wa zamani wanatengeneza propaganda, hawa ni madiwani wale
ambao hawakubaliki katika kata zao…wanawahamasisha watu wasichukue fomu
kwa kigezo kwamba wasubiri kauli ya Mbunge Lowassa, jambo ambalo siyo
kweli," alisema.
Aliongeza: “Lowassa
hajawahi kufanya kitu kama hicho cha kuwaambia wanachama wasichukue
fomu hadi atakapotoa kauli yake…jana (juzi), alikuja hapa Monduli
kujiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, hakutamka lolote,
alisema tu hana la kusema.”
Alisema watu hao wanatumia mgongo wa Lowassa kueneza propaganda.
Alisema
kwa upande wa ubunge hadi sasa amejitokeza mwanachama mmoja tu, Mbayani
Tayayi, aliyechukua fomu yake jana saa 4:00 asubuhi, wakati kwa upande
wa udiwani waliochukua fomu ni mwanachama mmoja mmoja katika kata za
Mswakini, Lepurko na Engutoto.
Pamoja na kusuasua huko, Kimaro alisema atahakikisha kata zote 20 zinapata wagombea wa udiwani na kumpata mgombea ubunge.
Alizitaja
kata hizo kuwa Engaruka, Engutoto, Esilalei, Lepurko, Loksale, Majengo,
Makuyuni, Meserani, Nalalani, Lemooti, Moita, Monduli Juu, Monduli
Mjini, Mfereji, Mswakini, Mto wa Mbu, Migungani, Selela, Sepeko na
Lashaini.
Alisema
tangu kumalizika kwa mchakato kupata mgombea ndani ya chama hicho Julai
12, mwaka huu, mjini Dodoma ambapo jina la Lowassa lilikatwa katika
mazingira ya kutatanisha, kumekuwa na maneno mengi yakisambaa kwenye
mitandano ya kijamii kwamba Lowassa anakihama chama hicho.
“Hizi habari si za kweli, bado tuna imani na Lowassa,” alisema.
Alisema mchakato wa kumpata mgombea ndani ya chama hicho tayari umemalizika kwa kumpata mgombea wake, Dk. John Magufuli.
Hali ilivyo:
Baadhi
ya wakazi mjini Monduli walisema kitendo cha kuenguliwa kwa mbunge wake
katika kinyang’anyiro cha urais, kimewavunja moyo kwa maelezo kuwa
utaratibu haukufanyika kwa haki.
Walisema
wanahamasishana kuwapigia kura wagombea watakaosimamishwa na vyama vya
upinzani wakidai CCM imefia mikononi mwa Mwenyekiti wao wa Taifa.
Katika
kituo cha mabasi cha Monduli, wapiga debe walikuwa wakiwataka abiria
ambao ni wanachama wa Chadema kuingia daladala za Arusha zilizopo
kituoni hapo huku wakiwataka abiria ambao ni wanachama wa CCM kwenda
kusubiri magari yao (mashangingi) yaliyopo eneo la CCM.
Wiki iliyopita, CCM walifanya vikao vya uteuzi wa mgombea wao.
Chama
hicho kilimteua Dk. John Magufuli kwa asilimia 87.1 na Samia Suluhu
Hassan, kuwa mgombea mwenza ili kupeperusha bendera ya chama hicho
katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
Mpekuzi blog