BADALA YA UTATUZI, KISOKI NA SPUTANZA SASA WAMEGEUKA TATIZO
KISOKI AKIWA NA MESSI WAKIINGIA KATIKA OFISI ZA TFF... SAKATA la Ramadhani Singano ‘Messi’ na mwajiri wake Simba ndiyo limesh...
https://samchardtz.blogspot.com/2015/06/badala-ya-utatuzi-kisoki-na-sputanza.html
KISOKI AKIWA NA MESSI WAKIINGIA KATIKA OFISI ZA TFF... |
SAKATA la Ramadhani Singano ‘Messi’ na mwajiri wake
Simba ndiyo limeshika anga la michezo, lakini limekuwa suala linalochanganya
sana.
Messi amekuwa akisema mkataba wake na Simba unaisha
mwaka huu lakini Simba inasema ni wa mwaka mmoja zaidi hadi 2016. Hapo ndiyo
utata ulipoanzia.
Mara kadhaa, utawasikia baadhi ya wadau wenye ugomvi
na uongozi wa Simba, wakitoa maoni yao kwa kusukuma lawama kwa uongozi huo kuwa
unafanya utapeli kwa kuongeza mkataba kinyemela.
Wako wenye mapenzi na Simba, wamekuwa wakimlaumu Messi
kwamba anafanya vitu ambavyo vinaonyesha havina mapenzi kabisa na klabu hiyo na
anastahili kuachwa.
Huenda ni kipindi cha kila mmoja kutoa hisia zake kwa
upande wowote, lakini kama watu wangekubali ushauri wangu, huu si wakati
mwafaka wa kumlaumu Messi au Simba kwa kuwa hakuna mwenye uhakika sana.
Chama cha Wanasoka Tanzania (Sputanza), ndiyo walikuwa
watu sahihi wa kueleza tatizo hilo na mwisho kupata usuluhishi wake na
Mwenyekiti wake, Mussa Kisoki ndiye amekuwa akishughulikia. Nilijua mwisho
ungekuwa mzuri kwa kuwa Kisoki ni mtu wa watu wa hatu na mpenda haki.
Lakini baada ya kile kikao kilichoihusisha Simba,
Messi, Sputanza na TFF nikaingiwa hofu kubwa na uwezo wa Sputanza kutetea
maslahi ya wachezaji na huenda badala ya kutetea au kusaidia basi wanaweza
kusababisha tatizo kubwa sana.
Maana baada ya kikao, nilimsikia Katibu Mkuu wa TFF,
Mwesigwa Selestine akizungumza, hakika hakunyoosha mazungumzo. Baadaye akazungumza
Kisoki ambaye alijichanganya zaidi na kunishangaza. Zaidi alisema amefurahishwa
na kilichofanyika siku hiyo na anaunga mkono Messi na Simba kukaa meza moja na
kujadili mkataba.
Dakika chache baadaye alizungumza Messi ambaye alionekana wazi hakuelewa kilichofanyika katika mkutano huo baada ya kusema haelewi kwa makubaliano hayo ni mchezaji huru na kama watashindwa kufikia makubaliano na Simba anakuwa wapi, tayari kujiunga na timu nyingine au anabaki kuwa mchezaji wa Simba!
Kwa maelezo ya Mwesigwa na Kisoki, kweli ilikuwa
inachanganya na utaona kuanzia siku hiyo mitandaoni na siku iliyofuata katika
magazeti, watu waliripoti wanavyojua. Maana ilikuwa vigumu kuelewa, TFF na
Sputanza wakajichanganya na Msemaji wa Simba, Haji Manara akaharibu zaidi
kuzungumza kibabe bila sababu za msingi.
Wakati waandishi wanahoji, walionekana ni tatizo.
Lakini sasa imethibitika kweli kulikuwa na tatizo na Kisoki amekuwa wa kwanza
kusema wanataka suala hilo lisikilizwe tena, maana yake hawatambui kile kikao
cha mwanzo ambacho kilikuwa na makubaliano aliyosema ameyafurahia.
Huu ni uthibitisho hata Kisoki alimaliza kikao akiwa
haelewi lolote lakini alikuwa amefurahishwa. Baadaye alikaa na wenzake
wakamueleza namna ambavyo alikosea.
Kikao kiliisha, Watanzania wapenda soka hawakuelezwa kwamba
je, mkataba wa Messi unaoisha 2015 au ule wa Simba unaofikia tamati 2016, upi
hasa ni sahihi?
Mimi nilibahatika kuona mikataba yote ilikuwa na
matatizo. Herufi kadhaa zilionekana zimechezewa hata kwenye ule mkataba wa
Messi. Hivyo nilipenda kujua mwisho itakuwaje. Inaonekana kila upande huenda
umeona kuna makosa, ndiyo mwanzo wa mkanganyiko mwingine kwa kuwa kauli za
Mwesigwa na Kisoki zilizonyesha wazi kuna jambo linafikichwa kutoka upande wa
Messi, Simba au pande zote.
Sasa Sputanza wameanza mchakato upya, nani ana uhakika
au anawaamini hata makubaliano mengine watasema jambo la uhakika kwa kuwa
anayeshughulikia ni braza Kisoki yuleyule aliyesema amefurahishwa na siku moja
iliyofuatia akayaruka maneno yake na kusema tofauti.